The Chant of Savant

Wednesday 17 October 2012

Ni mbwa gani mwenye ujasiri wa kumng’ata bwana wake?




BAADA ya Takokuru -- ile Tume ya Kupokea na Kulinda wala- Rushuwa inazidi kujirusha kimanga au tuseme kuonyesha kuwa ni wambea watupu, Kijiwe kimeamua kuunda kamati ya kwenda Uswisi.
Msiseme nawasingizia au kuwaonea gere. Nani mara hii walivyotaka kumsafisha Eddie Ewassa lilipobumburuka soo la Richomonduli?
Kama siyo Kijiwe kushauri jamaa wa kwenye mjengo chini ya Sam Sixx kupewa uwazahili kuja juu huenda jamaa na jamaa yake wangekuwa bado wanatuibia tena zaidi.
Hakuna mtu aliyeniacha hoi kama Dk Eddie Washea aliyemwambia mwanadiplomasia wa nchi ya kwa Obamiza kuwa mkuu anamkwamisha lakini akachomoa wambea walipotonya na kumwaga mambo hadharani.
Pia nasikia kuwa jamaa naye amejilimbikizia mimali itokanayo na rushwa hakuna mfano!
Baada ya kugundua hizi ngonjera na kutaka kujilisha pepo hata kuwatoa watuhumiwa mshiko, tumeamua kufuatilia mabilioni ya dola yaliyofichwa na vibaka wa kaya kama ilivyoelezwa hivi karibuni.
Seriously, tunakwenda kule kufanya kweli. Hatutakuwa tayari kuhongwa jezi, kutongozwa tujigawe na watu wetu wala nini bali kuhakikisha tunakuja na vitu viwili; yaani fweza na majina ya mibaka na majambazi walioficha pesa hiyo kule bila kujali kama ni waheshimiwa, wastaafu au wenye mamlaka.
Sisi sasa hivi tumeishakuwa machizani wasioogopa kitu wala mtu bali kugeuzwa majuha.
Hatuogopi ngurumbili tena bali tunaogopa wajukuu wetu siku moja baada ya kurejesha namba kukojolea makaburi yetu siku moja kama hatutafanya kweli.
Tunaogopa vitegemezi vya wanetu siku moja kuamru makaburi yetu yafukuliwe ili kugundua ugonjwa uliokuwa unatugeuza mazezet ili hili lisijirudie katika maisha yao na baada ya hapo.
Tunaogopa makaburi yetu kuchapwa bakora siku moja kama adhabu ambayo wangetupa kama wangeishi kipindi kimoja nasi.
Hilo ndilo linalotushughulisha kuliko yote.
Baada ya kusikia sanaa za Takokuru kuwa itashughulikia suala hili kwa kuwasiliana na Banki za Uswisi wakati tukijua ni upuuzi, tumeamua kufanya kweli kwa kuunda tume ya Kijiwe.
Tunajua kabisa kuwa Sanaa za Takokuru ni uhuni wa kawaida ukiachia mbali nao kuwa wala rushwa wakubwa. Saa nyingine utakuta walioficha pesa kule wengine ni madingi wa Takokuru hiyo hiyo. Kwa Kaya yetu kila kitu kinawezekana kutokana na madingi kutopenda kutangaza mali zao kuanzia mkuu.
Katika kuchukua uamuzi wa kuunda tume tulizingatia mambo mengi. Mfano, kama mlishindwa Richmonduli iliyokuwapo hapo uani mwenu mtaweza NSB?
Kama mlishindwa kuwakamata hawa jamaa kabla ya kufanya au wakati wa kufanya madili yaliyowawezesha kupata mwanya wa kutibia na kuficha, mtawaweza saa hizi ambapo pesa iko mbali hivyo? Ni mbwa gani atamng’ata aliyemfuga anusurike kupigwa mpini?
Tukubaline Takokuru. Hawa siyo saizi yenu bali saizi ya Kijiwe ambacho watendaji wake wote ni fyatu wasioogopa mdudu wala gendaeka.
Acheni ushamba na ulimbukeni wa kutufanya sisi majuha. Nijuacho ni kwamba kama watajifanya wanakwenda Uswisi kufuatilia pesa, watakachofanya licha ya kushangaashangaa ni kufanya shopping za kilimbukeni na kishamba huku wakitumia fursa hiyo kuiba pesa nyingi toka kwenye Hazina ya kaya.
Maana Kaya yetu huendeshwa kwa dhana mfu ya kufa kufaana.
Mkuu wetu wa kijiwe akienda kuzurura nje na mkewe na washikaji wake wanalipana mipesa kibao licha ya kutojali kuwa hata safari zenyewe ni ufisadi mtupu.
Hebu fikiria jitu linakwenda nje kupewa zawadi za leso kwa mfano. Hii ina tofauti gani na zama za akina Mangungo waliohongwa shanga na mvinyo wakauza watu wao na ardhi yao wakiwamo wao wenyewe?
Heri akina Mangungo hawakujua kusoma na kuandika na walifanya hivyo wakidhani walikuwa wakiwasaidia watu wao tofauti na hawa wanaosukumwa na roho mbaya na uroho, ujuha na upogo.
Takokuru mwamhadaa nani? Kama mlishindwa kuwanyaka walipofanya ufisadi hapa hadi wakakusanya mshiko na kupeleka Uswisi huko ndiko mtawaweza?
Semeni ukweli kuwa mnataka kudandia pipa angalau muwaangalie kunguru kwa chini siyo kila juu mnaogopa hata kuwaangalia ili wasiwanyee.
Mshindwe na mlegee kama siyo kupagawa. Yaani Kaya yetu imekuwa ya vibaka watupu! Au mnataka mkazamie maana wabongo kwa kuzamia sina hamu!
Kijiwe kimeishachoka na ujuha na ushangingi wa kukamata vidagaa huku mapapa wakitanua Tutaleta orodha ya majina yao bila kujali vyeo jinsia wala mitandao yao ya kijambazi na kichama.
Pia tutakuja na orodha ya majina yote ya makampuni jambazi ya kigeni yanayowawekeza fweza hawa majambazi.
Tunataka wanakaya wajue wezi wao na waanze kuwapa kichapo kama wataamua kuamka na kusikiliza mawazo ya ukombozi. Kumbe huku ndiko pesa ya miminerozi inaishia!
Tunaambiwa kukuza uwekezaji kumbe watu wanakuza uchukuaji!
Mkuu wa kijiwe yumo bila shaka. Hapa Ben Makapu Tunituni na Anna Tamaa, Ally Hoseni Ruksa hawakosi.
Rafiki zangu Endelea Chenga, Heze Maige, Ni ziro Karamagi, Dan son of Jona Bassie Pesa2 Dk Abdi Kikalio, Rizzie1 Kibosile na majambazi wengine wakubwa wamo.
Lolol! Nilitaka kumsahau Eddie Ewassa, Idd Lion, Ibra Bangusilo M7ha na Dk Idd Iliisha.
Kuna watu wanajulikana hiyo hongo yao wanajulikana walipoitoa.
Ruksa bila shaka alipewa na yule aliyemuuzia Loliondo, Ewassa ni Richmonduli, Chenge ni Bea, Ziro-karamagi ni Buzwagu.
Ngoja I don’t need to preempt. You can take this to bank. What I am saying is true and it the truth beyond truth so to speak. I call upon everybody to glean this truth and put it to work. OMG! Kumbe naongea kikameruni! Tusameheane ni kwa vile nategemea kwenda Uropa kuwakamata wezi wenu. Hivyo lazima nifanye mapraktizi ili nikifika kule watasha wajue nachonga maza inglish yenye kuwa polished and not policed like Mwangosi.
You know what? Wezi wenu ni wale wale mnaowaambia wajikamate. Nani anaweza au mnataka kufanya kama ndata? Unaramba mtu shaba anadedi halafu unaunda tume ya kujichunguza na mjinga mjinga mmoja Nchimvi anajisifu kuwa ametenda haki. Tell it the birds. Nikupe siri? Nakitoa taratibu.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 17, 2012.

No comments: