Msomaji wangu mmoja aliwahi kunitumia ujumbe mfupi akiuliza
ni kwani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kupuuzia sauti za umma unaotaka
kusitishwa kwa bunge hil kutokana na kuendelea kinyume cha sheria. Japo
nilimjibu msitari miwili, baada ya hapo lilinijia wazo la kuendelea kumjibu kwa
urefu yeye pamoja na wale wenye swali hilo au mengine yanayofanana nalo.
Je
kwanini CCM haitaki kusitisha BMK au kurejesha rasimu halali iliyowasilishwa na
Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba iliyoongozwa na jaji Joseph Warioba? Jibu la
swali laweza kuwa gumu au rahisi kulingana na welewa wa mtu au mafungamano yake
japo ukweli unabaki pale pale kuwa BMK inakutana kinyume cha sheria na utashi
wa watanzania wanaoona kama linatumiwa na kundi la watu wachache kutaka
kuwaibia fedha wanazolipana au kuwapandikizia katiba,.
Je
kwanini CCM haisikii sauti ya watu wake yaani wananchi? Ajabu! Je CCM ni ya
watu au watu wachache? CCM si chama cha
wananchi. Hivyo, hakina haja ya kuwajali wananchi bali wenye fedha wachache
wanaokitumia kifisadi na kigaidi kuwaburuza na kuwaibia watanzania. Watani wake husema kuwa CCM ina wenyewe na
wenyewe ndiyo wenye nchi ambao ni wala nchi wanaowatumia wananchi. Wananchi ni
kundi lenye maana kisiasa mbele ya macho ya CCM. Wananchi hao hawana nguvu wala
lolote mbele ya wenye nchi ambao hujifanyia watakavyo baada ya kuwalaghai
wananchi wakawapa madaraka wanayotumia dhidi yao kikatili na bila kujali.
Je
bado kuna BMK au Bunge Maalum la Katiba kama kinavyoendelea kule Dodoma dhidi
ya utashi wa umma kinavyopachikwa jina zuri? Bunge Maalum la Katiba lilikufa siku
UKAWA walipotoka nje. Hakika, bunge lilikufa siku rasimu halisi ya Warioba
ilipowekwa kando na nafasi yake kuchukuliwa na mizengwe, ghilba na nyaraka za
kutengenezwa na kundi moja ili kulinda maslahi yake binafsi dhidi ya maslahi ya
taifa.
Kimsingi, BMK ilikufa siku rais Jakaya Kikwete
mwenyekiti wa CCM alipovaa unazi na ukada akiweka wazi utaifa akamvizia,
kumzushia Warioba kwa kutangaza nini wajumbe wajadili badala ya rasimu. Hakika,
hii ni siku ya msiba kwa taifa ambayo hata kama ni kwa ubaya na mapigo yake,
itakumbukwa na vizazi vijavyo kiasi chakuuliza utimamu wa akili za wahusika
kama jamii na taifa kwa kufumbia macho uhuni na jinai hii ambayo inaweka taifa
na vizazi vijavyo msambweni,
Hakika, hakuna ubishi, BMK ni marehemu sawa na
rasimu ya wananchi iliyowasilishwa na Warioba na Tume yake. Ajabu, walioua BMK
wanajulikana kuwa ni CCM Kikwete na Samuel Sitta ila wahanga na wenye nchi
wanasita ima kwa woga au ujinga kuwachukulia hatua stahiki. Kwa ukatili na
jeuri vya hali ya juu, walijifanya hamnazo wakalikatili taifa kwa kuendekeza
maslahi binafsi kuanzia madhambi yaliyopita, yaliyopo na tamaa ya madaraka. Ni
kipofu, bazazi na kichaa pekee ambaye angeua BMK kwa vile lililenga kuwa
mkombozi wa taifa. Sitaki niamini kuwa wauaji wa BMK hawakujua wala kuliona
hili. Huenda hawajachelewa wanaweza kuliona na kulifanyia kazi kabla historia
haijawahukumu vibaya.
Je
haya mazingaombwe yanayoendelea yakaitwa BMK ni nini? Unaweza kuyapa jina
lolote kuanzia Bonge la Mazingaombwe na Kuula. Kimsingi, kinachoitwa mjadala wa
kupata katiba mpya si chochote wala lolote bali gea ya kuula au tuseme Bonge la
Mizengwe na Kuula. Kinachoitwa BMK ni Bonge ya Mshiko Kirahisi kwa waramba
viatu wa chama tawala ambacho kimefumba macho na masikio kuhakikisha
kinalihujumu taifa ili kiweze kuendelea kuwa madarakani kinyume cha sheria. Je
huu ni ukatili na kuisha na kuishiwa kiasi gani? La kufa halisikii dawa hata
hivyo.
Je
ni kwanini umma unaendelea kufanya makosa tena makubwa? CCM iliwahi kusema kuwa
haiwezi kuondoka madarakani kwa vipande vya karatasi yaani kura kabla ya kuja
na sayansi ya uchakachuaji na wizi wa kura. Baada ya kugundua kuwa kuandikwa
kwa katiba mpya kunaweza kuwa silaha kali na hatari kuliko karatasi, imeamua
kuuia hata kabla ya kuzaliwa ili iendelee kuishi na kuula kama kawaida yake.
Hapa ndipo wanufaika wa ulaji huu wanapoamua kufanya lolote liwe halali au
haramu ili kuhakikisha ulaji wao hata kama ni wa haramu kirafi na kifisi
unaendelea bila kuguswa. Kugusa hasa kupinga kulaani na kutaka kukomesha ulaji
wa genge hili la wachache hutafsiriwa kama kupinga mawazo ya wengi na kuwawekea
maneno vinywani.
Nani
anaweza kuwawekea vinywani umma kama huyu anayeua BMK akaanzisha kituko
akakiita BMK? Jibu la swali hili linapaswa kutolewa na umma ambao ni wahanga wa
jinai hii ya zaidi ya miaka hamsini ambapo umechezewa mahepe na kila mlaji awe
mwenye kufuata kanuni au vinginevyo. Tunaamini umma umefahamu siri ya CCM
kutosikia sauti na vilivyo vyake na badala yake ikaamua kuiua BMK na Rasimu ya
Jaji Warioba. Wanaweza kuua nyenzo hizi mbili adhimu japo kwa muda tu. Je
watafanikiwa kuua ukweli kuwa watanzania wanahitaji utashi na mawazo yao ya
kuandikwa na wao wenyewe kwa namna watakayo?
Chanzo:Dira Sept., 8, 2014.
No comments:
Post a Comment