How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday, 16 December 2013

Mlevi alivyohudhuria mazishi ya Madiba


 
Walevi wote nawasalimuni sana na leo nina habari njema sana ambayo ilikuwa siri. Na hii ni kweli. Si rongorong, kamba wala fix bali ukweli mtupu. Mna habari mimi na Mandela ni dugu moja? Babu wa bibi wa bibi wa bibi yangu alizaliwa Mvezo karibu kabisa na nyumbani kwa akina Madiba. Hata baba yake marehemu chifuGadla Mphakanyiswa aliwahi kupiga ulabu na babu yangu.
Mimi na Diba tunafanana sana. Kwanza, majina yetu yanaanza na herufi “N”. Pili, majina ya baba zetu yanaanza na “M”. Tatu, wote ni wasupu yaani flamboyant and handsome kwa lugha ya kimakonde na isiyo ya kitaalamu. Nne, wote tuliandika vitabu, yeye “Long Walk to Freedom”, mimi “Saa Ya Ukombozi” (Long Hour to Liberation).  Tano, wote tulitetea watu wote duniani yeye wasauzi mimi walevi. Sita, wote hatuogopi mtu bali kumpa vipande vyake kama alivyofanya kwa makaburu sawa nami ninavyofanya kwa mafisadi ambao kimsingi nao ni makaburu.  Yeye aliteswa na makaburu wakati mimi niliteswa na mwalimu wangu aliyeitwa Kaburu. Anyways, hayo tuyaache. Wenye kutaka kubisha au kutaka kujua Zaidi waje waninunulie kanywaji niwape stori ya jinsi ninavyotoka kwenye ukoo (isiduko) mteule wa akina Diba wa Madiba Madibane. Ukoo wangu unaitwa Mkhwanazi msichanganye na waswahili Mkweaminazi.
  Cha mno, leo nawaletea salamu toka Sauzi kwa familia ya Mzee Madiba aliyetutoka hivi karibuni. Niliandamana na bi mkubwa mpenda safari za majuu. Nay alikwenda kumzika shemeji yake. Tofauti na washikaji zangu fulani waliofanya ujumbe wao kuwa siri, mimi nilifanya kila kitu wazi wazi. Wao walifanya misafara yao kuwa top secret kuepuka kustukiwa na makapuku wanaofuja njuluku zao. Hata hivyo, nilikuwa nimechoka kwa safari ya ulaya lakini sikupenda ujiko huu unipite hivi hivi. Hivyo nilikwenda na hangovers zangu za majuu hadi Sauzi.
Kuna kitu kilinifariji kwenye msiba nacho ni watu kujua unafiki wa wakubwa zetu. Si walimtolea Jake Zuzuma uvivu na kumzomea kila alipoamka kuongea kwa vile wanajua chafu yake.  Kilichonisumbua wakati wa misa ya kumuombea Diba ni ile hali ya kujiuliza kweli kama madude na mabuda waliohudhuria mazishi yake wannafaa kukaribia hata jeneza lake achia mbali kuingiza miguu yangu kwenye viatu vyake vikubwa kama nyumba. Diba alikuwa mlevi kama mimi, ila hakuwa fisadi na mpenda makuu kama wao. Kama mimi, alipenda watu na kuchanganyikana nao kama vile ninavyochanganyika na walevi hata wa mataptap. Pia Diba  alikuwa akijihisi kama  mkosefu aliyejijua siyo kama hawa wahalifu wanaojifanya watakatifu na watukufu wakati ni wachafu na wajaa chafu na wataka chafu na watenda chafu kila siku na kila mahali.
Hakuna kitu kilinikera nusu niamke kwenye sehemu ya wageni maarufu na kwenda kumzaba mtu kibao kama kuona wale waliomsaliti walivyokuwa wakijisifu na kujidanganya kuwa watamuenzi wakati walishaanza kubungua kazi yake. Sikuishia hapa. Nilijiuliza swali jingine. Je ni pesa na muda kiasi gani wazururaji wasiofanana na Madiba walitumia tena ya kuwaibia walevi?
Ajabu alipokuwa akiumwa wajivuni hawa hawakumtumia hata salamu achia mbali kumjulia hali. Kumbe walingoja afe wamtumie kujipatia ujiko! Kumbe walingoja afe wamsanifu kama walivyofanya?
Ajabu hata wale waliomuita gaidi na kutunza jina lake kwenye vitabu vya magaidi walikuwapo. Joji Kichaka unanipata? Hata wale waliomsusa wakaunga mkono utawala wa kishenzi wa kikaburu eti nao walikuja kumsifu na kumzika! 
Nilipokuwa nikipita pita kwenye mitaa ya Vilakazi huko Soweto yalipo makazi ya kwanza ya Madiba nilishuhudia hata wale waliombagua au makuwadi wao wa kigabacholi eti wakinunua kumbukumbu zake kama vile skafu, picha na kila kitu.  Ghafla Madiba alieguka lulu kiasi hata cha bunge la kwa mama kule kwa wakameruni eti kumuenzi wakati ni wale wale waliokuwa wakiusaidia utawala wa kikaburu kumsaka ili kumnyotoa roho. Wanafiki siku zote hawana aibu wala utu. Yaani watasha na wa kwa Joji kichaka walivyokuwa wakimkwepa Madiba zama zile akiitwa David Mutsamayi kukwepa kukamatwa, sikutegemea kuwa wangejitoa kimasomaso hivyo. Heri watu kama Kamuzu na Thatcher na Reagan waliishajifia. Si ajabu nao huenda wangejidai wanakwenda kumzika na kumuenzi wakati walimtenza.
Nilicheka nilipomuona rais Uhuhu Kinyata eti naye akienda kumzika Diba wakati nchi yake na Malawi walimwekea ngumu Diba zama zile.
Diba alikuwa mlevi wa haki na demokrasia. Ajabu japo si wote, amezikwa na baadhi ya wakandamizaji wa demokrasia na dhulumati wa umma wao.
          Wote walifanya makufuru yao. Hakuna walioniudhi kama mashoga kudai kuwa Diba aliwaruhusu wafanye uchafu wao. Ajabu hata wanene wa taifa lile hawakuwakemea kwa uongo wa mchana na mchafu kiasi hiki. Watu wengineni kweli ni viumbe wa ajabu. Wanamsingizia hata marehemu? Hata hivyo, wana tofauti gani na wale waliomwangusha halafu wakaanza kujifanya wanamuenzi. Huwezi kumuenzi Madiba wakati unakula rushwa aliyoichukia. Huwezi kumuenzi Diba wakati ukishiriki ufisadi, mihadarati, wizi, ufujaji wa fedha na raslimali za walevi. Ukifanya hivyo wewe ni mshenzi na mnafiki wa kunuka tu hata kama utakuwa ukidanganywa kuwa u mtukufu. Huwezi kuwa mbaguzi ukamuenzi Madiba. Jamaa zangu wanaotesa wafanyakazi wa nyumbani wa Kiswahili mnanipata? Veve iko fanya baya sana. Hata Swahili iko tesa lakini hapana bagua wao.
Diba alikaa madaraki miaka mitano wakati nyinyi mnakaa hamsini halafu mnasema eti mnamuezi! Shame on you! Kama mnamuenzi basi achia ulaji kama alivyofanya siyo mgoje kuondolewa kigadafigadafi mkilia kama vichanga.
Madiba hakushiriki madaraka na watoto wake wala marafiki zake. Je nyie mnafanyaje kulaleki?
Kwa vile bado nina majonzi makubwa ya kumpoteza ndugu na rafiki na mlevi mwenzangu Diba, leo sitaandika mengi. Hamba kahle Diba, lala ngoxolo tata. Leo salamu zangu ni kwa wanyonge wote duniani aliowapigania Diba.
Chanzo: Nipashe Jumamosi 14, 2013.

No comments: