The Chant of Savant

Friday 19 October 2012

Kikwete toa tamko na msimamo wako





Ingawa wengi ambao tumekuwa tukikosoa staili ya utawala wa rais Jakaya Kikwete, tumeonekana wabaya. Ingawa lengo letu ni kumsaidia kufanya anachopaswa kufanya badala ya kugeuka kiguu na njia kila siku angani akizurura ughaibuni, tunaonekana wabaya. Hakuna ubishi kuwa nchi yetu sasa iko msambweni ikitishiwa kusambaratishwa na udini utokanao na ujinga, ukosefu wa ajira, usongo na husda kwa baadhi ya watu wetu tulioshindwa kuwaendeleza. Hapa ndipo unatakiwa uongozi wenye visheni na mipango madhubuti ili kupangua  janga hili la kujitakia. Kumekuwa na malalamiko kuwa serikali inatumia nguvu nyingi kupambana na upinzani badala ya kutimiza wajibu wake. Jeshi la polisi limekuwa jepesi kuwahi kusitisha mikutano ya upinzani. Bila kujua kuwa kuna upande mwingine ambao umekuwa ukiutumia udhaifu huu, sasa serikali inajikuta uso kwa uso na wahafidhina wenye hoja zao fichi. Je ni wakati wa utawala wa Kikwete kuwekwa kwenye mizani au kuumizwa na wale uliowadharau na kuwafumbia macho. Ingawa tunaona machafuko yanayoendelea kama matokeo ya udini, ukweli ni kwamba ni matokeo ya ufisadi, umaskini, ujinga, ufisi, uroho na kasumba.
Watu wetu wengi hawana ajira na hawajui kesho yao itakuwaje. Wamekata tamaa na wanaweza kutumiwa na yeyote awezaye hata kuwaahidi jibu achilia mbali kutoa hilo jibu. Hii ndiyo maana hot spots za vurugu ni kwenye makazi ya watu maskini kama vile Mbagala na siyo Oyester Bay wala Masaki. Walioko kule wana uhakika wa maisha wagombee au kuandamana kwa kitu gani?
Sasa Kikwete amerejea. Tumshinikize atoe mwelekeo wa taifa. Kwa mazoea yake ya kutojali unaweza kuambiwa kuwa kesho ana safari ya kikazi kwenda nje. Amekuwa akituchezea akili hivyo. Kila kukitokea matatizo Kikwete na genge lake wako nje wakitanua huku umma wetu ukiendelea kuteseka. Amekuwa akitumia jeshi la polisi kuzuia rabsha. Sasa ameishiwa hadi anaanza kutumia jeshi ambalo kikatiba kazi yake ni kupambana na maadui wa nje na si wa ndani.
Tumalizie kwa kumuasa Kikwete kuwa kama hatabadili staili yake ya kutawala ataiweka nchi pabaya. Ameacha mambo yajiendee ambapo kila tapeli anaweza kuanzisha dhehebu au kundi la dini kama walivyofanya Uamsho na Ponda Issa Ponda. Tunao wachumia tumbo wengi waliojificha nyuma ya majoho ya dini kutokana na kuujua udhaifu wa Kikwete. Rais Kikwete toa tamko na msimamo kuhusiana na mwelekeo wa taifa letu.
Mungu ibariki Tanzania.

1 comment:

Jaribu said...

Usiwe na matumaini yoyote kuhusu huyu jamaa. Nilishasema kuwa staili yake ya utawala ni kujifanya? au kuwa juha.