Yameandikwa mengi kuhusiana na mikutano ya chama cha mapinduzi-CCM iliyokwisha hivi karibuni kule kijijini Butiama alikozaliwa na kuzikwa mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere.
Nyoyo zote za watanzania zilikuwa zimeelekezwa Butiama pindi tu CCM ilipotangaza ingefanyia vikao vyake muhimu na vya juu kijijini pale. Wapo waliodiriki hata kusema kuwa CCM ilikuwa inakwenda Butiama kujipanga upya ili angalau kurejesha heshima yake iliyokwisha kumomonyoka. Walikosea sana.
Wapo waliosema kuwa kwenda kwa CCM Butiama ilikuwa ni kwenda kutafuta laana zaidi. Hawa kiasi fulani walipatia. Maana ingawa hayasemwi, kilichofanyika na kutokea Butiama ni aibu na hasara kwa taifa, Mwalimu Nyerere na waliokwenda kule.
Tulitegemea angalau Rais Jakaya Kikwete angewakaripia hata kuwavua uanachama, nyadhifa na kuwachukulia hatua mafisadi wanaojulikana wazi. Lakini halikuwa? Kwanini? Kwa sababu tangu itoke list of shame imekuwa vigumu kumtofautisha Kikwete na mafisadi.
Baya zaidi hata madai dhidi yake ameyanyamazia akijenga hisia kuwa kilichodaiwa ni ukweli kama ilivyokuwa kwa Daudi Ballali, Edward Lowassa, Nazir Karamagi, Ibrahim Msabaha, Basil Mramba na mafisadi wengine bila kumsahau rais mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye umma ungemtaka mahakamani yeye na familia yake na marafiki zake.
Katika utani wangu kwenye gazeti hili chini ya safu ya kijwe nilisema tunakwenda Butiama kuwatambulisha wajasiriamali,wezi na wafanyabiashara wanaoiua CCM na Tanzania.
Hii maana yake ni kwamba hakuna ambalo lingefanyika la maana. Na kweli imekuwa hivyo. Ni kwanini? Kwa sababu:
Mosi, kwa mtu anayemjua Kikwete vizuri na jinsi alivyofika alipo, hakutarajia Kikwete achukue hatua yoyote ya maana zaidi ya kutoa maneno matamu na viapo vya kusogezea wakati. Wapo wanaosema Kikwete ni mwororo mno kiasi cha kutoweza hata kuua inzi. Hawa kimsingi wanaitanabahisha jamii kuwa rais wao siyo jasiri.
Pili, ukiangalia CV ya Kikwete tangu akiwa hana madaraka na upenzi wake wa kwenda dansi na mambo mengine ya starehe, ungeshangaa kumuona anachukua hatua ambazo angezichukua mtu kama Marehemu Nyerere, Sokoine au hata Mrema.
Yeye ameonekana mtu wa utani utani kama alivyo kiongozi wa zamani wa waasi wa Msumbiji, Alphonso Dlakama. Kikwete hatumsemi vibaya. Ni mtu anayeweza kuimba msibani. Hebu jikumbushe alivyotoa majibu dhidi ya kumtaka amshughulikie Mkapa. Alitoa majibu rahisi na kwa utani utani alipokuwa ziarani Sweden kuomba misaada ambayo kimsingi kwa mtu makini ilikuwa ndiyo ilikuwa imeibiwa na mtangulizi wake.
Tatu, ukiangalia jinsi Kikwete amekuwa akitawala Tanzania, unagundua kuwa amekuwa na tabia na sifa ya kurudia yale yale anayokatazwa. Rejea kumteua rafiki yake mkubwa na mshirika wake, Edward Lowassa kuwa waziri mkuu dhidi ya upinzani na kelele za wananchi. Ameishia wapi?
Rejea pia kuendelea kurudia makosa aliyotenda mtangulizi wake. Ameweza kuwabakiza serikalini watu wachafu waliosaidiana na Mkapa kuifilisi nchi hadi juzi juzi maji yalipozidi unga alipofukuzwa Lowassa ambaye alikuwa akionekana kama ndiye mkuu wa nchi. Rejea utani wangu kuwa nchi haihitaji rais anayekuwa remote controlled kama Joice wowowo. Je Kikwete ameacha mchezo wake huu ambao ni hatari kwa taifa letu?
Bado hajaacha. Rejea kwa watu kama Andrew Chenge, Peter Msolla na Juma Kapuya kurejeshwa kwenye baraza la mawaziri ilhali wanakabiliwa na shutuma za ufisadi. Rejea kushindwa kuwawajibisha watu kama mkurugenzi wa TAKUKURU, Edward Hosea, mwanasheria mkuu wa serikali, Johson Mwanyika, mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji, Emmanuel Ole Naiko na katibu wa wizara ya hazina, Gray Mgonja na wengine ambao ni vinara wa wizi na ufisadi wa Richmond na EPA.
Nne, Kikwete alionywa kuhusiana na makundi katika chama chake maarufu kama mitandao. Hebu angalia wanavyoanza kuvurugana na kupakana matope. Rejea kashfa ya hivi karibuni ya matumizi wa spika wa Bunge, Samwel Sitta.
Rejea matamshi ya Kikwete kuwa CCM ndiyo chama kilichobainika kuleta amani na kupigania haki wakati kwa sasa ni chama cha vurugu na chenye kupinda haki tena mchana kweupe.
Tano, Kikwete amekuwa mugumu wa kujifunza na kujirekebisha. Siku mia moja za utawala wake, aliwaahidi watanzania kuwa serikali yake isingeiruhusu Tanesco kupandisha bei ya umeme. Baada ya muda kidogo tu ndani ya wiki tatu alijipiga mtama na kuridhia Tanesco kupandisha umeme kwa zaidi ya asilimia 40! Hii ni baada ya kugundulika kuwa Tanesco ni mkangafu-kwa mujibu wa maneno ya mkurugenzi wake mtendaji, Dr. Idriss Rashid. Hivyo kwa kujua kuwa Tanesco ilikuwa imefikishwa hapo na mtangulizi wake aliyelazimisha kuingizwa kwa menejimenti ya kijambazi kwa mtutu wa bunduki ya Net Group Solution, aliufanyata mkia?
Sita mtathmini Kikwete kuhusiana na muafaka wa mtafaruko wa Zanzibar ulioanzishwa na Mkapa na Salmin. Anazidi kutenda makosa yale yale! Je ni kwanini hajifunzi? Rejea alivyopoteza fursa ya Butiama katika hili.
Kitu kingine kinachoonekana kuwa Kikwete ni mugumu wa kujifunza ni kudanganywa kuwa CCM ifanyie mikutano yake Butiama bila kuwa na ajenda zinazofanana na Butiama. Alichofanya ilikuwa ni sawa na mlevi kwenda kunywea ulabu msikitini au changudoa kwenda kufanyia uchafu wake makaburini. Samahani msomaji tunatumia maneno na mifano mikali ili ujumbe ufike. Hivyo utahadharike kuwa maneno haya yanatumika kama mifano tu ili kufikisha ujumbe na siyo kumshambulia mhusika ambaye pamoja na mapungufu yake tunamheshimu maana ni rais wa nchi.
Kitu kingine kinachoonyesha kuwa Kikwete ni mugumu wa kujifunza na kubadilika ni kuendelea kujizungushia watu wachafu. Rejea maneno ya Kikwete alipokuwa akikubali waziri mkuu wa zamani kutimuliwa. Alisema anapokea taarifa hizi kwa masikitiko makubwa sana ilhali anaowatawala walikuwa wakipokea kwa furaha ya ajabu. Na hii inaonyesha usugu katika tabia hii. Maana kwa mtu aliyekuwapo wakati wa serikali ya mabavu ya Mkapa alipokuwa akikubali kuwajibika kwa mawaziri wake waliokuwa wamebainika kwenda kinyume alitumia maneno kama haya. na umma ulimgunia na kumchukia kwa kufanya hivyo. Kwa mtu mwepesi kusoma hali asingerudia kitu hiki.
Kitu kingine cha wazi kinachobainisha usugu wa kutojifunza na kubadilika ni kitendo cha Kikwete aliyeshuhudia madhara na hatari alivyopata Mkapa kutokana na mkewe mpenda pesa. Nake ajabu amemruhusu mkewe kufanya yale yale yenye kutia shaka aliyofanya mtangulizi wake. Hili japo haliandikwi, halipendezi kwa watanzania. Maana wameishaona jinsi Mkapa alivyoletewa tunda na mkewe kiasi cha kuishia kuwa kituko kwa nchi na wananchi wake. Wapo wanaosema mazingira aliyojenga Kikwete yanaonyesha atakapokuwa anaondoka madarakani atakuwa ameleta madhara makubwa kiuchumi kuliko hata Mkapa. Maana mambo yanajiendea ovyo ovyo tu.
Anayebishia hili atueleze ni nini sera na falsafa ya utawala ya serikali ya Kikwete. Aende mbele afanye tathmini ya utekelezaji wa serikali ya Kikwete ndani ya miaka mitatu ya kuwamo madarakani. Hakuna kitu zaidi ya maneno yasikuwa na vitendo.
Kitu kingine ambacho kimempiga chenga Kikwete na kumuangusha vibaya sana ni ile tabia yake ya kutoa ahadi hata kabla ya kutimiza na kutekekeleza zile za mwanzo za maisha bora kwa watanzania alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Alituahidi Kanani lakini hali inavyoonyesha tumerudishwa Misri tena kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya na staili mpya vya ajabu! Je kwa yote haya kweli Kikwete hajawa mugumu wa kujifunza na kubadilika?
1 comment:
mpayukaji napenda kukupongeza kwa makala zako zenye kutufunza watanzania wazalendo maana wako walio wazalendo na wasio. mimi sina mengi zaidi ya kusema kuwa raisi hatuna ila tuna garasa, na siyo mgumu tu wa kuelewa bali ni mbumbumbu. tuamke tuikomboe nchi yetu.
Post a Comment