How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 26 April 2016

Kijiwe chadurusu daraja la Kigamboni


















Baada ya rahis Joni Kanywaji Wine Makufuli kufungua daraja jipya la Kigamboni alilopendekeza liitwe mzee Mchonga, Kijiwe kilikaa na kudurusu baadhi ya mambo kuhusiana na daraja hili adhimu na la kwanza la aina yake “Duniani.”
Mgosi Machungi anaingia akiwa amevaa picha ya daraja la Kigamboni kifuani. Anaamkua na kuchonga, “Wae waiokuwa wakisema kwao ni kama Ulaya sasa wajiandae kuja si kushangaa fei tu bai hata daaja jipya la Kigamboni aka mzee Nchonga.”
Mpemba anadakia, “Hayawi hayawi sasa huwa; ngalau sasa kaya yetu yaweza kuwa kama Ulaya yakhe. Nataka sasa lijengwe jingine kutoka hapa Bongo hadi Pemba wallahi ili tuachane na kuzama baharini na kuliwa na samaki.”
Kapende hakubaliani na mawazo ya wenzake. Anakwanyua mic, “Kipya kinyemi japo kidonda muangalie. Tokana na kaya yetu kuwa ya kifisadi na roho mbaya, sina cha kufurahia. Maana, sina uhakika kama daraja husika limekidhi viwango vya usalama vya kimataifa,” anapiga chafya na kuendelea, Je mradi walingana na thamani ya mabilioni yaliyounguzwa pale au wajanja weshapata chao?”
Kabla ya kujibiwa, Mipawa anakula mic, “Nami nina shaka kweli kweli. Hata hivyo, nashangaa hii tabia ya kutaka kugeuza kitu kuwa mtu.Kwanini liitwe Nyerere na si mashujaa wengine kama vile mzee Mpayukaji, Mkwawa au Milambo kama si Nyungu ya Mawe hata Eddie Sokoine?”
Kutaja tu jina langu naangua kicheko ila sisemi chochote. Nikiwa natabasamu kwa kuitwa shujaa hata kama wa kijiweni, Mbwamwitu anadaka mic, “Nyang’au sasa watatukoma. Humkusikia rais Joni Kanywaji akiwatupia kimondo kuwa wote waliozoea kusema kila kitu kiko kwao sasa wanaisoma namba na kuchukua tahadhari? Ngoja Flyovers za kumwaga uone Bongo itakavyopiku majiji yote ukanda huu.”
Mipawa anamchomekea Mbwamwitu, “Hapo kaka umeua.  Sijui kama hawa jamaa wapenda sifa na dezo ukiachia mbali majivuno wataanza kusema kuwa na daraja la Mchonga liko kwao. Usishangae kusikia likiitwa Kinyata badala ya Mchonga. Walipojenga flyover na barabara kubwa miaka iliyopita walijivuna sana wasijue nasi tulikuwa nyikani tukisuka mipango namna ya kujiondoa na kadhia ya kuonekana kichwa cha mwendawazimu ingawa hatujatoka huko bado.”
Mijjinga aliyekuwa akimtext mshikaji wake anaamua kutia guu, “Kama wasemaji walioonyesha shaka, nami nina mashaka na maswali kadhaa kuhusiana na daraja hili na Maflyover pendekezwa. Je yanadumu na ni salama? Nikiangalia mijengo iliyojengwa kigabachori na kifisadi, sina imani na mradi huu. Nitakachofanya ni kupunguza safari za kwenda Kigamboni ili kuepuka maafa.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kuingia fosi, “Kaka wala huna haja ya kuacha kwenda Kigamboni kwa kuogopa kuliwa na samaki. Mbona kaya zima ni bomu! Angalia utitiri wa vituo vya kuuzia mafuta jijini na kwenye miji mingine. Unadhani hata hapa tuko salama? siku vitakapolipuka–kama utanusurika–utayakumbuka maneno haya. Si hilo tu. Hii mijengo iliyorundikana kama uyoga nayo mtaiweka upande gani?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kutia timu, “Kama waliosimamia kazi ya ujenzi wa daraja hili walikuwa wakweli, hakuna haja ya kuogopa ingawa hili nalo laweza kuwa gumu hasa ikizingatiwa kuwa hii ni kaya inayotawaliwa na Chukua Chako Mapema bila kuwajali wenzako hata wewe mwenyewe baadaye. Kuna haya ya sirikali kufanya uchunguzi wa mradi mzima ili kujiridhisha kuwa hakuna ufisadi uliofanyika hapa ili tuweze kuwa na imani na mradi uliogharimu mabilioni ya fedha yetu ya kodi.”
Kanji anamchomekea Sofi, “Da Sofi iko kuna mimi veve hapa. Kama sirikali nafanya chunguzi takuwa juri sana. Kama taacha vatu iliwe na samak basi laumu yeye.”
“Nakuna veve vapi Kanji acha uhuni,” anachomekea Mchunguliaji aliyekuwa akisoma gazeti.
Mheshimiwa Bwege anaamua kutia buti, “Kanji mbona unafikiri kama jana! Unadhani watawala wetu wanaogopa lawama? Ukiwalaumu sana sana watakuchukia kama jamaa waliokosoa utumbuaji majipu wa bwana nkubwa wakaishia kutishiwa na kuitwa majipu. Mie naungana na wale wanatakaoamua kupunguza safari za Kigamboni basi.” Anampa kikombe muuuza kahawa amtilie kahawa na kuendelea, “ Hivi mliona yule nyampala wa mkoa alivyowachoma wenzake wakaishia kusimamishwa ulaji? Ama kweli nyampala ameonyesha kujitahidi ingawa sikubaliani na ukurupukaji unaosikiliza upande mmoja. Rahis hakupaswa kuamua pale pale kana kwamba ajira za wanene ni mnada. Alipaswa kuwaita wahusika na kuwapa nafasi ya kujitetea ili wasitumie kisingizio hicho mbele ya pilato.”
Msomi anarejea, “Usemacho ni kweli. Japo rahis ana nia nzuri tu, anapaswa kufuata sheria ili kuwa na utawala bora na wa sheria. Pia asichukie wala kuogopa kukosolewa. Itakuwa zahama kama atapenda kusikiliza vibwagizo vya wanyampala wake wanaofanya usanii na kutetea kitumbua chao. Lazima akubali kuwa hawezi kujua yote wala kuwa sahihi wakati wote. Isitoshe hii kaya ni yetu sote naye yuko pale kututumia na si kutuburuza au vipi?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si lakipita shumbwengu la Willy Kabwea, wacha tulitoe mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: