Zoezi la ununuzi wa madawati nchini linatia moyo sana. Zoezi hili pia lina somo kuwa kumbe Afrika ikiamua inaweza kujitegemea na kuachana na uombaomba na kopa kopa. Kama alivyowahi kusema marehemu baba wa taifa, kweli uchumi tunao ila tumeukalia.
Jambo jingine linalojitokeza kwenye zoezi la kujitosheleza kwa madawati ni ukweli kuwa tulichokuwa tunakosa ni muamko na vipaumbele. Nadhani, baada ya kumaliza zoezi la madawati, tuhamie kwenye vitanda kwenye hospitali na zahanati zetu. Kama tutaendelea kubana na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, tunao uwezo wa kujitosheleza kwa kila kitu kama taifa kiasi cha kuwa mfano bora kwa nchi nyingine ambazo hazijachukua hatua kama tulizokwisha kuchukua.
Leo tutaongelea mambo machache ambayo taifa letu limeonyesha kuwa waafrika wana kila sababu ya kujikomboa na kuondokana na udhalilishwaji kimataifa na kitaifa.
Mosi, angalia jinsi fedha nyingi za umma zilivyookolewa baada ya kuopiga marufuku safari za nje ambazo nyingi zilikuwa ni kwenda kufanya shopping na kujilipa per diem kwa wezi wachache wenye madaraka.
Eneo jingine ni utenguaji wa uteuzi wenye kutia shaka. Hili litasaidia kila mteuliwa kujua kuwa yuko kwenye ofisi ya umma kuwatumikia wananchi na si kuwatumia au kuzitumia ofisi kama kijiko cha kuchotea utajiri. Ukiachia safari za nje, kuna hili la kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi. Si haba, hatua hii inatoa tahadhari kuwa sasa mafisadi wajiandae. Tusiridhike na kubweteka na mahakama. Tubadili mifumo na sheria zetu ili kupambana na jinai hii inayotishia mshikamano na mustakabali wa taifa. Sasa mahakama tunayo. Twende mbele na kuwakamata mafisadi bila kuangalia sura wala mafungamano kama ilivyo sasa.
Ukiachia kulega lega kwenye mapambano dhidi ya ufisadi–ambayo, kimsingi, yanamtegemea rais peke yake–kuna eneo jingine ambapo tumepiga hatua ambayo ni kupunguza ukubwa wa serikali. Hatua hii licha ya kuokoa fedha nyingi na kusambaza ajira kwa watu wengine badala ya kung’ang’aniwa na watu wachache imeleta damu mpya kwenye nafasi za juu. Hakuna kitu kimesaidia kupunguza matumizi ya fedha za umma kwenye ajira zisizo na ulazima kama kuwa na baraza kubwa la mawaziri. Sambamba na kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, tunaishauri serikali kuhakikisha haiongezi idadi ya mikoa au wilaya. Kama tungeangalia kwa makini, kuna baadhi ya mikoa iliyoanzishwa kisiasa zaidi ya uhitaji.
Pamoja na kufanya vizuri kwenye mambo yaliyotajwa hapo juu, kuna maanguko. Haya ni pamoja na:
Mosi, kuminya demokrasia kwa kuwazuia na kuwafungia wabunge wa upinzani kuhudhiria bunge jambo ambalo linawanyima fursa ya kufanya kazi waliyotumwa kufanya na wale wanaowawakilisha. Pia kuendelea na uhuni ambao umekuwa ukiendelea bungeni ni ushahidi kuwa licha ya kuvunja katiba na haki za binadamu, tunajenga dhana kuwa serikali inaogopa demokrasia hasa kukosolewa jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa kama chachu ya maendeleo. Isitoshe, nchi hii si mali ya chama fulani wala kundi fulani la watu eti kwa vile lilipata kura nyingi. Inashangaza kuona serikali inajiwekea rekodi mbaya kwa kuwapuuzia wananchi wapatao milioni sita na ushei ambao hawakuichagua. Hata wangekuwa wawili au mtu mmoja, bado wana haki ya kusikilizwa mawazo yao hata kama hayawafurahishi wala kupendwa na waliopo madarakani.
Sehemu nyingine tulipoanguka ni kutokuwa na ithibati na kutenda haki sawa katika vita ya ufisadi. Unashangaa kuona watumishi wanaotuhumiwa kusaidia wizi kwa mfano bandarini kufukuzwa kazi au kusimamishwa wakati watuhumiwa wa kashfa kubwa kama vile Lugumi, Escrow na nyingine wakiendelea kutanua. Je kunani nyuma ya pazia au nchi yetu imegawika kwenye matabaka ya sacred and black cows?
Sehemu nyingine tulipoanguka sana ni ile rais kuonekana kama yuko juu ya katiba akiamua nani afanyiwe au asifanyiwe nini hasa kuhusiana na tuhuma za ufisadi na matumizi ya fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka na uzembe. Rejea, kwa mfano, rais kutoa hakikisho kwa watangulizi wake hivi karibuni baada ya baadhi ya watanzania–ambao kimsingi, ndiyo wahanga wa kadhia zilizotajwa hapo juu–kutaka baadhi ya wakubwa wafikishwe mahakamani kwa kadhia tajwa. Hii inajenga dhana kuwa kuna watu wasioguswa hata wakabiliwe na jinai kiasi gani. Hii si sawa na si vizuri kwa taifa linalotaka kujirekebisha tokana na makosa ya nyuma huku likitoa onyo kwa wajao.
Sehemu nyingine ni ile hali ya serikali ya sasa kushindwa kuwakamata watuhumiwa wakubwa wa biashara haramu ya mihadarati. Japo ni mapema kuilamu serikali, kwa namna ilivyokaa kimya bila kuonyesha makucha yake dhidi ya kazia hii, uharibifu unazidi kutendeka kwa taifa na watu wetu.
Tumalizie kwa kuitaka serikali irekebishe kasoro zilizotajwa huku ikiongeza mkazo kwenye maeneo ilikofanikiwa. Kwani, bado watanzania wanakabiliwa na changamoto ambazo nyingi zake zinasababishwa na ukosefu wa nia thabiti, vipaumbele na ushirikiano katika kupambana nazo. Pia tunashauri kuwa baada ya kukamilisha madawati mashuleni twende kwenye taasisi nyingine kama mahospitali, zahanati, vituo vya kulelea watoto yatima na wazee na nyinginezo ambazo zina hali mbaya bila kusahau kuongeza nguvu katika kupambana na jinai ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili.
No comments:
Post a Comment