Magufulification: Concept That Will Define Africa's Future and the Man Who Makes Things Happen

Magufulification: Concept That Will Define Africa's Future and the Man Who Makes Things Happen

Sunday, 3 April 2016

Tunaipongeza serikali kubomoa jengo hatarishi

            Hakuna ubishi kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya rais John Pombe Magufuli imeanza kuleta mapinduzi tena ndani ya muda mfupi kama haitalewa mafanikio na kulegeza Kamba. Tukio la hivi karibuni ambapo jengo sugu na hatarishi lililokuwa mtihani ulioishinda awamu iliyopita ni la kupigiwa mfano na kupongezwa.
            Kwa kuvunja jengo hatarishi la Uhindini–tunadhani bila shaka–serikali imetoa onyo kwa wale wote waliokuwa wanadhani kuwa hawagusiki kwa vile wana uwezo na fedha ya kuwahonga watendaji wabovu serikalini kuhalalisha jinai yao. Wengi wanaokumbuka malalamiko ya wananchi juu ya hatari ya majengo mabovu hatarishi kama hili wanajua jinsi serikali iliyopita ilivyowapuuzia na kuacha maisha ya mikononi mwa Mungu. Hata hivyo, ujio wa rais Magufuli unaonekana kuleta pumzi mpya kwa wanyonge waliokuwa wakikwazwa na vitu kama hivi.
            Inabidi tuseme kuwa kuipongeza serikali isiwe sababu ya kubweteka na kuona sasa kazi imekwisha. Kimsingi, kazi ndiyo inaanza. Kwani yapo majengo mengi yaliyojengwa chini ya viwango ambayo hayajagunduliwa na kushughulikiwa. Na kama si jengo lililoporoshwa kuchongewa na jengo jingine pacha kuanguka na kuua watu zaidi ya 30 huenda jengo hili hatarishi lingekuwa limeishamalizika na kupangishwa kwa watu wasio na hatia wakingoja majaaliwa ya Mwenyezi Mungu. Hii maana yake ni kwamba kuna majengo mengi ambayo yanapaswa kukaguliwa na kushughulikiwa yatakapogundulika kujengwa kwenye mtindo ule ule wa kuwahonga watendaji wabovu serikali na kuhalalisha mauaji ya halaiki kwa watu wasio na hatia.  Hivyo basi, tunategemea kasi na ari ya kupambana na jinai hii inayofanya miji yetu iwe makaburi yanayongojewa kujifukia na kuua wengi wasio na hatia iendelee. Tunategemea yatafuatia majengo mengine yaliyojengwa kwa mtindo wa chapchap ili kutengeneza fedha chafu chapchap bila kujali usalama wa wananchi. Je tunavyo vitega uchumi hatarishi kama hivi vingapi nchini kuanzia majumba ya short time ya kueneza ukimwi, zahanati na hospitali visivyokidhi viwango nchini?
            Je tunayo majengo mangapi kwenye fukwe zetu na mabonde na vyanzo vya maji nchini? Kwa kumbukumbu ni kwamba kuna hoteli na mahekalu ya watu binafsi vilivyojengwa kwenye fukwe zetu na maeneo oevu kama vile hekalu la Getrude Rwakatare ambalo limesitishwa uvunjaji wake tokana na mhusika kukimbilia mahakamani. Kuna haja ya kubadili sheria zetu ili kuondoa mianya wahalifu wanaojenga sehemu zisizoruhusiwa kuzitumia kutukwamisha. Hivyo, tunategemea–baada ya kuangusha jengo hatarishi la Uhindini–majengo ya kwenye fukwe na sehemu nyingine zisizoruhusiwa yafuatie haraka huku ukaguzi wa mejengo yote nchini ukifuatilia ili kuondoa kadhia hii ambayo licha ya kuhatarisha usalama wa watu wetu ni kikwazo kiuchumi.
            Pia tuchukue fursa hii kuiasa serikali isifanye upendeleo katika kupambana na kadhia hii. Kwa mfano, kila mtanzania anajua kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinamilki majengo mengi ya umma kinyume cha sheria. Hili nalo linapaswa kushughulikiwa ili haki itendeke kwa wanyonge wa taifa hili wajisikie kuwa sasa nchi ni mali yao na si mali ya wezi wachache wenye madaraka na fedha kama ilivyokuwa. Nani asiyejua kuwa viwanja vingi ambavyo CCM inatumia kukodisha kwa kuegeshea magari vimepatikana kinyume cha sheria kwa vile CCM ni chama tawala. Hatuwezi kuendelea na uoza huu halafu tukajiridhisha na kujisifu kuwa tunatenda haki kwa watu wetu kwa usawa.
            Pia serikali ihakikishe kuwa watanzania wanakuwa na makazi na miji salama. Maana, unapokuwa na majengo hatarishi kama hili lililobomolewa, yanakatisha tamaa uwekezaji kwa shaka ya kupata hasara baadaye. Pia majengo kama haya yanaweza kuathiri uchumi hasa sekta ya bima ukiachia mbali mabenki ambayo yanaweza kutoa mikopo kwa wenye majengo kama haya wakiweka majengo mabovu kama dhamana na kuingiza mabenki hasara  kutokana na majengo haya kutokuwa na thamani sawa na ile wamilki wanayodai yanayo.
            Hapa tunaongelea sababu za kiuchumi. Kuna upande mwingine ambao ni kusababisha vifo na uharibifu wa mali ukiachia mbali kuwa matokeo ya jinai ya kughushi na kudanganya kuhusiana na thamani na viwango vya majengo husika.
            Tumalizie kwa kuipongeza serikali na kuitaka ifanye kila liwezekanalo ili kuepuka madhara majengo hatarishi yanaweza kusababisha kwa watu wasio na hatia hata uchumi wa nchi.
Chanzo: Tanzania Daima,  Aprili 3, 2016.

No comments: