The Chant of Savant

Monday 16 December 2013

Ghasia,Mgimwa Mwanri, Majaliwa na wengine wawajibishwe




 Mawaziti saba watoswa 
KWA mara ya pili, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekunjua makucha yake. Hii ni baada ya kuwataka mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Hawa Ghasia na manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa wajipime na kujiwajibisha. 
Hii ni baada ya wizara hii kuvurunda kwa muda mrefu ambapo serikali za mitaa zimekuwa zikiiba pesa kwa mabilioni karibu kila mwaka. Rejea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha ya Serikali (CAG) ambayo karibu kila mwaka inafichua madudu na wizi wa mabilioni ya shilingi lakini hakuna anayewajibishwa. Ajabu ni kwamba kila mwaka pesa inayoibiwa inaongezeka.
Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi nchini vikiwahusisha wakubwa Serikalini, wapo wanaoona kama dhana nzima ya kujipima ni kama kulindana au kuwachezea wananchi. 
Kwanini wabunge wawape watu nafasi ya kujipima wakati walishindwa kufanya hivyo kwa muda mrefu? Kwanini kujipima wakati mtu amebainika wazi kufanya madudu? 
Je hii ni njia fichi ya kulindana na kuuhadaa umma hasa wakati huu kuelekea kwenye uchaguzi ambapo kila chama kinataka kionekane kizuri kwa kuficha uchafu wake? Je ni kwanini wabunge waliogopa kuwaambia wazi watuhumiwa kuwajibika badala ya kuwapa fursa ya kujipima? Je kwa namna hii wabunge hawajashiriki haya madudu na kuyabariki?
Je wahusika watajipima hasa ikizingatiwa kuwa utamaduni wa kujipima na kujiwajibisha ni kitendawili nchini ukiachia mbali kuwahi kutumiwa na Edward Lowassa waziri mkuu aliyetimliwa kutokana na kubainika kushiriki vilivyo kwenye kashfa ya Richmond iliyoliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya shilingi? Hili ni swali linalowasumbua wachambuzi wengi. Ikitokea jamaa wakaamua “kula jiwe” je waliowateua watakuwa na ubavu wa kuwawajibisha?
Tamisemi iko chini ya ofisi ya waziri mkuu, Mizengo Pinda. Je ni kwanini bunge limemuacha waziri mkuu katika shinikizo hili la kujipima?  Je ilikuwaje wizara ambayo iko chini ya waziri mkuu ivurunde yeye asichukue hatua? Je kutofanya hivyo hakukusaidia kuvurunda zaidi kiasi cha kumfanya naye abebe lawama chini ya kile kisheria huitwa vicarious accountability yaani ambapo mtu hulaumiwa kwa wadhifa wake? 
Hata chini ya dhana ya uwajibikaji wa pamoja, collective accountability, Pinda hawezi kuponyoka kwenye shinikizo hili. Ili kuondoa kuonekana kama bunge linawatoa kafara mawaziri wahusika, na waziri mkuu anapaswa kuunganishwa. Kwani hii ni wizara ambayo iko chini ya ofisi yake. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), Rajabu Mbaruku alikaririwa na vyombo vya habari akisema, “Hata waziri mkuu nimemtaja kwa jina, na nimesisitiza kama ananisikia kuhusu ofisi yake.” Je kama waziri mkuu ametajwa ni kwanini hakuunganishwa na mawaziri wake katika kutakiwa kuwajibika kwa madudu haya?
Ni bahati nzuri kuwa waziri mkuu anajua kila kitu ingawa aliacha mambo yajiendee.  Mei 9, 2013, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 29 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika hoteli ya Sundown Carnival, nje kidogo ya Jiji la Arusha, waziri mkuu alikaririwa akisema,  
“Tatizo hili ni kubwa na lina sura mbili kuu. Moja ni kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya watumishi na madiwani katika usimamizi wa fedha za Serikali za Mitaa. Baadhi ya madiwani wamediriki kushirikiana na watumishi wasio waaminifu katika kuhujumu fedha za umma. Pili, ni Watumishi wa Serikali za mitaa kushindwa kutekeleza wajibu wao hivyo kulipwa mishahara ambayo hawaitumikii ipasavyo.” 
Huu ni ushahidi tosha kuwa waziri mkuu na mawaziri wake wanajua kila kitu. Wanajua mbinu zinazotumika kuhujumu taifa na wanaofanya hivyo. Sema hawataki kuwawajibisha wahusika kutokana na sababu wanazojua wenyewe. 
Kutochukua hatua kwa madudu unayofahamu yapo ni uzembe wa hali ya juu pia kushiriki katika kulihujumu Taifa kosa ambalo halipaswi kutolewa nafasi ya kujipima zaidi ya kuwawajibisha wahusika. Wahusika wameonyesha uzembe wa hali ya juu. Hivyo, kuwapa fursa ya kujipima na kuamua ni kupoteza muda. Kwani, kwa uzoefu na uzembe wao, hawatafanya hivyo. 
Ni bahati mbaya kuwa hili si tukio la kwanza kuwahusu mawaziri na watendaji wazembe serikalini. Yaliishia wapi mashinikizo kwa waziri wa Elimu na Ufundi, Shukuru Kawambwa pale wazira yake ilipovurunda kwenye elimu? Si anaendelea kupeta na kutesa kama wasemavyo watoto wa mjini?
Kwa watu wenye kuwa na uchungu na taifa lao na wanaojua majukumu na wajibu wao, kitendo cha ripoti ya mkaguzi mkuu wa fedha za serikali kufichua madudu kila mwaka na wasichukue hatua ni jinai ya aina yake. Inashangaza hata wale waliowateua kuendelea kuwavumilia watu wao. Je huu nao ni mtandao mkubwa zaidi ya ile anayosema Pinda? 
Kwa wanaojua jinsi madaraka yanavyotafutwa nchini kwa kutumia pesa safi na chafu, si ajabu ikawapo mitandao inayotumia serikali za mitaa kujichumia pesa ya kutumia kuwahonga wapiga kura. Isitoshe, hali imefikia pabaya hadi wabunge wanakamatwa wazi wazi wakiwatoa rushwa watendaji wa serikali za mitaa ili kupitisha hesabu zao mbovu. 
Je kwa namna hii hawa wanaweza kuwajibishana? Ingawa si wabunge wote waliotuhumiwa kudai na kupokea rushwa toka kwa watendaji wa serikali za mitaa, ushahidi uliopo ni kwamba huu mchezo upo na haukuanza jana wala juzi. Ni bahati mbaya kuwa wakubwa wameendelea kunyamazia jinai hii. Tuangalie upande mwingine wa sakata hili. Bunge ndiyo limetoa nafasi kwa wahusika kujipima na kufanya maamuzi magumu. Je wasipofanya hivyo bunge litawafanya nini na lini?
Kuhusiana na uwepo wa mtandao wa wizi ndani ya Tamisemi, Mbaruku anatoa jibu. Alikaririwa akiliambia bunge akisema, “Kamati imebaini kwamba Tamisemi imekuwa ikitumia mtindo huu kuwalinda watumishi mafisadi ndani ya halmashauri na kuifanya kamati iamini Tamisemi ni sehemu ya mtandao huu.”
Je hapa kuna ushahidi mwingine unaotakiwa au kutoa fursa kwa watu kujipima na kuchukua uamuzi zaidi ya kuwachukulia uamuzi na kuwashitaki ili mahakama ipime ukubwa wa makosa yao na kutoa adhabu ili liwe funzo kwa wengine? 
Nani anamdanganya nani hapa kama ukweli wote uko wazi na unajulikana kama alivyobainisha Mbaruku? Tunashauri wahusika wawajibishwe mara moja badala ya kupoteza muda kwenye kujipima.
Chanzo: Dira Desemba, 2013.

No comments: