WANA Kijiwe wapendwa na wapondwa, wiki mbili zilizopita niliwaaga nikielekea Butiama alikozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Mchonga (Mungu amrehemu).
Pamoja na kuwapa ratiba ya shughuli, sikuwapa namna ya kuzifanya. Nawajulisha kwa ufupi niliyofanya huko. Namshukuru huyo Bwana sijui Bi aliyepo mbinguni kwa kunitangulia kwenda, kurudi na kunionyesha niliyoyaona ambayo sasa nasimulia. Kwanza vyangu walikuwa wa kumwaga kuanzia wa kisiasa na kisasa. Ngoja niongee taratibu Mama Kidume asije kuzinyaka akanisotesha na baridi. Nilipata wangapi? Usiulize.Kitu kingine ni kwamba tulimuenzi Mwalimu vilivyo. Niliongoza wachovu kwenda kwenye kaburi na kuweka bonge ya shada la maua baada ya watukufu kumaliza. Wachovu walikuwa wengi. Mbwa Mwitu alikuwapo. Kama mimi, bila aibu naye aliandamana nami kuweka shada asijue umma unajua alivyo kibaka na Mwalimu hakupenda vibaka! Baada ya hapo tulinangwa picha kibao tukiwa na Mama Maria Nyerere aliyetukaribisha kwa sana.
Baada ya kupiga picha na kumfunga kamba Mama Maria na walioshuhudia kuwa nilikuwa niko pale kumuenzi marehemu mumewe, niliwaita wachovu wenzangu kufanya kikao chetu sambamba na cha CCM. Mpemba bila aibu eti alitaka tutoe msimamo kuhusiana na muafaka wa mashaka. Hata kabla hajamaliza nilimwambia aachane na mambo ya kizamani. Nani aliona kondoo na mbuzi wanachanganywa? Nani anaweza kunieleza kama mashangingi ya vigingi na vigogo ni madume au majike? Utadhani tulikuwa tumeambiana. Na wenzetu waliamua kula jiwe na kukataa kujiingiza kwenye miafaka baada ya Karumekenge na genge lake kutia ngumu. Aliwataka waende kwa wanachi! Ajabu! "Kama alikuwa anaona hiyo ndiyo njia kwanini hakuipendekeza mwanzo akangoja muda, matumaini na pesa zetu viteketee?" alihoji Mpemba nami nikamzima. Hayo ni ya CCM na CUF. Hayanihusu. Watajijeijei. Halo halo!
Kikao chetu kikiwa kinaendelea huku mie nikicheka cheka, mara zilikuja taarifa kuwa wenzetu walikuwa wakikabana makoo kutafuta zengwe la kuondolea aibu. Maana tulijuzwa: mtoto wa mwanzilishi wa mapinduzi ya mawe na mapanga aliamua kuwatolea nje! Tulijuzwa kuondoa aibu, wenzetu waliiba mpango wetu wa kurudisha hoja kwa wanakijiwe! Hivyo ndivyo tulivyonusurika kuvuana nguo ingawa zilivuka tukabaki bila hata Godfather, yaani …! Ashakum. Tustahimiliane ndiyo hali yenyewe. Azimio la kukataa kutoa tamko la jibu la muafaka lilimkera Mpemba akasema akizidaka lazima azamie majuu kutushitakia, asijue hao watasha ni washirika wetu! Tutawapa kahawa na kashata watanywea.
Mchunguliaji ambaye anaonekana kuanza kuasi Kijiwe alikuja na hoja yake kuwa tuwalaani kina Mbwa mwitu vibaka kwa kuiba pesa ya Kijiwe! Hapa nusu tuchenjiane wenyewe kwa wenyewe! Mie kama mkiti nilitia ngumu. Ningeruhusuje upuuzi kama huu wakati nami nilishiriki kwenye kuponyoa njuluku za Kijiwe? Hivyo, wale viherehere waliotaka tuumbuane na kufukuzana waliambulia wa chuya. Hawajui siasa zetu za mizengwe zengwe. Hawajui. Katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu. Hawajui sisi tunapanda maneno na kuchuma mapesa! Washindwe na kulegea na kuumbuka kama Daktari Rwakatarehe alivyoshindwa kuuingiza umma mkenge kwa miujiza na maombi uchwara. Hawajui siasa ni kama ndoa. Mkiwa nje mnachekeana lakini ndani moto wa kuotea mbali! Wapuuzi hawa. Hawajui mchezo huu ni sawa na karata tatu! Ni mhuni gani wa karata tatu anaweza kumwadhibu mwenzake wakati lao ni moja? Ni muuzaji gani bangi anaweza kumfungulia mwenzake mashitaka kwenye mahakama ya sheria? Thubutu! Hata kama tumeishiwa hatujafikia huko. Hawa ni wapuuzi kweli. Hawajui kuwa kambale wote wana sharubu? Inaonekana wanaanza kuehuka! Nani alitegemea kutafuta uhai katika ufu? Eti wapo waliopendekeza niwafukuze kina Mbwa Mwitu! Ebo! Hawajui ndio walioniwezesha kupata uchache kuwahonga wanakijiwe nikapeta?
Kwanza acha niwapayukie hawa wapuuzi. Stupid you. Stop your nonsense of ufisadi kijiweni. Nani ambaye si fisadi? Mngekuwa si mafisadi mngenivumilia niendelee kuwaibia kashata na kahawa? Mngeshuhudia mimi na kina Kanji tunavyokatua msitutolee uvivu? Acheni uvivu wa kufikiri kama mjasiriamali fulani na mkewe waliouza dhamana zao wakajiuza na wao wenyewe!
Basi Bwana. Baada ya kumaliza zoezi la kuwekana sawa, nilipata bahati ya kwenda kuongea na Mwalimu. Alifurahia kwa kwenda kwetu kumtembelea na kumuenzi kwa namna ya pekee! Pia alifurahi sana kusikia wanakijiwe wanavyo furahia mafanikio baada yake. Alinipa hata salamu za mjasiriamali ambaye aliogopa kufika Butiama.
Kuhusu salamu zangu za kitaifa ingawa haukuwa ni wajibu wangu, sikuwa mjumbe wa mikutano ya CCM, alieleza kufurahishwa na uwajibikaji hasa kukuza uchumi na kuboresha hali za wanakijiwe. Alifurahi sana nilipomwambia kuwa jamaa sasa ni bilionea kutokana na kujiwekezea makampuni fulani fulani. Alisema huu ndio uzalendo wa kupigiwa mfano. Pia alifurahia kukataa suala zima la muafaka. Maana lingeligawa taifa.
Pia alifurahishwa na wapiga kura kuzingatia ushauri wake wakati wa uchaguzi wa 2005 kwa kuchagua watu makini na wazalendo, pia chama chake cha Mapinduzi ambacho kinavutia hata wenye nazo kiasi cha kukipiga tafu.
Baadaye lilifuata zoezi la kutambulisha miradi ya kitaifa kwa Mwalimu. Alifurahi sana kusikia kuwa kumbe kampuni za ANBEN, EPA, Richmond, Fosnik, Deep Green Finance, Kagoda, Net Solution, Consortium of Colluders and Managements (CCM) yalililetea taifa mafanikio makubwa kiasi cha nchi kujulikana kimataifa. Mwalimu pia aliwaonya wanaoleta umbea na fitina kuwa BoT kulikuwa na ufisadi. Alionya. Wanaweza kuigawa nchi.Alisifia sana kampuni zilizotajwa hapo juu na kusema zizidi kupewa ushirikiano ili kuikomboa kaya. Alipendekeza wanaozusha na kuziona kama za mafisadi wanyongwe na si kuonewa huruma. Pia Mwalimu alishauri rais ambaye ni chaguo la Mungu, aendelee kuchapa kazi na watakaojitia kumpinga wafungwe maisha huku wakikatwa ndimi zao. Mwalimu alisikitishwa sana na wasioona haya maendeleo. Alishauri watu kula mlo mmoja kwa siku kwa ajili ya afya zao. Alionya wanaokula sana. Ni hatari kwa afya zao. Pia alishauri tutafute utajiri wa ahera kuliko kumalizana kwa utajiri wa duniani. Ila Mwalimu alitushangaza kwa kitu kimoja. Nilipomwambia kuna watu wanataka kumpa daraja la utakatifu alisema eti hautaki. Maana utakatifu hutolewa na Mungu na si binadamu, tena wachafu! Alihoji utakatifu ni wa nini kama alitimiza wajibu wake?
Nilipompa salamu kutoka Zimbabwe kwa rafiki yake Mugabe, alitikisa kichwa na kushangaa kwanini Mugabe hakuja Tanzania kuazima ‘mbinu’ za kushinda kwa kishindo!
Kuhusu vifo vya Mererani, alisema vijana waache tama, badala yake waiachie serikali yao tukufu na aminifu ilete Wazungu wachimbe madini, wao wapewe chao, tena kwa haki kama ilivyo. Kuhusu usalama wa nchi, Mwalimu alisema vitendo vilivyoanza vya kuwaandama watu kuwa ni mafisadi hata kuwachomea nyumba viachwe mara moja. Kwani wanaofanya ufisadi ni wale wanaowafichua mafisadi. Watuhumiwa inapaswa ‘walindwe.’ Kwani ni watu wakubwa na ‘muhimu’ kwa taifa. Na isitoshe matumbo yao ni bora kwa kuliletea ‘sifa’ taifa.
Alisema kama watu wana ushahidi au wanauchukia ufisadi wasichomeane nyumba wala kulalamika ‘waandamane kuwapongeza.’ Tukiwa tunaendelea kuchonga na Mwalimu, mara mashangingi ya vigingi na vigogo yalitutimulia moshi na Mwalimu akayeyuka ghafla! Wewe acheni hizo, Mwalimu hawezi kutoa upuuzi kama huu. Mtajijeijei.
Source: Tanzania Daima Aprili 9, 2008
No comments:
Post a Comment