Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding
Saturday 7 December 2013
'Vyangu wa kisiasa koma kujiuza kwa mafisadi'
Baada ya mlevi kutangaza nia ya kugombea urais na kupata walevi wengi wakisema watampa kura ya kula, ameamua awe mkweli.
Anaamini ukweli huweka huru hata kama utawauma baadhi ya wanoko hadi wakamnyima kura kwa vile hayuko tayari kuwapa kula.
Kilichomfurahisha mlevi ni ile hali ya kuzidi kujenga chama chake cha wanywaji.
Hatuna migogoro chamani wala watu wanaosaliti chama kwa kujifanya wao ni maarufu kuliko chama, hivyo watakacho lazima kitimizwe hata kama ni cha kipumbavu na kuvunja katiba ya chama kama ilivyotokea hivi karibuni ambako Mzigo, sorry, Mzito Kabwela alitaka ajifanyie atakavyo tena kwa mkumbo.
Hayo ya Chakudema tuwaachie wao wenyewe wavuane madaraka na kufukuzana kutokana na kusalitiana na kuasiana kama wanavyosema. Hebu sasa niwachapie stori yangu ambayo imenilazimu kuandika waraka huu.
Naandika kwa masihara lakini kwa chuki na seriousness vya hali ya juu.
Naandika kuwaambia wajinga ninaowalenga wakome na kukomaa hata kama wamekataa kukomaa na kujitegemea kiasi cha kujigeuza vyangudoa wa kisiasa tena wa kiume.
Basi wajameni, nikiwa kwenye matembezi yangu mitaa ya Ilala mitaa ya Kilwa na Songea, si nikasikia tapeli moja tena jitu zima linalojiita shehe wakati ni ganga tapeli la kienyeji likijisifu kuwa yeye na wazee ombaomba walimtoa upepo Eddie Lowassa hivi karibu walipojipitisha kwenye ofisi yake kujikomba na kuomba.
Kwa vile zee hili jambazi la zamani na haribifu la ndoa za watu kutokana na kujifanya linatibu magonjwa ya akina mama, halinijui liliendelea kujisifu upumbavu kwenye kijiwe cha kahawa.
Nilitamani nilizabe vibao kwa kufanya wazee waonekane ombaomba na mtu mzima hovyo. Kwanza, niseme wazi na kwa makini tena kwa kimombo, please beggars and conmen looking for mshiko from fisadis don’t approach me looking for mshiko. I’ll order boozers to skin you alive. Naona yule mdingi ameishanuna nusu kupasuka. Huna haja ya kupasuka babaangu. Nisemayo ni kweli tupu sema wapo wasiotaka kuupokea na kuukubali ukweli ili wawe huru kama mimi.
Imeandikwa kuwa mkijua kweli itawaweka huru. Nani huyu asiyetaka huru? Hata hivyo poa babu yangu. Naongelea baadhi ya mizee mitapeli na vyangudoa wa kisiasa inayojipitia kwenye waroho wa madaraka na mafisadi ili waipe makombo na iuze kaya kwa mafisadi na majambazi halafu ikishaingia mkenge na kuanza kusota inakuwa ya kwanza kupiga kelele wakati tatizo ni uroho na upogo wao.
Mkome na mkomae akina Njalambaya au Njalambi kama wasemavyo wajomba zangu.
Basi zee hili lenye jina lifananalo na kujidai liliendelea na upuuzi wake hadi nikaondoka. Na kama si kuogopa ndata kunibambikia kesi na kuja kulitetea kwa vile linaunga mkono chama chao ndata, huenda ningelinyonga kwa mikono yangu na kuondoka pale kwenda kuyatembezea bakora yale mengine ambayo hayakuwa kwenye kijiwe kile siku ile.
Hakuna kilichonikera kama tambo na upuuzi wake kuwa vilikatiwa mshiko wa nguvu wakati mshiko wenyewe ni wa siku chache na baadaye yataendelea na njaa zao.
Lilivyokuwa likijisifu na kumsifia fisadi upuuzi nilitamani ningekuwa na gun nilimwagie shaba ili majuha na mafisi kama haya yanayokwamisha kaya yetu yapungue.
Je! yako mangapi huko nje? Mijitu haikutaka kutafuta riziki kihalali na kwa wakati sasa inazeeka vibaya kwa kujiuza kwa mafisadi. Ingejiuza yenyewe na si kuviuza vitegemezi vyetu na mustakabali wao.
Nasema nipeni mimi kura ya kula ili nikomeshe hii mifisadi inayojipitisha ikimwaga mwaga rushwa itokanayo na pesa ya kuuza kaya yetu kwa madudu kama Richmonduli AIPITIELO, Songagas na majambazi wengine tunaowajua. Hata hivyo, nilipata somo kubwa kuwa bado mijitu iliyokataa kukua na kama imekua haikukomaa na kama imekomaa, imekomaa kwenye upuuzi na uendekezaji njaa.
Hata hivyo, sikushangaa mizee ya namna hii kujiuza kwa vile ilishiishiwa utu na akili. Hebu fikiri unakuta familia nzima ni waganga wa kienyeji unategemea nini?
Hili zee ninalosema lina toto lake tapeli lililokuwa likiwaibia wajinga kuwa linaweza kuongea na majini pale kwenye mitaa ya Migomigo lilipofungua kujiofisi.
Hivi kuongea na majini unadhani mchezo? Shame on you! Unaongea na majini au unaongea na majinuni na majuha? Ama kweli wajinga ndiyo waliwao. Hata hivyo, sishangai kwenye kaya yetu. Nani hajui kuwa siku hizi tuna matapeli wengi toka Unigeriani na UDRC wakijfanya wachungaji wakati ni wachunaji?
Hivi kesi ya kubaka ya yule aliyekuwa mume wa Angelina Chiba-lonza imeishia wapi kule Dom ambako nasikia ndata walikuwa wakimkingia kifua kwa vile anawapa njuluku?
Hawa jamaa ni wa kufunga maisha ili wakome kuwaibia walevi wetu. Mijitu inauza mibwimbwi inajifanya michungaji, mishehe na upuuzi mwingine. Mnadhani hatuwajui?
Nikichaguliwa kuwa rahisi mjue mtakoma. Sitawadekeza kama yule jamaa anayesema ana orodha ya majina yenu.
Nikiwa rais nitawanyonga badala ya kuwahadaa walevi kwa kula na kunywa na mateja kama jamaa anayewafuga wauza bwimbwi. Hayo tuyaache.
Turejee mikakati ya mlevi kutoruhusu vyangudoa wa kisiasa kumuibia. Kwanza, sina mshiko wa kuchezea wala kuhonga. Pili, mimi si mla wala mtoa rushwa kama hao wanaotapeli na kutapeliwa kwa kuotea ukuu.
Tatu, mimi si fisadi mwenye kuwaibia watu na kuwahonga pesa hiyo hiyo niliyowaibia. Nne, mini sijanunuliwa na mafisadi wawe wa ndani au wa nje. Maana mzee Mchonga alituusia kuwa ukiona mtu anawanunua wenzake jua naye amenunuliwa. Hivyo, hao wanaowahonga matepeli wenzao kama hii mizee niliyotaja hapo juu, wamenunuliwa ili kuwauza walevi kama watafanya makosa wakawapa ulaji. Jamaa kama hawa ni wa kuogopa kama ukimwi.
Pia ifahamike kuwa mlevi hana haja sana na urais kiasi cha kuwachuuza walevi wenzake. Ukweli ni kwamba, mlevi hawezi kununulika kwa vile mipombe na mibangi ikipanda atapayuka na siri itamwagika.
Kwa wale wanaopenda dezo na kujidhalilisha kwa wagombea nawaambia kabisa, mkija kwangu nitawapa majembe mwende vijijini mkalime na kujitegemea badala ya kukaa mijini mkiuaibisha utu uzima.
Mijitu iliambiwa isome ikaogopa umande sasa imezeeka inaanza kufanya mambo ya kitoto ambayo yalipaswa yafanywe na wajukuu zake.
Msiseme natukana. Wapo wazee waliopiga vitabu wakaitumikia kaya na kustaafu na uchache wao. Wako mijini wakitumia lakini si kujiuza kama vyangu wa Kinondoni Makaburini.
Leo nawakumbuka washikaji zangu wa stendi ya mabasi Tanga na mpakani Horohoro waliokuwa wakinipa tafu. Jamaa leo mmekumbukwa na mshikaji wenu Mwana wa Adam. Nawasalimuni jamanini.
Chanzo: Nipashe Jumamosi, Desemba 7, 2013.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment