Magufulification: Concept That Will Define Africa's Future and the Man Who Makes Things Happen

Magufulification: Concept That Will Define Africa's Future and the Man Who Makes Things Happen

Saturday, 30 April 2016

Mlevi kutaja walioficha njuluku nje


            Baada ya kufichuliwa ukwepaji mkubwa wa njulu kule Panama, nafanya mipango kwenda kule kuibua wafichaji wa Kibongo ambao wameponea chupuchupu kutotajwa japo wengi wengine bado wamo kwenye documents ambazo hazijashughulikiwa. Kwa sasa nawasiliana wanasheria wenzangu tuliokutana kwenye chuo kikuu cha Yaleyale Jürgen Mossack na Ramón Fonseca wa Mossack Fonseca company kutaka wamwage mtama mwingine hasa wenye majina ya wabongo. Mnadhani utani? Hawa jamaa ni washirika zangu wa siku nyingi; na lazima tuwatumbue watu hapa. Tunataka tupate majina ya majambawazi ya kibongo na kumpa Dk Kanywaji Makufuli tuone kama atafanya kile kilichowashinda watangulizi wake ambao nao tuna wasi wasi wana njuluku ughaibuni hata kama si Panama.
             Najua sasa vibaka wetu wanene wanajisifu kuwa wao ni safi kwa vile majina yao hayamo kwenye orodha hii wasijue kuwa mambo bado ukiachia mbali kuwa bado ya Cayman Bahamas, Dubai, Switzerland, Hong Kong, Mautius Island of Man na kwingineko hayajamwagwa hadharani ili waumbuke vizuri. Nawashauri wangoje kwanza. Kwani, mpango wangu ukifanikiwa, wengi watabaki bila nguo. Na hii ni kweli wala sitishii.
            Hata yule Jaji gabacholi wa Kenya Kalinipa Rawalu Absii Kalu alitajwa na waziri mmoja wa Ka-Game hawakutajaria wangetajwa tena kavukavu bila kuficha wala kufunika majina yao mwingine aliyetajwa bila kutegemea ni ni Riz wa Ghana na Congo na sister yake Kabila ambaye alikuwa mwanafunzi wangu pale Kinondoni seco kabla sijarejea vyuoni kunyaka shahada kama sina akili nzuri baada ya wabongo kunitilia mtima nyongo. Mwingine aliyevuliwa nguo huku mjomba wake akiwa tayari uchi si mwingine bali anko Bonge Khubuluse Xuma wa Sauzi anayesemekana kuwa na njuluku kama Bill Gate.
            Baada ya kupata inshu toka kwa washikaji zangu wa pale Panama City kwenye mtaa wa 54th East. Naona yule anatikisa kichwa asijue nimetia timu sana kwenye jiji hili la kisasa ambao umaridadi na utajiri wake umetokana na chumo la wizi ambalo mabwege wengi huibia kaya zao na kwenda kuficha kule.
            Baada ya kukamilisha kila kitu, nitamshauri Dk Kanywaji awasiliane na mamlaka za Uswisi mara moja ili kuleta ule mshiko ambaye Njaa Kaya alijifanya hamnazo na kuzuia uzirejeshwe kayani ili kusaidia mambo mengine kama vile elimu na afya. Kwa vile Olivier Chave ni mshikaji wangu ambaye tulikuwa tukinywa pamoja alipokuwa balozi hapo Dar, lazima atakuwa tayari kumpa tafu rais Kanywaji tena bila masharti wala kusitasita. Pia nitamshauri afufue makabrasha ya Daudi Balalii ili kujua kama kweli alidedi au anakula mikuku mitaa ya Washington kama siyo Hawaii. Kama alirejesha namba, washirika zake lazima wajulikane na kutumbuliwa tena haraka sana wakiwa uchi.
            Katika nusa nusa yangu nshapewa inshu kuwa wabongo walioficha njuluku Panama ambapo wako kwenye rada yangu ni pamoja na Njaa Kaya aliyekalia orodha ya majina aliyopewa.
            Mwingine anayepaswa kuchunguzwa vilivyo hata kufikishwa kwa pilato ni munene wa Takokuru ambaye alipewa inshu nyingi za ufisadi na ufichaji njuluku nje lakini akayatumia kujipatia nshiko kiasi cha kutokea kuwa bonge ya bilionea. Hata mjengo wake wa kule Beach siyo noma. Lazima naye afanyiwe kweli aeleze alivyochuma hiyo njuluku ya kuweza kuwa na mjengo wa kukata na shoka kama huu.
            Mwingine ambaye nilishapewa inshu yake ni jizi Kagoda ambaye ameficha mabilioni ya madafu Dubai na Panama na kwingineko ambako bado navuatilia.
Pia yume mzee wa Vijisenti ambaye naye alikatiwa sana njuluku kibao tokana na kuwawezesha wachukuaji waitwao wawekezaji kuingia mikataba ya kijambazi ambayo licha ya kufilisi kaya yetu, imesababisha kaya yetu kuonekana kama shamba la bibi aka kichwa cha mwendawazimu kwa kila jizi kujifunzia kuiba.
            Majizi ya Escrew nayo yanasemekana kuficha njuluku nyingi kule Panama, Singapore na kwingineko ambako bado nafuatilia kwa karibu ili baadaye niyavue nguo ingawa yako uchi tayari kiasi cha kufanya umma ushangae namna Dk Kanywaji anavyoyagwaya na kujifanya hajui chafu yake.
             Mwingine ninayepanga kumfuatilia ni Mzito Kabwela aliyeficha majina aliyowahi kudai alikuwa nayo lakini akagwaya kuyaweka wazi. Kuna mlevi amenitonya kuwa naye si safi. Kwani alitumia mwanya ule ima kujipatia umaarufu au kuwatoa njuluku watuhumiwa.  Ndiyo maana napendekeza rais Kanywaji ambane mbavu aeleze anachojua na kwanini alificha majina ya wezi wakati anajua jinsi wanavyoua walevi wengi kwa umaskini ukiachia mbali huduma mbovu za kijamii zilizohujumiwa kiasi cha kutisha.
            Loooh! Niliataka kusahau wengine ambao nitawashughulikia. Wote wanaoficha njuluku kwenye mijumba na migari ya bei mbaya hapa hapa downtown lazima nao nitawashukia bila kuwasahau wale viongozi wa kiroho wenye uroho wakwasi. Lazima waeleze walivyochuma huo ukwasi kama hakuna namna. Maficho ya njuluku si Panama wala Isle of Man au Jersey bali hata Masaki na kwingineko kwa wanene.
Pfyaaa, pfyaaa. Hii chafya nayo jipu!
Chanzo: Nipashe.

No comments: