Akiongea
kwenye ibada ya pasaka, rais John Pombe Magufuli aliwataka watanzania kuchapa
kazi ili Tanzania iweze kuondokana na uombaomba na utegemezi wa makombo ya
misaada toka ughaibuni. Na kweli, siku chache baada ya rais Magufuli kuyasema haya Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia
(MCC) ilitangaza kusitisha msaada wa dola za kimarekeni milioni 700 tokana na
kutoridhishwa na uchakachuaji uliotokea Visiwani kwenye uchaguzi uliobatilishwa
mwishoni mwa mwaka jana bila sababu. Hata hivyo, ni bahati mbaya kuwa taifa
letu–ukiondoa serikali ya awamu ya kwanza–limekuwa ikitawaliwa na viongozi
wenye mawazo tegemezi na mafisadi kiasi cha kutegemea kuombaomba bila hata
kuona aibu. Wazo la kujitegemea ni la kimapinduzi kama litafanyiwa kazi na pia
kujitegemea huku kutalenga kutenda haki na si kufanya madudu kama ya Visiwani.
Inatia aibu kuona kiongozi wa nchi kwenda kwa viongozi wenzake wa nchi nyingine kujidhalilisha kana
kwamba hana ubongo na anaongoza watu wasio na ubongo wala mikono. Ni aibu hasa
kiongozi anayefanya hivyo anapokwenda kule akidai anaongoza taifa huru lakini
lisiloweza kujitegemea hata baada ya kuwa huru kwa miongo zaidi ya mitano. Taifa
ombaomba si huru. Taifa tegemezi si huru. Kwani wanaolifadhili ndiyo
wanaoliwatawala kwa mlango wa nyuma kama ilivyo kwa mataifa mengi ya kiafrika
ambayo yamekalia raslimali lukuki lakini watawala wake wakazivuja na kwenda
kuomba bila hata chembe ya aibu. Tunampongeza na kumshajihisha Magufuli
alifanyie kazi hili kwa vitendo na haraka sana ili taifa letu liweze angalau
kuwa huru.
Haiwezekani
nchi iliyojaliwa raslimali kama vile ardhi nzuri yenye rutuba na madini kila
aina, bahari, mito maziwa, mbuga za wanyama wa aina mbali mbali na watu
kuendelea kuishi kwa kujidhalilisha ikiombaomba. Kuendelea kuomba –hata kama
hili laweza kuonekana kuwa tusi –ni ushahidi kuwa ima tuna matatizo ya kiakili,
na kama siyo sisi bali wale wanaotutawala wawe ni wafadhili au wafadhiliwa. Ili kuweza kujitegemea, tunahitaji kufanya
yafuatayo:
Mosi,
tuwe na uongozi na usimamizi bora wa raslimali zetu. Hapa lazima tupambane na
maadui kama vile ukwepaji kodi, uvivu, misamaha ya kodi, uwekezaji wa kijinga
na kifisadi na pia matumizi mabaya ya raslimali zetu.
Pili,
lazima tujenge utamaduni wa uwajibikaji unaoandamana na uchapakazi wa kweli na
si kwa viongozi tu bali watanzania wote kwa ujumla wao. Mfano, watanzania
wanapaswa kujua kuwa wana mchango mkubwa katika ubomoaji wa taifa letu. Kadhalika,
wana mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa letu. Wapo wenzetu wanaowasaidia
wageni kuibia taifa letu kwa kupewa vijisenti kidogo wakati wageni hawa wezi
wakiondoka na mabilioni ya shilingi. Rejea utoroshaji wa wanyama, madini na
raslimali nyingine. Hawa wanapaswa kukamatwa na kunyongwa ili kuwa onyo kwa
wote wanaodhani Tanzania ni shamba la bibi.
Tatu,
lazima kuwepo na mfumo unaosimamia na kutekeleza nidhamu ya matumizi ya mapato
na fedha ya umma tena wenye uwazi na ukweli.
Nne,
lazima tuwe na mfumo wa sheria zenye kusimamia uwekezaji ambao utasaidia
kupambana na kuwashughulikia wale watakaokwenda kinyume na dhana nzima ya
uwajibikaji na matumizi bora ya mali za umma. Mfano, sheria itamke wazi wazi
kuwa atakayeshindwa kuelezea namna alivyochuma mali zake, atafikishwa
mahakamani na mali husika zitatwaliwa na serikali. Pia sheria hii itasaidia
kurejea mikataba ya kijambazi na kipumbavu tawala zilizopita zilizoingia kwa
sababu ya maslahi ya watu wapumbavu, vipofu na waroho wachache. Ni bahati mbaya
kuwa tangu aingie madarakani na kuanza mapambano dhidi ya ufisadi, rais
Magufuli hajagusia namna atakavyofumua mikataba hii ambayo imegeuka mashimo
makubwa ya kuzamisha fedha za taifa. Wengi wangependa kusikia mikakati yake juu
ya kupambana na kadhia hii ambayo watangulizi wake waliogopa kutokana na
kufaidika nayo.
Tano,
bila kuwa Katiba mpya yenye kuanisha wajibu na haki za watanzania, tutakuwa
tunatwanaga maji kwenye kinu. Mfano, unapokuwa na rais ambaye yuko juu ya
sheria, ataweza kuitumia nafasi hii kujitajirisha na kufanya atakavyo kwa vile
hakuna anachochelea. Tawala zilizopita zimetupa somo kuwa rais anapokuwa juu ya
sheria inakuwa rahisi kwa waliomzunguka kuyatumia madaraka yake vibaya kuwaibia
wananchi huku wakijitajirisha na wananchi wakiendelea kuwa maskini bila sababu.
Uzoefu wa kashfa kama Kiwira na EPA unapaswa utupe somo kubwa juu ya namna
madaraka ya rais yanavyoweza kufujwa na wahalifu waliofanya hivyo wakaepa mkono
wa sheria kutokana na rais kuwa juu ya sheria. Hata hii kadhia ya ukwepaji
kodi, ufisadi na misamaha ya kodi imechangiwa kikubwa na hali ya rais kuwa juu
ya sheria.
Sita, ili kufanikisha yote hapo juu,
lazima–kama taifa na jamii ya watu wanaojua wanachofanya–turejeshe maadili ya
utumishi wa umma na ikiwezekana kwa watanzania wote kama ilivyokuwa wakati wa
awamu ya kwanza. Kila mtanzania ajaze ripoti ya mwaka ya mapato na matumizi
yake, kutangaza mali zake na kutoa maelezo ya namna alivyozichuma ili kubaini
kama ni kwa kufuata sheria au kifisadi.
Tumalizie
kwa kumsisitizia rais na serikali yake wajenge mfumo wa kitaasisi
utakaoliwezesha taifa kujiondoa kwenye aibu na kadhia ya uombaomba usio na
ulazima. Watanzania lazima tujisute na kuonea aibu kadhia ya kuishi kwa makombo
kama mbwa.
Chanzo: Mwanahalisi.
No comments:
Post a Comment