The Chant of Savant

Tuesday 23 October 2012

Serikali ijilaumu kwa kuufuga udini


HIVI karibuni taifa letu limekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari vya kimataifa. Hata hivyo, si kwa sababu nzuri bali uchomaji wa makanisa uliotokea baada ya watoto kufanya utoto kutokana na kufundishwa imani potofu na za kishirikina.
Chanzo cha yote ni ubishi baina ya watoto wawili mmoja mkristo na mwingine Muislam kuwa akojoleaye au kuharibu, kutemea mate Korani aweza kugeuka mjusi hata kufa.
Hakuna anayeunga mkono kitendo hiki hata kama ni cha kitoto. Kadhalika, hakuna mtu mwenye akili na nia nzuri anayeweza kuunga mkono matokeo ya kadhia hii.
Katika utoto huu mmoja wa watoto aliamua kufanya majaribio kujua kama alichoambiwa ni ukweli au la. Baada ya kufanya hivyo bila kufa wala kugeuka mjusi, tunaambiwa mwenzie alichukia na kwenda kuripoti kwa wazazi.
Kimsingi, watoto wamefanya utoto kiasi cha kuwaingiza mtegoni watu wazima kushabikia na kufanya utoto zaidi. Wanaojiita waislam wenye ajenda zao za siri walipata fursa ya kuhubiri kiama huku wakishinikiza makanisa yachomwe!
Je, hii ni busara, elimu au dini aina gani isiyotumia hata chembe ya akili? Akikosa mkristo au mkwere mmoja basi unaadhibu wakristo au wakwere wote!
Ili kuona kama kweli kulikuwa na haja ya kujichukulia sheria mkononi ngoja tuhoji. Je, Korani ni nini? Korani ni kitabu sawa na vitabu vingine ukiondoa kuwa husemekana kuwa kimetoka kwa Allah. Ukiondoa hiki kitabu tunachoona, Korani si vile vitabu tunavyomilki bali ujumbe ambao mtume Mohammad (SAW) alikuwa akipokea na kuwakaririsha wafuasi wake.
Ni ajabu: Mohammad alipokufa, aliacha kila kitu kwenye uislam ambao alisema aliukamilisha isipokuwa kitabu kinachotugombanisha.
Je kwa msingi huu, hii Korani (kitabu) ambayo hata mtume hakuiacha inakuwaje inapewa umuhimu kuliko hata ubinadamu?
Binadamu ameumbwa na Mungu. Korani imetengenezwa na binadamu. Huu ni ushahidi ima wa ushirikina au kutojua mambo.
Nasema hivyo kutokana na ukweli kuwa anapochomwa moto kibaka kwa mfano ambaye ni kazi ya mikono ya Mungu, watu hawaandamani wala kuchoma makanisa.
Ajabu kikichomwa kitabu kazi ya mikono ya binadamu watu wanakamiana na kutaka kuuana! Je hapa kweli tatizo ni kuchomwa kitabu au kuna jingine?
Si uzushi wala upendeleo kusema kuwa serikali yetu imefuga hisia za udini nchini mwetu. Maana kumekuwa na watu wanaoota ndoto za mchana kuwa kuna siku Tanzania itatawaliwa Kiislam au Kikristo.
Ila wanasahau kuwa uislam haujawahi kutawala popote ukiachia mbali baadhi ya watawala kuutumia kufikia malengo yao. Mfalme Constantine aliutumia Ukristo kutawala Rumi, Ezana (Kush) huku watawala wa Ottoman, Mughal na Safavid nao wakiutumia uislam kujiimarisha kwenye madaraka.
Je, chanzo cha manabii wa vita na machukizo kama vile Uamsho na wana mihadhara ni nini? Ni ulegelege wa serikali bila shaka.
Tunao wahubiri wengi wa kiislam wanaotumia Biblia kushawishi watu kuwa waislam pasina kutumia Korani kutokana na kutoijua wala kusoma dini.
Hili ndilo kundi kubwa lenye mashehe wa kuzuka kama huyu anayehubiri machafuko aitwaye Issa Ponda Issa ambaye shehe mkuu Shabaan Simba alisema si shehe wala msomi, bali mhuni wa kawaida anayetafuta riziki kwa kujificha nyuma ya joho la uislam.
Leo tuna makundi yenye kila alama za ugaidi kama Uamsho yakijidai kupigania haki za waislam hata watanzania. Ukiwauliza aliyewachagua na kuwatuma hupati jibu zaidi ya kuvunja sheria ya nchi.
Hawa na wale wa kikristo wamekuwa wakiwapigia watu kelele bila hata kujali kuwa wanahitaji utulivu. Leo, kwa mfano, ni hatari kulelea mtoto kwenye baadhi ya maeneo jijini Dar kutokana na kelele zinazotoka misikitini na kwenye makanisa hasa ya mikesha.
Kinachofanya serikali ilaumiwe ni ile hali ya kuruhusu kila mtu kujifanyia atakavyo bila kufuata serikali. Madhehebu ya dini yalipaswa kusajili kwa sharti kuwa yakienda kinyume na matarajio ya serikali yanafutiliwa mbali.
Leo tuna maaskofu wengi feki wanaotumia dini kuwaibia maskini na kuwadanganya wanamchi kila uchao.
Tuna mashehe wengi wanaoibuka na kutangaza vitu vya ajabu kama hawa wanaotaka kuangusha Bakwata au kutaka kueneza uislam wa kihafidhina ambao hata Mtume hakuuacha.
Hata hivyo, inapaswa watu wa namna hii kuambiwa kuwa tulipopigania uhuru tulipigania uhuru kama watanzania na si waislam wala wakristo. Mtu yeyeto aweza kuingia dini yoyote na kutoka lakini hawezi kufanya hivyo kwa uraia wake kirahisi hivyo.
Kwenye kujiunga na dini hakuna maombi wala masharti sawa na uraia. Mbona wakati tukiingizwa kwenye mfumo wa kikoloni au kupelekwa utumwani hizi dini zinazotaka mamlaka leo hazikutusaidia zaidi ya kuwa wakala wa mateso yetu?
Kuna haja ya kusoma historia kuepuka aibu ya kiakili kama hii. Hivyo, hawa al muthnaka wanaoota mchana kudhani Tanzania inaweza kutawaliwa kidini, washikishwe adabu mara moja.
Ni upuuzi na utaahira ukiachia mbali uchizi kwa watanzania maskini kujificha nyuma ya imani za kimapokezi na kimamboleo hadi kuchelea kumalizana. Ni ajabu leo watu wanahamanika hata kufikia kutaka kutoana roho kwa mambo mepesi wakati mambo mazito kama kupambana na ufisadi wanayafumbia macho!
Kimsingi, Tanzania hakuna udini bali uchovu wa kifikra na umaskini wa kunuka.
Sioni tatizo baina ya wakristo na waislam ukiachia mbali wahuni na matapeli wanaotumia dini hizi kuleta vurugu.Hatuwezi kuwahukumu waislam wote kwa ujuha na ajenda fichi za makundi madogo ya kitapeli yenye kufadhiliwa na maadui wetu.
Tumekuwa mafisadi hata wa kiakili kirahisi hivi? Mbona hatuongelei viongozi mafisadi wa kiislamu wanaowaibia na kuwatumia waislamu maskini sawa na wale wa kikristo wanavyowaibia wakristo?
ACHENI UVIVU WA KUFIKIRI na kulialika janga ambalo hamuwezi kuli-contain. Tukianza vurugu wengi wa watu wetu hawatakufa kwa matundu ya risasi bali, njaa baada ya kushindwa kwenda kuhangaika maana ni maskini mno; hawana hata ujanja wa kutorokea nje-hawana pasi za kusafiria wala pesa.
Tuwaacheni waishi maisha yao ya mahangaiko yanatosha, Tatizo la nchi yetu siyo udini bali ufisadi wa kimfumo hata wa kidini.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 24, 2014.

No comments: