The Chant of Savant

Tuesday 20 October 2009

Mpayukaji aadhimisha miaka kumi ya kifo cha Nyerere

Katika kuadhimisha miaka kumi tangu kuondoka kwa paka na panya kujitwalia uhuru- yaani miaka kumi ya kifo cha mzee mchonga Julius K. N Burito, mzee mzima Nilitinga Butiama. Ni baada ya kuona kila mmoja akijitahidi kuonyesha sanaa zake.

Ingawa matendo yangu hayafanani ya marehemu Nyerere, bila aibu, nilijipeleka Mwisenge kuuhadaa umma kuwa nilimpenda mwalimu wakati nilimchukia hasa kuingilia ulaji na dili zetu na ndugu yangu Eddie Ewassa Mchunguliaji wa Mkwapuaji.

Kama walevi wengine, nilitinga Butiama kwa pipa la Precision Eya. Nililipa bei gani? Hayakuhusu. Najua vizabazabina vitaanza kuhoji nilipata wapi hizi chapaa au ni yale yale ya EPA na Richmonduli? Kwa taarifa yenu nilitumia pesa ya kijiwe full stop and period.

Baada ya kufika nikiwa nimejinyenyekeza kama kondoo ilhali ni chui kwenye ngozi ya kondoo, nilikutana moja kwa moja na mjane wake, Mama Maria pamoja na vitegemezi vyake. Ingawa roho ilikuwa ikinisuta, sikuwa na jinsi bali kwenda ili kupata tafu kwenye uchaguzi wa kijiwe ujao. Mambo ya politics na politricks za kijiwe bila kufanya usanii unaweza ukaumbuka mchana mzee mzima.

Kuzidi kuwabamiza mkenge wadanganyika walevi, niliamuru wapiga picha wangu wakiongozwa na Mchuuzi, Mbwa Mwitu na Mgosi Machungi wapige picha kama kufuru ili zitoke kwenye magazeti na walevi wazione wajue siku hizi nimeokoka toka kwenye ufisadi na kurejea kwenye Ujamaa na kujitegemea -wakati ukweli ni kwamba siasa zangu kijiweni ni za uhujumaa na kujimegea. Upo hapo mwanangu? Wajinga ndio waliwao. Tusameheane. Na isitoshe sikuitwa bingwa wa sanaa kimakosa. Ni msanii kweli kweli kuliko hata yule mwimbaji wa ngonjera mkuu.

Siku hiyo sikuvaa suti. Nilivaa vazi la Chu En Lai alilopenda Mwalimu ili nionekane nafanana naye wakati kutulinganisha ni sawa na kumlinganisha kupe na tembo! Na kama si kuogopa wambea kunipakazia ningetinga na mgolole kama aliouvaa mwalimu wakati wa kupokea uhuru. Lakini ningefanya hivyo ningeoneka nasikiliza ushauri wa Mizengwe iliyopinda wa kuacha kupiga pamba kali. Ingawa moyoni nilikuwa na furaha kwa kufaidi uhuru bila mwalimu kuwepo kunisuta kwa ufisadi wangu kwa kijiwe, nilijifanya nina majonzi kumpoteza shujaa huyu nguli.

Kuwapumbaza walevi, niliapa kwa miungu yote kuwa urathi wa mwalimu hautatoweka kabisa ingawa mema yake yote aliyopigania tumeishayamomonyoa.

Kunogesha mambo, niliandamana na mama Kidume (ambaye watani wake wanamwita Mama Machinga msaka ngawira na mchumia tumbo na kadhalika na kadhalika) ili kumpa tafu Mama Maria. Kwa vile mimi si mwepesi wa kulia, ilibidi niende naye ili ikibidi kumwaga chozi anisaidie. Ingawa mama Kidume na Mama Maria ni sawa na kifo na usingizi kutokana na anavyotumia cheo changu kukiibia kijiwe, hivyo hivyo, kisanii kama mumewe, tulijitoa kimaso maso.

Laiti walevi wangeangamua kuwa Mama Maria alikuwa amezungukwa na walevi na wazinzi kuadhimisha kifo cha Mtakatifu mtarajiwa, angetutimua kama mbwa koko hata kusiri. Hata ukijikumbusha vitu vya mke wangu, utagundua hili. Wakati Mama Maria alivalia kama wanakijiwe wengine, bi Mkubwa alijitona midhahabu chekwa kama hana akili nzuri. Mama Maria hakuwa na kampuni ya kuchotea pesa ya taifa sawa na bi Mkubwa wangu ambaye ana kampuni yake iitwayo MAWAWA yaani Maulaji ya Wake za Wakubwa-aitumiayo kukikomba kijiwe.

Walevi kweli ni walevi. Una habari eti walitaka niwe mgeni rasmi kwenye kumbukizi hili lakini waliogopa wakamwalika mkuu badala yangu kwa kujua angejinyonga kama angejua adui yake mie ndiye mgeni wa heshima hata kama hatuna heshima.

Nilipiga mbio na kwenda kwenye kaburi la Mwalimu na kuomba sala ifuatayo:

“Ee Mwalimu Nyerere, kwanza naomba tusameheane kwa yote ninayokutenda. Naomba unisamehe sana kwa kuwakumbatia wezi na vinyamkera kama akina Mbwa Mwitu, Mgosi Machungi, Ewassa aitwaye Mchunguliaji, Enderea Chenga wa Makengeza na vibaka wengine. Najua unajua. Tumebinafsisha kahawa, kashata na tangawizi hata vigoda tunavyokalia bila kusahau hata kijiwe chenyewe. Nakiri ulikuwa mtu safi . Mimi ni mchafu ninukaye kama nguruwe. Kwa vile wafu hawasimulii hadithi, naomba unisamehe ninapofaidi huu uhuru. Paka akindoka Mwalimu, panya hujitawala. Najua inaudhi hasa kuona tunakutenda hivi. Tunahujumu kazi zako na kujitia kimbelembele kuwa tu wanafunzi na wafuasi wako.”

Nilikohoa kidodo na kuendelea. “Mwalimu siasa za dunia ya karne ya 21 zimebadilika. Zama zako siasa ilikuwa ni utumishi wa umma. Kwa sasa ni kuutumia umma kupata mshiko ukwasi na sifa kama zangu. Pia ni kuchuma mipesa na kuficha nje. Hatuna haja ya kutaja mali zetu. Maana walevi wakijua wanaweza kutunyotoa roho. Wewe hukuwa na haja ya kutangaza mali zako. Kwani zilijitangaza. Ulikuwa rais kapuku. Mimi siwezi kutaja maana utajiri wangu na marafiki zangu na mshirika wa bedroom zinatisha mwalimu.”

Nilikohoa kidogo na kuendelea huku mama Kidume akijifanya kumwaga chozi la mamba hadi Mama Maria akamuonea huruma na kumfariji asijue ni msanii na kibaka wa kawaida. Niliendelea. “Mwalimu hukuandaa vitegemezi vyako kuchukua madaraka au kukalia nafasi nono chamani na serikalini. Mimi nimeruhusu vitegemezi, ndugu zangu na bi mkubwa wangu kukitumia kijiwe kujineemesha. Hukutoa takrima ulipoingia madarakani. Mimi niliibia kijiwe kiasi cha almanusura nikifilisi. Mie ni mchafu mwalimu. Naomba unisamehe sana kwa uongo ninaowaambia watu wako na familia yako. Mie sina taifa lako moyoni kama wewe. Mie nina tumbo langu moyoni. Uliongoza kwa ushupavu. Mie ni ujanja ujanja. Kijiwe nakiendesha kama danguro mwalimu. Naomba unisamehe sana kwa ninavyoendesha kijiwe. Hata hivyo siyo tatizo sana kwa sababu mimi si rais.”

Nilivuta kitambaa toka mfukoni na kujifuta chozi la uongo hadi Mama Maria na umma kwa ujumla kunionea huruma wasijue wa kuhurumiwa ni wao!

Nilimalizia. “E nwalimu, sistahili kuja kwako. Lakini nasema neno moja tu ili roho yangu ipone. Mimi ni fisadi uliyemstukia mara nilianguka kutokana majonzi na uchovu wa safari.





Khalas tamam

No comments: