The Chant of Savant

Monday 21 April 2008

Ya Chenge na Kikwete, tulisema utawala wa panya

NIMELAZIMIKA kurejea makala niliyowahi kuandika huko nyuma iliyokuwa na kichwa cha habari; ‘Bunge lisiwe kapu la makapi na cabinet haina mpya.’

Hii ni baada ya Rais Jakaya Kikwete ‘kulivunja na kulisuka’ upya baraza la mawaziri tata na kulirudisha kwa mlango wa nyuma. Ni pale alipoachia ngazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Hakuna ubishi, Andrew Chenge, ni mmoja wa vigogo katika Serikali ya Kikwete waliozusha utata baada ya kurejeshwa katika baraza la mawaziri badala ya kuchunguzwa.

Pia hakuna ubishi kuwa Chenge amekuwa kitendawili kwa wengi kiasi cha kumtaka Rais Kikwete amtimue. Wapo wanaomshangaa rais ni kwanini anamng’ang’ania wakati wenye nchi wanamtuhumu kuiingiza kwenye matatizo kwa kutoa ushauri mbaya kuhusu mikataba ya uwekezaji chini ya serikali ya Mkapa.

Chenge, mwanasheria mkuu wa zamani katika serikali kitendawili ya Mkapa na sasa waziri mwandamizi mara mbili kwenye serikali ya Kikwete, amevuta hisia za watu wengi kuhusu ufisadi na usaliti kwa taifa.

Nakumbuka, Chenge alipoulizwa sababu ya kurejeshwa katika baraza la mawaziri alijibu kwa nyodo; muulize Kikwete. Sasa tunamuuliza Kikwete kama alivyotutaka Chenge: Kikwete, ni kwanini ulimrejesha Chenge?

Na kwa kashfa iliyomuandama utazidi kumlinda? Je, umma utakuelewaje? Je, huku siyo kutumia vibaya ofisi ya umma na mamlaka ya urais? Je, utamlinda hadi lini? Una masilahi gani na uchafu wa Chenge na hata Mkapa?

Nadhani Rais anapaswa kurejea kwenye uzembe wa Mkapa ambao unamgharimu kwa kuwalinda watu waliokuwa wakitiliwa shaka katika uongozi wake.

Rais ameambiwa bila woga na wanaompenda kuwa amejaza mapanya nyumbani kwake. Lakini kwa sababu anazojua mwenyewe, amekuwa akitudharau kwa njia ya kunyamaza.

Vyombo vya habari kwa muda mrefu vimekuwa vikimshauri hata kumshinikiza Rais Kikwete kuwatimua na kujitenga na watu wote wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi akiwamo Chenge.

Lakini kwa sababu anazozijua mwenyewe, amekuwa mgumu kufanya hivyo wala kutoa maelezo. Hiki nacho kimegeuka kuwa kitendawili.

Lakini hakuna kitendawili kisicho na mteguaji. Wazungu wana msemo wao usemao kuwa, ‘even the busters can be busted.’

Ndivyo ilivyotokea hivi karibuni kwa Chenge ambaye amekuwa akijichukulia kama mtu asiyeweza kugundulika ujanja wake wala kuguswa kwa vile ana kinga kutoka kwa rais.

Nani alijua kuwa ungefika wakati wa Chenge kuwekwa hadharani ili wanaojitahidi kumsitiri nao waone kuwa umma sasa unajua ambacho hawakutaka ukijue?

Tuwe wakweli, madhambi yanayofanyika na kupewa kinga ya rais yamezidi kipimo. Kiwango cha uvumilivu hata ukondoo wa umma inabidi kikaripiwe.

Kwanini rais hataki kusikia kilio cha Watanzania, anaendelea kuwalinda waharifu huku nchi ikizidi kuteketea? Je, kimetimu alichosema Mwalimu Nyerere?

Mwalimu alisema hawezi kuacha nchi yake kwenda kwa ‘mbwa’, alipoambiwa upinzani ungeiondosha CCM asijue hata huko alikokuwa akiikabidhi chini ya utawala wa mwanafunzi wake, Benjamin Mkapa, ilikuwa sawa na kule alikokuwa akikataa! Ama kweli usilolijua litakusumbua!

Iwapo watu kama Chenge hawatashughulikiwa ipasavyo kama ilivyokaririwa hivi karibuni kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwa wanaogopa kulipua nchi, basi wananchi wanaodhulumiwa na kulalamika kwa rais asiwasikilize watailipua nchi.

Rais na chama chake wamekuwa wakiwekeza kukaa madarakani kwa vile upinzani nchini umedhoofishwa.

Lakini hali ilivyo, kama rais hatachukua hatua za makusudi kuiondoa nchi kwenye kujuana, kulindana, ufisadi na kutawaliwa na ombwe, ufisadi utamtoa madarakani.

Lazima aambiwe, nchi inanuka na inateketea mikononi mwake.

Rais amegeuka mzigo kiasi cha kututia kwenye majuto huku tukibakia kama yatima tusio na pa kukimbilia wala wa kumkimbilia.

Akitaka kujua hali ikoje, asome makala mbali mbali kwenye magazeti huru atauona ukweli ulivyo.

Rais sasa umaarufu wake unashuka kwa sababu ya ukarimu wake kwa watu wachache wanaojifanya marafiki zake wakati vitendo vyao vichafu vinaonyesha walivyo maadui zake wakubwa. Wanamchekea na kujifanya wanamheshimu ilhali wanamdharau na kumtumia.

Hili nimelijadili sana kwenye kitabu changu cha ‘Nyuma ya Pazia’ ambacho inshallah akipatikana mchapishaji wa kufaa kitakuwa mitaani siku moja.

Heri kuilipua nchi katika kutenda haki kuliko kutofanya hivyo kwa kuwalinda waharifu wachache. Kuna utata kwenye kitendawili cha jinsi mamlaka zinavyoshughulikia ufisadi. Kuna swali kubwa linaloanza kutusumbua vichwa:

Je, nchi hii ni yetu, rais au mafisadi? Je, rais alichaguliwa na mafisadi? Hata kama wahusika walimpa ‘tafu’ kwa kuchangia kampeni zake, bado nchi hii ni ya Watanzania. Na rais yupo kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania na si kuwatumia kama ilivyo sasa.

Muulize rais, sakata la Richmond na EPA yameishia wapi? Serikali imefanya nini zaidi ya kujifanya haihusiki huku ikitoa maneno makali yasiyo na ukweli wala maana?

Zaidi ya kuachia ngazi kwa Edward Lowassa na wenzake, nini kimefanyika kuonyesha kuwa serikali iko makini? Ajabu wahusika waliokiri wenyewe kwa kuachia ngazi bado wako bungeni!

Niliwahi kuandika kutahadharisha kuwa Bunge letu lisigeuzwe pakacha la kutupia makapi ya kisiasa na mafisadi. Nani anajali na kuchukua hatua.

Kinachokera zaidi, rais aliwahi kuwataka wananchi wampelekee ushahidi wa ufisadi aufanyie kazi. Sasa kama hili la Chenge anataka ushahidi gani?

Kwanza ni aibu kwa vyombo vyetu vya usalama na TAKUKURU ambayo badala ya kupambana na kuzuia rushwa imekuwa mstari wa mbele kuwalinda wala rushwa na mafisadi. Ingekuwa amri yangu, ningeivunja hata leo bila kutoa maelezo.

Yaani tumekuwa wa hovyo hadi ulinzi wa pesa na mali zetu ufanywe na wafadhili? Tuliishazoea. Kuna kipindi waziri fulani aliwahi kujisifia kuwa alikuwa amepata wafadhili wa kuchimba vyoo! Inawezekana huyu aliingia madarakani kwa bahati mbaya.

Kama hali itaendelea hivi, hakuna haja ya kumung’unya maneno. Nchi yetu imeporwa na kikundi cha watu wachache. Tumegeuzwa watwana na walamba makombo kwenye nchi yetu wenyewe!

Tujiulize, Je, sisi ni wa hovyo kiasi hicho sawa na wao kuwa mashahidi wa maangamizi yetu tena kwa kutumia mamlaka zetu?

Kikwete ameambiwa kuwa nyumba yake imejaa mapanya aliyoacha Mkapa. Amekuwa mgumu kuelewa na kuchukua hatua! Je, anangoja yaanze kumguguna yeye kama ilivyo kwenye sakata la kuzimwa Rostam Azizi ndipo atie akilini?

Huwa sina kawaida ya kuandika makala ndefu kwa vile zinachosha. Lakini hili la ukimya wa rais limenikera kupita kiasi.

Sasa pazia limefunguka. Yaliyopo nyuma yake kuhusiana na Chenge yameanza kuonekana na hadhira. Je, ya wale tuliouliza yataletwa lini mbele ya hadhira?

Turudie swali letu. Je, ni siri gani ya kuwarejesha mawaziri kama Juma Kapuya, Peter Msolla, Lawrence Masha, Juma Ngasongwa na wengine wanoonyoshewa kidole na umma?

Na kama waziri wa jana kama Chenge ana mabilioni, hivi hawa wazee kama Pesambili, Kapuya, Kigoda, Ngasongwa, Kingunge, na wengine wana matrilioni kiasi gani?

Je, kina Mkapa, mkewe na Sumaye wanayo matrilioni kiasi gani? Kweli adui wa Watanzania si mwingine isipokuwa watawala.

Hakika nihitimishe. Ya Chenge, Kikwete na vita dhidi ya ufisadi ni kero kwa umma. Je, Kikwete ataendelea na ujasiri ule ule unaohitaji roho ngumu huku mambo yakiharibika naye akiwa shahidi?

Je, wapo kina Chenge wangapi nyuma ya pazia? Je, hii pesa pauni 507,500 ni hiyo tu au kuna akaunti nyingine nyingi tu?

Mungu ibariki Tanzania.

Source: Tanzania Daima Aprili 20, 2008

No comments: