How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 13 July 2016

Tunamsihi rais aongee lugha ya taifa


 
            Kwa watu wanaojua maana na sababu ya kuwa na rais kama kielelezo na mwakilishi wa nchi yeyote, watakubaliana nasi kuwa kila anachofanya lazima kiakisi taifa lake. Moja ya kitu kinachotengeneza taifa ni pamoja na kuwa na lugha yake ya taifa. Tanzania–tangu kupata uhuru–tuliamua, kama taifa, kufanya lugha ya Kiswahili iwe lugha ya taifa. Pia, tuliamua lugha ya mtawala wetu wa zamani Uingereza, yaani kiingereza kuwa lugha ya pili ya taifa ili kutuunganisha na mataifa mengine. Hivyo, Tanzania ina lugha rasmi mbili; Kiswahili na Kiingereza.
Baada ya rais John Pombe Magufuli kuingia madarakani, amejitahidi kuepuka kutumia lugha zetu mbili. Badala yake–kwa sababu anazojua mwenyewe–hutumia lugha isiyo rasmi almaaruf Kiswanglish yaani mchanganyiko wa Kiswahili na maneno machache ya Kiingereza.  Japo wapo waliokwisha kutoa shule juu ya umuhimu wa rais kutumia lugha kwa usahihi, huko hatutaenda. Tutakachozungumzia hapa ni umuhimu wa rais kutumia lugha moja ili kuweza kuwasiliana na watu wake. Mfano, rais anapochanganya Kiingereza na Kiswahili–licha ya wananchi hasa wa kada ya chini kielimu–anawachanganya hata wageni wanaotaka kujifunza Kiswahili. Mfano, hivi karibuni, rais alikaririwa akisema, “Ukitumia tuta hilo hilo, it even becomes more cheaper.”  Sijui kama mkulima wa Kahama au Geita anaambua kitu katika mkanganyo huu unaofanywa na kiongozi wao. Hata ukiandika neno more cheaper–kwa wanaotumia kikokotozi lazima kikuonye kuwa umechamsha. Neno sahihi ni cheaper than au much cheaper…..lakini si more cheaper. Mahali pengine ambapo rais anakosea mara kwa mara ni the East African Community ambayo yeye huiita East Africa Community ambayo kisheria haipo.  Nisingependa kuhariri hotuba yote ya rais aliyoitoa kwa muda mfupi ikajaa makosa mengi. Ninachotaka kuonyesha ni umuhumi wa rais wetu kuchagua lugha rasmi na sahihi ya kutuwakilisha kama taifa lenye utajiri wa lugha. Je rais hana washauri na wataalamu wanaopaswa kumwandikia hotuba kama hawezi au kumshauri kuandaa hotuba ya lugha moja kama anaweza? Najua kinachomsukuma Magufuli kupenda kutumia Kiswahili zaidi ni uzalendo. Hata hivyo, anapaswa akubali; Kiingereza ni lugha kubwa kuliko zote duniani kiasi cha kulazimisha mataifa kama China, Urusi na mengine ya Kiarabu kutumia mabilioni mengi kuwatuma watu wao kujifunza lugha hii ya kibiashara duniani. Hapa Kanada tuna lugha mbili za taifa, Kiingereza na Kifaransa. Hakuna anayeweza kuwa waziri mkuu wa Kanada bila kuzimudu lugha hizi barabara. Hata viongozi wa hapa wanapozitumia, huwa hawazichanganyi. Kwani, huchelea kuwachanganya wananchi wao. Hata pale anapochaguliwa mtu anayeona kuwa hawezi lugha moja au zote, hufanya bidii kuzimudu ili aweze kuwasiliana na wananchi wake barabara.
Wakati akimkaribisha rais wa Rwanda Paulo Kagame kufungua Maonyesho ya 40 ya Kimataifa ya Dar Es Salaam, rais Magufuli alichanganya lugha mbili kwa kupachika neno hapa na pale wakati mgeni wake aliamua kuzipanga kwa kuongea moja baada ya nyingine na siyo kuzichanganya ili kuwapa nafasi wakalimani wafanye kazi yao.
Kwa vile Kiswahili ni lugha taifa–tena inayokua kwa kasi–rais anapaswa ashauriwe umuhimu na ulazima wa kuongea Kiswahili safi bila kuchanganya Kiingereza au kama ataamua basi aongee Kiingereza pekee na Kiswahili pekee. Kama akichanganya basi asichanganye maneno bali kila lugha aipe fursa kwa usahihi wake kama alivyofanya Kagame. Nadhani, Magufuli atakuwa amejifunza hilo toka kwa Kagame ambaye amemsifia kwa kumpa kile alichoita madesa ambacho nacho si Kiswahili sanifu. Rais Magufuli–kama ataamua–anao uwezo na sababu za kuongea ima Kiswahili au Kiingereza safi na sanifu bila kulazimika kuchanganya. Tunaona hili kama tatizo kwa taifa lenye lugha inayojitegemea. Kwanza, rais anawafundisha nini vijana walioko mashuleni na watanzania kwa ujumla? Pili, anatoa picha gani kwa wageni kuhusiana na itifaki ya matumizi ya lugha kwa usahihi wake?
Tatu, kwa kiwango chake cha elimu, anapaswa kuzimudu lugha zote mbili bila kikwazo vinginevyo kuwe na namna. Haiwezekani mtu mwenye shahada ya uzamivu (PhD) asiweze lugha husika iwapo ametumia miaka zaidi ya 15 akitumia Kiingereza kama lugha ya kujifunzia asiweze Kiingereza. Najua rais Magufuli si mtaalamu wa lugha. Ni msomi wa kemia. Bado, kwa kipindi alichotumia Kiingereza kama lugha ya kitaaluma, lazima awe anakimanya vizuri tu. Itakuwaje watu wenye elimu ya chini kulinganisha na yake kama vile Kagame, Jakaya Kikwete na hata Amani Karume wakiweze yeye asiweze? Kama rais atahitaji kupigwa msasa kwenye kimombo asione aibu. Hakuna anayeweza kujua yote duniani. Heri akubali kutojua ili asaidiwe kuliko kuendelea kuruhusu utata uliopo kwa sasa kuhusiana na matumizi ya lugha ya rais Magufuli. Pia, ifahamike; kama walio karibu naye wanashindwa au kuogopa kumwambia ukweli, tutamwambia kama watanzania.
Tumalizie kwa kumshauri rais na washauri wake kuliangalia hili ili kuepuka kuwachanganya wananchi wetu hasa wa vijijini. Rais wetu lazima aeleweke kwa kada zote za wananchi wake na si wasomi au wajuzi wa Kiingereza tu kama ilivyo sasa anapochanganya lugha. Pia, ifahamike, tunatoa ushauri kwa nia ya kujenga na si kubomoa. “We should learn languages because language is the only thing worth knowing even poorly.” –Kató Lomb.
Chanzo: Mwanahalisi Jumatatu.
 
 

No comments: