Inanikumbusha ile amri ya dingi mwenyewe ya kupiga marufuku vijiwe vya walevi huku akibariki vya waishiwa, wachunaji wajiitao wachungaji, mashehena wajiitao mashehe ukiachia mbali vile vya akina Anna Kimlango Malisera waliovurunda kule Shy wakaambiwa: watapangiwa ulaji mwingine. Unapoteua mijitu iliyobwagwa kwenye kura za maoni unategemea nini?
Kwa kumbukumbu ni kwamba hata huyu dogo anayetaka kuwatimua ombaomba amewahi kukiri: alikuwa akienda canteen kuomba chakula kilichokuwa kiende kwa wenye mbwa. Ama kweli mkuki kwa nguruwe. Anayebishia au kufikiri nazua abonyeze https://www.youtube.com/watch?v=0FmCByYhV0c&nohtml5=False
Kama aliongea kuwafurahisha watazamaji, ajue huu ndiyo ushahidi na imekula kwake.
Sina haja ya kutetea ombaomba. Kwanza, hawana uchache wa kunilipa. Pili, wanachofanya ni aibu sawa na kaya yao. Nadhani ili kupata kile waCameron huita moral authority, kaya ilipaswa, kwanza, iache kuombaomba ndipo ipate udhu wa kuwafukuza ombaomba wenzake. Ombaomba wana akili, nguvu na mikono kama nyenzo za uchumi; ila wanavikalia sawa na kaya inavyokalia uchumi huku ikishikilia kuombaomba. Kwa walevi, ombaomba wa mitaani ni nafuu kuliko wa maofisini wanaoomba kitu kikubwa na kidogo. Sidhani kama ombaomba wa mitaani ni wabaya sawa na wale wanaokwenda Ulaya kuomba halafu njuluku ikaishia Uswisi, Panama, Jersey na kwingineko. Au mnawaonea kwa vile hawakupiga buku? Nani amewafanya ombaomba kama siyo wakubwa wa hovyo walioacha kaya igeuzwe shamba la bibi huku wao wakitanua kila uchao kwenda nje kufanya kazi hiyo hiyo?
Sidhani kama ombaomba wetu ni hatari kama wamachinga wa kigeni waliofurika miji yetu wakiuza ubuyu wakati wachovu wetu wanaweza kufanya kazi hii au wale wanaosamehe kodi, kuruhusu makontena kupita bandarini bila kulipa ushuri, kuingiza mafuta kayani kwa miaka mitano bila kuwa na mita; au wanene walioruhusu kaya yetu ifilisiwe wakati wao wakicheka cheka; au wale waliojimilkisha Kiwira, UDA au kushiriki ujambazi kama EPA, Escrow na uchafu mwingine. Pamoja na ulevi na mibangi yangu, sijui kama ombaomba hawa wana hatari sawa na majambazi walioingiza mikampuni jini kama IPTL. Sijui na sijajua kusema ule ukweli. Kamata hao kwanza wafuatie ombaomba.
Tuache utani. Hata tukimpiga darubini huyu dogo mkubwa wa mkoa, ukubwa wake haukutokana na kingine zaidi ya kuomba ateuliwa na Njaa Kaya hasa baada ya kumdhalilisha mzee Jose Waryuba. Mbali na hayo, badala ya kuangalia ni kwanini wachovu wanakimbia vijijini na kuja mijini, mnadhani kuwafukuza ni jibu? Pelekeni maendeleo na maisha bora kule. Hamtawaona mijini. Tokana na elimu yangu ya uchumi niliopata wakati nikisomea PhD yangu kwenye Environment, Resource, Development and Economy (ERDE) ni kwamba wachovu wengi wanakimbia vijijini kutokana na kutokuwapo maendeleo. Watafanya nini iwapo wanasikia mijizi kama Singasinga, Jimmy Rugemalayer, Rosti Tamu la Aziz, Ni Ziro Kadamage, Has Kitiliya, Say Kisenena na wengine wanapiga dili na kuibuka mabilionea bila kutoa jasho? Mnadhani hawasikii wala kujua kinachoendelea kwenye majiji kama Bongo ambako gendaeka wanauza mibwimbwi na kulala maskini na kuamka mabilionea na hakuna anayehoji walivyozichanga? Nani aende shamba wakati hata marahis wastaafu hukomaa jijini? Do you think they’re stupid son? Think twice. Sijui kama ombaomba wa mitaani ni wabaya sawa na majambazi ya bunduki na kalamu. Sijui kama ombaomba hawa maskini ni wabaya sawa na viongozi wa kiroho wanaowachuna na kuwaibia maskini wakitangaza ujinga kama kutenda miujiza wakati miujiza yenyewe ni kuwatapeli wachovu na kuwa matajiri wa kutupwa. Brother mchunaji Rwakatarehe, Gamanyua, Lusekelelo, Mwasengesenge, Ka-tortoise, Jose Gwaijimani na matapeli wengine wa kiroho mnanideku hapa?
Sasa ngoja nitoe ushauri wa kitaalamu. Kwanza, nashauri wakubwa wasihubiri maji wakanywa mvinyo kama yule jamaa wa kwenye kitabu fulani aitwaye Po kama huyu bwana mdogo aliyesema fuateni niwambiayo lakini siyo nitendayo. Hawa hakika wanakikumbusha mama ntilie fulani ambaye alikuwa akiagiza mlo wake wa mchana wakati akiuza msosi kutokana na kujua kilichokuwapo nyuma ya pazia.
Pili, kaya iache kuomba. Ikusanye ushuru, ilinde mali za umma, ikamate mafwisadi wote na kuwanyonga, ijitegemee ndipo ipate udhu wa kuwafukuza ombaomba. Jogoo aliyewafundisha vifaranga kunya ndani. Kwanini lisirikali linaloomba linataka kuzuia wachovu wake kuomba wakati lina kila raslimali tofauti na wao? Ukiishi kwa upanga utakufa kwa upanga. Ukiishi kwa kuomba na wachovu wako wataomba kama wewe hata kama hawana sura wala hawaongei kimombo katika kufanya hivyo. Sijui hapa ni ombaomba yupi anataka kumfukuza yupi wakati wote ni wamoja?
Ngoja nijikate kisilesi nikingoja kiumane!
Chanzo: Nipashe, Aprili, 16, 2016.
No comments:
Post a Comment