Akiwa mjini Chato mkoani Geita hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli alizungumzia mambo mbali mbali yahusuyo mstakabali wa taifa. Moja kati ya mengi aliloongelea –au tuseme kugusia –ni namna baadhi ya watanzania waroho na wabinafsi wanavyoishi maisha mazuri kuliko hata malaika wakati wengi wa watanzania wakiishi kwa mateso.
Magufuli alisema, “Kuna watu wanaishi maisha mazuri kuliko hata Malaika,” wakati watanzania wengi wakisoteshwa na kuteseka kwa umaskini. Ni roho mbaya kiasi gani? Hata fisi–pamoja na kuwa hayawani na kiumbe mroho sana–hawezi kuwafanyia hivyo wenzake. Ajabu watu wa namna hii wanaitwa wasomi na wanaamini kuwa wanachofanya–licha ya kuwa haki–ni wajibu wao kwa taifa. Watu wa namna hii si wa kuficha majina yao wala kufumiliwa. Nadhani wakati wa kulalamika umekwisha. Kilichobaki ni kuwashughulikia bila huruma wala ajizi. Hivi ndivyo Tanzania inaweza kuondokana na kugeuzwa shamba la bibi na wahalifu wachache wasioona mbali. Kuendelea kuwa na wezi wa namna hii ni tishio kwa amani na usalama wa taifa huko tuendako.
Pamoja na taarifa za ufujaji na wizi huu kuchukiza, kukatisha tamaa na kuchefuam, cha kufurahisisha ni ukweli kuwa rais Magufuli aliahidi kuwa atahakikisha watu wachache wanaojinufaisha kwa fedha ya umma kwa kujipangia na kujilipa marupurupu, maslahi na mishahara mikubwa–aliyosema inapitishwa na bodi za mashirika za kifisadi–wanapunguziwa mishahara yao toka milioni 40 hadi 15. Wengi wangetaka aanze hata leo na si baadaye. Kama hili litafanyiwa kazi vilivyo, basi ni ni hatua nzuri ya kutenda haki, kuwawezesha wanyonge na kuziba pengo baina ya wenye nazo na wasio nazo linalozidi kuongezeka kiasi cha kutishia usalama wa nchi. Katika kuelezea namna nchi ilivyokuwa imegeuzwa “shamba la bibi” Magufuli alisema, “Wapo waliofikia hata kufanyia mikutano ya bodi nje ya nchi.” Hakuna namna ya kuelezea kadhia hii. Huu si ufisadi wala jinai tu bali dhambi isiyohitaji msamaha. Hata kama ni ni jinai, basi huu ni ufisadi, uroho, roho mbaya, ulafi na ufujaji wa fedha za umma na ni jinai ya aina yake yenye kuweza kutendwa na binadamu. Hivyo, tunamuomba Magufuli awashughulikie wote waliobainika kwenda ughaibuni kufanya mikutano ya bodi.
Katika kushughulikia wezi na wafujaji hawa wa fedha za umma, Magufuli anapaswa kufanya yafutatayo:
Mosi, uchunguzi wa kina ufanywe na majina ya wahusika yatangazwe hadharani na kiasi gani cha fedha walifuja, nchi gani walikokwenda na kwa muda gani waliokaa kule. Hii licha ya akubaini wahusika, unaweza kugundua madudu mengine kama vile watu kwenda kufanyia ufuska nje kwa kisingizio cha mikutano ya bodi.
Pili, wahusika walazimishwe kurejesha fedha zote walizofuja katika matanuzi yao haya huku wakilazimishwa waeleze mantiki ya kufanya hivyo hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu ni maskini inayoishi kwa kuombaomba.
Tatu, wafunguliwe kesi mahakamani ili kuwa somo kwa wengine. Kama sheria za sasa hazina meno, basi zirekebishwe kwanza ili kutoa adhabu kali ndipo watuhumiwa washitakiwe ili wakipatikana na hatia wapewe adhabu kali isiyohusisha faini.
Nne, wafukuzwe kazi; na uanzishwe utaratibu wa kuhakikisha watu wenye ajira nyingine hawateuliwi kwenye bodi za mashirika ya umma. Hii itasaidia kuepusha keki ya taifa kufaidiwa na waroho wachache wakati taifa lina wengi wasio na ajira hasa vijana waliosoma kwa fedha ya mikopo ambayo inakuwa vigumu kuirejesha bila kuwa na ajira wala kipato. Tungependekeza itungwe sheria ya kumtaka kila mtanzania awe na chanzo kimoja cha mapato; na kama ni ajira asiwe na ajira zaidi ya moja ili kutoa fursa kwa jeshi kubwa la watu wasio kuwa na kazi ambalo taifa linakabiliana nalo. Nadhani hii itaondoa ufisadi wa kilafi wa namna hii.
Tano, bodi zote za mashirika yote ya umma zifanyiwe ukaguzi wa mahesabu na kubaini wengine ambao hawajabainika ikiwezekana kuanzia wakati mashirika yalipoundwa ili kubaini ni fedha za umma kiasi gani zimeibwa na nani wanahusika wawe hai, wameishastaafu au kufa lazima watajwe ili umma uwajue na kupendekeza hatua za kuchukuliwa dhidi ya warithi wao au walio hai kulipa wenyewe.
Sita, mali za watuhumiwa zikamatwe na kurejeshwa serikali hasa zile zinazoonyesha kuzidi toka kwenye malipo halali waliyopaswa kulipwa.
Saba, iundwe taasisi maalumu ya kuchunguza na kuratibu shughuli za bodi za mashirika ya umma.
Nane, irejeshwe sheria ya maadili ya utumishi wa umma itakayowataka wajumbe wa bodi kuwa wanaripoti mali zao kila mwaka ili kubaini wizi wa mali ya umma.
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli asiishie kulalamikia kadhia hii. Achukue hatua tena mara moja ya kuwatumbua wahusika au hata “kukata miguu” kama alivyosema pale jipu linapokuwa kubwa au limeishautafua mwili.
Chanzo: Tanzania, April 10, 2016.
No comments:
Post a Comment