The Chant of Savant

Friday 17 April 2009

Umefika wakati wa kuwawajibisha Hoseah na Mwanyika

Watu wengi hawakuamini kuwa watu kama Edward Lowassa, Andrew Chenge na Nazir Karamagi wangejuzulu. Walishasema wazi: hawakuwa wana mawazo ya kufanya hivyo. Lakini wananchi na wabunge wao walipochachamaa, imebakia historia na somo kwa wale wanaong’ang’ania madaraka wakati wameishayachafua vibaya.

Leo tutajadili watu wawili wanaopaswa kufikiria au kujiandaa kufunga virago na kutokomea walipo watajwa hapo juu.


Hawa ni Mkurugenzi wa Takukuru Edward Hosea na Mwanasheria mkuu wa serikali Johnson Mwanyika.

Hosea alijikuta akikumbwa na tafrani katika semina ya Miundombinu ya Uadilifu iliyoandaliwa na Takukuru na Chama cha Wabunge wa Afrika (APNAC) na kufanyika kwenye hoteli ya Whitesands jijini Dar es salaam.

Katika semina hiyo,mambo yalianza kumwendea kombo Hosea wabunge walipotumia semina ya uadilifu kuhoji uadilifu wake.

Mbunge wa Busega Raphael Chegeni alikaririwa akiuliza swali ambalo Hoseah hakupenda. Aliuliza.“Inakuwaje wakati wa mjadala wa Richmond , wewe mkururugenzi wa Takukuru ulikanusha kuwapo rushwa na uchunguzi wa kamati ya bunge ulibaini kuwepo rushwa ndani ya kampuni hiyo? Je ni nani mwenye dhamana ya kukuadhibu wewe na taasisi yako kuhusu rushwa.”

Hebu angalia kutapa tapa na kutishana kwa Hosea. Yeye alijibu ifuatavyo:Hapa siyo jukwaani hivyo tusilete siasa. Nipo hapa kwa ajili ya kufundisha na kama ni suala la Richmond waziri mkuu alishaliongelea na ndiyo mwenye dhamana ya kujibu hilo . Mimi sina jibu kwa hilo na kama mtu hapendi kuvuliwa nguo kwanini umvue mwenzako,"

Je ni kosa kwa mwakilishi wa umma kuulizia maslahi ya waliomtuma?

Ulazima wa watu kama hawa kuondoka mara moja unajitokeza pale wanapolewa madaraka hadi wanaanza kuwatisha wawakilishi wa umma. Hivi karibuni Hosea aliwatishia wabunge kuwa anaweza kuwachafua kwa sababu tu kuulizwa aeleze uadilifu wake!

Bila aibu wala woga aliwafokea wawakilishi wa umma wakati yeye ni mteule tu wa mwajiriwa wa umma-rais. Anapata wapi hii jeuri wakati ameishaharibu nafasi yake muda mrefu? Je wabunge watakubali jeuri na aibu hii licha ya kuwa tayari Hosea aliishaliingizia taifa hasara kwa kutaka kutetea Richmond ?

Naye Dk. Zainab Gama hakujivunga, alipigilia msumari mwingine. “Sisi ni muhimu sana na tunaamini kwamba kiongozi, mwanasiasa au mtendaji yoyote akiingia madarakani kwa rushwa, hataweza kusimamia mapambano dhidi ya rushwa kwa uhakika. Sisi wabunge wanachama wa APNAC tuwe ndio mfano."

Majibu ya Hoseah si ya mtu mwadilifu na mwenye kujua mipaka ya madaraka yake. Amejivua nguo kwa kutoa vitisho kwa watu wazima tena wanaowakilisha umma. Je anangoja nini kwa jeuri na upogo huu?

Umma umekuwa ukishinikiza Hoseah na Mwanyika waachie ngazi halafu wafikishwe mahakamani. Lakini rais Jakaya Kikwete amekuwa anawakingia kifua kwa njia ya kujifanya hasikii. Je ana faida gani na uchafu wao au naye yumo nyuma ya pazia kwenye Richmond hasa ikizingatiwa kuwa swahiba yake na mshirika wake mkuu, Edward Lowassa aliwahi kusema kuwa rais alikuwa akipewa taarifa zote kuhusiana na mchakato mzima? Je Kikwete hapa atakwepa kuwa mhusika wa Richmond ama kwa kutochukua uamuzi wa kuwawajibisha akina Hoseah au kwa kushiriki moja kwa moja?

Kwa Kikwete kuendelea kuwakingia kifua watendaji ambao wameishathibitisha kutokuwa wadilifu si ushahidi tosha kuwa hawa ni wabia wa serikali yake ingawa amekuwa akikanusha hili?

Umefika wakati wa kujua upande aliopo Kikwete. Lazima achague moja. Awe nasi au na mafisadi. Lakini hawezi kuwa kati yetu na mafisadi.

"Mjadala huu aachiwe Waziri Mkuu Mizengo Pinda na aliyeuliza swali hilo hanitendei haki kwani hakuna hoja nyingine ya maendeleo kwa jamii ambalo inaweza kujadiliwa...” Aliongeza Hosea.

Hoseah anataka suala lake liachiwe waziri mkuu! Waziri mkuu kama nani iwapo wawakilishi wa wananchi wanataka maelezo? Kama anadhani kuwa: waziri mkuu aliposema wamepelekewa barua wajieleze ndiyo suluhu amekosea. Waziri mkuu si mahakama wala bunge. Hivyo, kitendo cha kuwatumia barua za kishikaji na kutaka yaishe lazima kisikubalike hata kidogo. Hoseah na mwenzake washughulikiwe kwa uwazi na si kwa kujuana au ki-CCM au kimizengwe. Waziri mkuu hana mamlaka wala msaada kwa mtu anayetuhumiwa ufisadi. Hata angeagizwa na bosi wake, hakuna bosi wa umma bali umma wenyewe.

Kuna haja ya wadau kuwashinikiza Hoseah na Mwanyika waachie ngazi. Kama rais ataendelea kuwabeba kwa maslahi na sababu anazojua naye ashinikizwe aachie ngazi. Na bahati nzuri uchaguzi ndiyo huo unapiga hodi. Nchi hii ni yetu si ya rais wala akina Hosea. Na ofisi wanazotumia ni zetu si zao wala nani wao. Hivyo waelewe wazi kuwa mwisho wao umekaribia.

Kama wenye vifua na ushawishi kuliko wao kama Lowassa wamekwenda na maji wao ni nani katika nchi hii hadi wawatishe wabunge? Huwezi kuwatisha wabunge ukawa salama kwenye ofisi ya umma uliowatuma.

Hakika ya Hoseah na Mwanyika ni ni hadithi ya kumbi kumbi. Akikaribia kufa huota mbawa akaruka na mwewe wakamuona na kummalizia kazi. Nasisitiza. Huwezi kuwatukana wabunge ukapona hata kidogo.

Funga kazi ya Hoseah hii hapa. “Wapo wabunge wanaohudhuria semina zaidi ya tatu kwa siku moja na kusaini posho, lakini hata baada ya kuwezeshwa kwa posho hizo, hakuna uwajibikaji. Kwa kweli kuna mambo mengi yanayotokea, lakini tunayafumbia macho.”

Sentensi ya mwisho ya Hoseah inaonyesha asivyo makini wala mwadilifu. Ni mambo gani haya wanafumbia macho huku wakilihadaa taifa kuwa Takukuru ipo kupambana na rushwa wakati ipo kufumbia mambo macho kama ilivyotaka kumsafisha Lowassa bila mafanikio? Je wanayafumbia macho kwa sheria ipi na kwa faida ya nani kama si ushahidi tosha wa ufisadi?

Hivyo, kuwasaidia wahusika waliobainika kushiriki uchafu wa Richmond , waachie ngazi kabla ya umma haujawatoa ofisini kwa nguvu.

Hoseah na Mwanyika, mnangoja nini wakati mmeishaharibu kibarua? Umefika wakati wa kumtaka Kikwete awafikishe mahakamani watuhumiwa wote wa Richmond bila kuangalia urafiki na kujuana.
Chanzo: Tanzania Daima April 15, 2009.

No comments: