Akiwa mkoani
Geita, rais Jakaya Kikwete alikaririwa wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusambaza
umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko wa Changamoto za
Milenia (MCC) kwenye Kijiji cha Katunguru/Nyamtelela wilayani Sengerema, mkoani
Mwanza akisema kuwa wanaombeza wataumbuka ifikapo 2015. Heri ingekuwa hivyo.
Hata hivyo, sijui kama Kikwete anayaona mambo kama yalivyo au anachukuliwa na
wimbi la kujiridhisha na kujiisha pepo kwa kuona mawenge. Kama Kikwete anataka
tunaombeza tuumbuke basi afanye yafuatayo:
Mosi, apambane
na ufisadi uliomzunguka ambao hata hivyo, harufu yake ni kali kiasi cha hata
kunguru kuihisi. Awawajibishe marafiki zake waliotuhumiwa moja kwa moja
kujihusisha na ufisadi na uhujumu wa taifa. Nitaumbuka kama Kikwete
atawashughulikia, kwa mfano, wezi wa Kagoda, EPA, Richmond, Sukita, Meremeta,
Mwananchi Gold, Buzwagi na ujambazi mwingine. Nitaumbuka kama Kikwete
atawashughulikia watuhumiwa wanaojulikana mfano Edward Lowassa, Nazir Karamagi,
Rostam Aziz, Andrew Chenge, Peter Noni, Japhet Mangula, Idris Rashid na wengine
wengi.
Pili, ataje mali
zake ili umma ujue ana mali kiasi gani na amezichuma vipi. Asisahau mali za
mkewe ambaye kupitia NGO yake ya WAMA atakuwa bila shaka ana pesa ya kutosha
tofauti na anayostahili kuwa nayo kihalali. Kama atavunja NGO hii ya shaka na
kuwataarifu watanzania jinsi alivyogundua kuwa inamtia doa basi huenda
tukaumbuka. Akiendelea na whitewash na window dressing asitegemee kuumbuka
zaidi ya kuimarika zaidi na kupata la kusema.
Tatu, aandike
katiba mpya isiyo na uchafu wala athari za chama chake. Nilishaliongelea hili
kuwa Kikwete amshinde shetani anayemrubuni achakachue katiba ili kulinda
maslahi ya chama chake.
Nne, Kikwete
atimize ahadi yake ya maisha bora kwa wote. Hili litasaidia kufuta kauli yake
ya kushindwa isemayo'raha jipe mwenyewe' akimaanisha kila mmoja ajiletee maisha
bora hata kama kufanya hivyo kunahujumiwa na ufisadi uliotamalaki nchini huku
Kikwete akiangalia.
Nne, ataje vigogo wa mihadarati ambao alisema
ana orodha yao mnamo mwaka 2006.
Tano, atoe
maelezo kuhusiana na tuhuma kuwa yeye ni miongoni mwa mafisadi wakubwa
waliotajwa na katibu mkuu wa CHADEMA,Dk Wilbrod Slaa kule Mwembe Yanga, 2007 kwenye kile alichoita
list of shame.Kwa kujua ukweli wa mambo Kikwete aliogopa hata kumtaka Dk Slaa
alete ushahidi. Anadhani haya yamesahaulika ndipo atuumbue? Je hawa mafisadi
wamelitia taifa hasara kiasi gani na pesa waliyofisidi ingejenga miradi
mingapi?
Sita, atoe
utetezi wake kuhusiana na kuhusishwa na kashfa za EPA, List of Shame iliyotajwa
hapo juu na Richmond ambazo amekuwa akikwepa kuziongelea.
Saba,
asambaratishe utawala wa kujuana ambao umeshindwa kuwawajibisha watuhumiwa wa kashfa mbali mfano, mawaziri waliotuhumiwa
kughushi ambao ni Makongoro Mahanga, Mary Nagu, Emanuel Nchimbi, William Lukuvi
na balozi wake nchini Ubelgiji Deodorus Kamala, katibu mkuu wa chama chake
Abdulrahaman Kinana aliyetuhumiwa kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu na
wengine waliotamalaki kwenye chama chake na serikali yake. Asipowawajibisha na
kuwajibika hata ajisifu na kujiridhisha vipi hatamuumbua mtu bali yeye
mwenyewe.
Nane, ahakikishe
anakusanya kodi na kuitumia kwa uangalifu na busara huku akiziba mianya ya
ukwepaji na misamaha ya kodi vilivyotamalaki. Aachane na matanuzi ya kusafiri
hovyo nje ya nchi akiandamana na misafara mikubwa kwa kisingizio cha kuomba.
Huwezi kutegemea kuomba omba halafu ukajisifu kuwa umeleta maendeleo kiasi cha
kuwazodoa wanaokupinga kwa haya.Mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe na si
wafadhili ambao hutoa misaada na mikopo kwa maslahi yao na si yako. Laiti kama
Kikwete ataacha nchi angalau imepunguza utegemezi kwa wafadhili ambapo bajeti
ya taifa kwa sasa inawategemea kwa asilimia 40, huenda tukaumbuka.
Tisa, asimamie
vizuri raslimali na pesa ya umma iibiwayo kila mwaka kama inavyofichuliwa na
mdhibiti na mkaguzi mkuu wa fedha za umma.Imefikia mahali wezi wa fedha za umma
wanajiona kama serikali ndani ya serikali. Rejea kiwango cha pesa zinazoibiwa
kinavyoongezeka mwaka hadi mwaka huku kukiwa hakuna waliowajibishwa achia mbali
namba ya wawajibishwa kuongezeka.
Kumi, thamani ya
miradi anayojisifia kujenga na kuzindua ifanane na miradi husika.Huwezi kusifia
miradi ambayo imejengwa chini ya kiwango baada ya wahusika kukatiwa ten percent
yao na kusunda nje kama ilivyotokea kwenye ununuzi wa rada mbovu na ndege ya
rais. Maana ukiangalia kwa mfano shule za kata anazojivunia, licha ya kutokuwa
na walimu wa kutosha, hazina vifaa muhimu na hata matokeo yake kila mwaka ni
kilio kwa wazazi wenye watoto kwenye shule hizo. Hata pesa inayosemekana
kutumika kuzijenga ikilinganishwa na shule zenyewe utakuta madudu matupu.
Kumi na moja,
awajibishe viongozi wengi waliotamalaki kwenye chama chake ambao anajua udhaifu
wao ambao ni kikwazo kwa maendeleo ya nchi. Kwa mfano katika hafla hii alikaririwa
akisema, "Mmekuwa hodari wa kushupalia dosari zinazosemwa na wapinzani na
kuacha mazuri haya?” Hapa anakemea tabia
ya nyani haoni kundule ashakum si matusi. Ameona fika ubovu wa CCM kiasi cha
kuamua kuwapasha wazi bila kujali watasuka au kunyoa.Hata hivyo, hawatabadilika
kwa vile wanamjua mtu wao alivyo mwepesi wa kusema na mgumu wa kutenda.
Kama wahusika mfano spika wa bunge na naibu
wake wangewajibishwa, kungekuwa na sababu ya Kikwete kutuumbua.
Kumi na mbili,
Kikwete ahakikishe anafanya yaliyopendekezwa hapo juu ndani ya muda mfupi
badala ya kuyafanya kwa mdomo na hotuba tamu majukwaani. Watanzania wamepigika
sana chini ya utawala wa Kikwete. Hivyo, wangetaka kuona na si kusikia ambavyo
Kikwete atabadili welekea wa mambo kutoka kwenye hali tete ya ufisadi na
kutowajibika kwenda kwenye maadili na uwajibikaji.
Mwisho, haitoshi
kwa Kikwete kusema atawaumbua wakosoaji ambao siku zote amepuuzia ushauri wao
wa maana na dhati. Sana sana, kama ataacha kutumia bunge kuwahujumu wapinzani,
huenda anaweza kufanya hayo yanayopaswa kufanywa ili kuweza kuwasuta wakosoaji
wake. Tunangoja kwa hamu sana Kikwete atusute vinginevyo siku ya siku tutamsuta
yeye bila kujali kuwa ataacha serikali dhaifu na nchi iliyofilisiwa.
Tutamuandama kama tunavyowaandama Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi walioweka
mizizi ya ufisadi na uhovyo nchini.
Chanzo:Dira Desemba, 2013.
No comments:
Post a Comment