How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday 12 December 2013

Mandela ‘anaenziwa’ na waliomtosa



INGAWA rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ameenziwa kwa marefu na mapana dunia nzima, kama marehemu Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere, ameenziwa na wale waliomtosa. 
Mandela amekufa akiwa mtu mwenye kukata tamaa kutokana na kuona jinsi chama chake alichokuwa tayari kukifia cha African National Congress (ANC) kilivyofisidika na kuchafuka mithili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Nyerere.
Ni bahati mbaya sana kuwa msiba wa Mandela ulitangazwa na kusimamiwa na watu wachafu wasiofanana naye hata kwa nukta. Mandela alishuhudia vituko vikubwa viwili nchini mwake. Kwanza, ilikuwa ni pale aliposhauri chama chake na mrithi wake Thabo Mbeki kuondokana na msimamo dhaifu na wa hovyo wa kudai kuwa hakuna ukimwi bali maradhi yatokanayo na umaskini. 
Ni bahati mbaya kuwa Mbeki hakumsikiliza Mandela ingawa baadaye alikuja kujutia msimamo wake hasa baada ya wabaya wake wakiongozwa na rais wa sasa Jacob Zuma kumuengua. 
Pili, Mandela alishuhudia makumi ya kashfa yakikiandama chama chake hasa yakimhusisha rais wa sasa Zuma ambaye amekumbwa na kashfa kuanzia za ngono hadi ufisadi wa kujipatia utajiri kupitia rushwa na kutumia pesa ya umma kujenga makazi ya kifahari kijijini kwake Nkandla.
Kimataifa, Mandela amekufa bila kusahau mataifa kama vile Marekani na Uingereza yalivyounga mkono utawala wa kibaguzi uliomfunga na kutaka kumuua. 
Nani mara hii amesahau jinsi mamlaka za Marekani zilikuwa na jina la Mandela kwenye orodha ya magaidi yake hadi hivi karibuni vyombo vya habari vilipopiga kelele na serikali kuona aibu? 
Ajabu ni hao hao wanaomzika na kumuenzi Mandela wakati ukweli ni kwamba walimsaliti na kumtosa?
Tumeanza hapo juu kwa kusema kuwa walimtosa Mandela sawa na Nyerere ndiyo leo wako vifua mbele eti kumuenzi. Je wanamuenzi au kumsanifu kama siyo kumtumia kujipatia kuungwa mkono na watu wao? 
Kama ilivyokuwa kwa Nyerere alipokufa msiba wake ulitangazwa na kusimamiwa na Benjamin Mkapa aliyempuuzia Nyerere kiasi cha kuuza kila alichokihifadhi kwa vizazi vijavyo hadi Nyerere akafunga safari kwenda China kunusuru baadhi ya rasilimali kama vile kiwanda cha Urafiki. 
Nadhani hakuna kilichomuuma Nyerere kama kuona Benki ya Taifa ya Biashara ikibinafsishwa kwa bei mchekea kwa makaburu wale wale waliomhangaisha shujaa mwenzake Mandela.
Kadhalika, Mandela amekufa akiwa na machungu hasa kushuhudia juhudi zake zikigeuzwa mtaji wa mafisi na mafisadi hata akiwa hai. Ukiangalia hata baadhi ya nukuu zake utagundua hili. Kwa mfano, aliwahi kusema, “Let there be work, bread, water and salt for all.” Yaani kazi kwanza, mkate, maji na chumvi kwa wote. (Tafsiri ni yangu). 
Huwezi kuwa na mkate na chumvi kwa wote kupitia uuzaji na uchuuzi wa wa nchi na watu wake wala wizi na ufisadi. Hapa Mandela alimaanisha viongozi kuchapa kazi na kuhakikisha matunda ya jasho la taifa yanafaidiwa na wote na si baadhi ya watu kama ilivyo sasa ambapo makuwadi na marafiki wa Zuma ndiyo wanaotumbua nchi huku walioifia wakifa maskini. 
Pia Mandela aliwahi kusema, “After climbing a great hill, one only finds that there are many more hills to climb.” Yaani baada ya kupanda milima unajikuta unapambana na vilima vingine,(tafsiri ni yangu). 
Hapa bila shaka Mandela alimaanisha vikwazo vitokanavyo na utawala wa kifisi na kifisadi ambapo mlima ulikuwa ubaguzi wa makaburu na vilima na hivi vijikaburu vyeusi vinavyogeuza madaraka kuwa mali ya ukoo na genge fulani kama ambavyo inaanza kuzoeleka katika bara la Afrika.
Ni bahati mbaya sana kuwa wanafiki na mafisi waliomsaliti Mandela ndiyo sasa wameshikilia hatamu wakila utamu kama ilivyotokea kwa Mwalimu Nyerere. 
Nani alijua kuwa kungetokea EPA na Kagoda kwenye nchi ya aliyopigania Nyerere? Nani alitegemea miaka 52 baada ya kujitawala tungekuwa na watu wasiojua hata wanachofanya wala kutafuta kwenye uongozi? 
Mwalimu aliwahi kuonya kuwa Ikulu ni patakatifu pa patakatifu. Hata kabla hajafa paligeuzwa pachafu pa pachafu na pango la wizi hadi akaamua kung’aka ingawa wahusika walimponda na kumpuuzia. Matokeo yake tulishuhudia kashfa za Kiwira sawa na kashfa ya Nkandla huko Afrika Kusini.
Hebu tuangalie nukuu nyingine ya Mandela, “As I have said, the first thing is to be honest with yourself. You can never have an impact on society if you have not changed yourself... Great peacemakers are all people of integrity, of honesty, but humility.” Kama nilivyosema, kitu cha kwanza ni kuwa mkweli kwako binafsi. Huwezi kuwa na athari kwa jamii bila kujibadili. 
Wapatanishi ni watu wenye ithibati na uaminifu pia utiifu, (Tafsiri ni yangu.)
Naye mwalimu Nyerere alituachia ya moyoni hasa pale aliposema alikata roho akiwawazia Watanzania wake ambao aliwaacha kama yatima.
Ingawa ni mapema kusema, baada ya kumaliza matanga na maombelezo mengi yataibuka kuhusiana na jinsi Mandela alivyotoswa na wanaojifanya kumuenzi. Wanamsanifu wakijidai wanamsifia. 
Nani mara hii kasahau viapo vilivyotolewa wakati wa mazishi ya Nyerere ambapo wajivuni waliomuangusha walisikika wakisema bila aibu, “Mwalimu tunaapa kuwa tutakuenzi na kufuata yale uliyosimamia.” 
Waingereza wana msemo usemao, easier said than done. Ni rahisi kusema kuliko kutenda. Je ni wangapi tutawasikia au tumewasikia wakisema eti watamuenzi Mandela wakati matendo yao ni machafu kiasi kwamba hawakupaswa hata kushiriki mazishi yake? 
Ni nchi ngapi zilimsaliti wakati wa mapambano ya kulikomboa taifa lake? Ukiachia nchi za Uingereza, Marekani, Israel, Ufaransa, Ujerumani na nyingine zilizoshirikiana na kustawisha utawala wa kibaguzi wa kikaburu  nani, kwa mfano, amesahau kirahisi kuwa nchi za Kiafrika kama vile Kenya , Malawi , Zaire ya wakati ule na nyingine nyingi zilimsaliti lakini leo viongozi wake ndiyo wako kimbelembele kwenda kuhudhuria mazishi yake? 
Tanzania hatujivuni. Chini ya Mwalimu Nyerere tulimsaidia Mandela hadi kumpa pasi ya kusafiria. Je wangekuwa watawala wa sasa wangepata ushupavu na moyo wa kufanya hivyo? Nina wasi wasi sana. 
Hakika waliosema kuwa kwenye msafara wa mamba na kenge wamo hawakukosea. Tumeshuhudia wenye dhambi wengi wakienda kumzika mtu mwema Mandela.
Tumalizie na nukuu ya Zuma, “What made Nelson Mandela great was precisely what made him human. We saw in him what we seek in ourselves and in him we saw so much of ourselves.” Yaani, kilichomfanya Nelson Mandela mtu maarufu ni haswa kile kilichomfanya mtu. 
Kupitia kwake tunajitafuta na tunajiona ndani yake. Si kweli. Sijui kama Zuma anaweza kufananishwa na Mandela au Mkapa na Nyerere.
Chanzo: Dira Desemba, 2013.

2 comments:

Anonymous said...

Mkuu yote uliyoyaeleza ni kweli, nimeangalia kipindi cha bbc cha question time live toka j'burg, wasouth wanasema yote uliyoyaelezea na wanasema na wao wanataka na wao wapewe arddi na wanamuunga mkono Robert Mugabe na wapo waliofikia kusema wapo tayari kwa lolote kwani hawaoni faida ya utawala wa sasa ambao umejaa wizi wa mali ya umma na kuwaacha rai walio wengi wakiwa katika hali duni, pamoja na Peter Hann mbunge wa labour toka Wales kujaribu kutetea lakini watu wamempa ukweli wake.Hivyo uko sawa,kuhusu Mandela na Nyerere kwani niliyoyasikia kwa wasouth yana onyesha huko tuendako kutakuja kuwa na matatizo makubwa.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon shukrani kuongeza wigo wa ukweli na welewa kwenye makala hii. Pamoja daima! Ukweli ni kwamba tulichoonyeshwa kwenye TV ni choreographed truth which has eclipsed the real Truth. Hata hivyo soon the Truth'll come forth forcefully.