Kwanza nikiri kuwa pendekezo la kuwanyonga wezi na wahalifu wakubwa wanaohujumu nchi yetu si la kuvuita. Laweza kuhusu wengi hasa wale wanaotetea haki za baadhi ya binadamu huku wakifumbia macho haki za wengine hasa wahanga wa maovu nchini. Hata hivyo, nitalitoa na kulijengea hoja ili wasomaji na wahusika wapambue na kuamua wenyewe. Nchi ya China inasifika sana duniani kwa sasa kuliko hata Marekani kutokana na mambo makubwa inayofanya kwa kipindi kifupi tangu ibadili mfumo wake toka ukomunisti kwenda kwenye ubepari mchanganyiko. China kwa sasa ni taifa linalotetemesha magwiji kama Marekani hata Umoja wa Ulaya kutokana namna inavyoendelea hasa kiuchumi.
Moja ya mambo yaliyowezesha China kufikia hapa ilipo ni ile hali ya kutokuwa na simile na uovu hasa ufisadi, uuzaji mihadarati na jinai nyingine.
Tanzania kama China, tulikuwa wajamaa muda si mrefu uliopita. Baada ya kuachana na ujamaa na kuingia kwenye ubepari uchwara, hata hivyo, Tanzania hatukusonga mbele zaidi ya kurudi nyuma. Rejea uhaba na ubovu wa huduma za jamii tulizokuwa tukipata wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya kwanza ya kijamaa ambayo sawa na China, ilipiga vita ufisadi kweli kweli. Mpaka tunavyoandika, China haisikilizi kelele za haki za binadamu ambazo mara nyingi zimekuwa zikilenga kuwatetea wahalifu huku wakifumbia masikio haki hizo hizo za wahanga wa wahalifu husika. Kama China ingekuwa Tanzania, kashfa kama EPA, Escrow, Lugumi, Kagoda, Meremeta, Mwananchi Gold, UDA na hii iliyoibuka ya mtu kutengeneza mamilioni kwa dakika zisingekuwa zinasuasua au kushughulikiwa kisiasa.
Tofauti na China, Tanzania ilibariki ufisadi kiasi cha kuonekana kama umehalalishwa kwa mlango wa nyuma. Hivi karibuni vyombo vya habari vilifichua kuwa rais John Pombe Magufuli amemtumbua mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akiliibia taifa shilingi milioni saba hadi nane kwa dakika. Hata Bill Gates tajiri mkubwa kuliko wote duniani hatengenezi fedha kiasi hiki na kwa njia hii haramu. Je mtuhumiwa kama huyu ameishasababishia taifa hasara gani? Je mchezo wake huu mchafu umeishasababisha vifo vya watu wangapi wasio na hatia kwa kukosa huduma kama vile madawa ukiacha mbali usumbufu wa kukosa huduma kama vile elimu, na hutuma nyingine za huduma tokana na serikali kutokuwa na uwezo kifedha? Je ni kosa kwa mtu kama huyu–akipatikana na hatia kuhukumiwa kifo–baada ya kufilisiwa? Hiki ndicho wenzetu wa China wanachofanya.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu ambaye–hata hivyo jina lake limefichwa sijui ni kwanini–kunafanya tuulize: je ni wangapi wameishacheza mchezo huu na serikali imeishapoteza kiasi gani? Mbona majambazi wengine wa kawaida wanapokamatwa au kuuawa majina yao hayafichwi? Je kuficha huku kuna nini nyuma yake au ni mtu ambaye wakubwa wasingependa ajulikane kutokana na utukufu wake na wao. Je mtuhumiwa amefanya mchezo huu kwa muda gani na kusababisha hasara ya fedha kiasi gani? Haya ni baadhi ya mambo tunayopaswa kuchunguza na kujua ili kuwashughulikia wengine kama yeye. Je washirika zake nao wamekamatwa? Maswali ni mengi kuliko majibu. Nadhani, kukamatwa kwa mtuhumiwa huu kunatoa hitimisho kuwa kweli Tanzania si nchi maskini wa fedha wala mali bali maskini wa viongozi wenye maono na uzalendo kushughulikia jinai kama hii.
Wenzetu wa China hawana ubaguzi katika kutekeleza sheria walizojiwekea. Tanzania ni tofauti. Mtu anaiba kuku na kufungwa miaka thelathini wakati mwenzie anaiba mabilioni na kuhukumia miaka michache na kusafisha sehemu za umma! Tusipobadili sheria na kutunga sheria kali na kuzitekeleza dhidi ya maovu kama haya, tutaendelea kupiga siasa na kuwa shamba la bibi kama si kichwa cha mwendawazimu. Tukiendelea kuwaendekeza wakubwa waliosisi hujuma na maovu kama haya, tutaendelea kujidanganya tu.
Japo tunaweza kumlaumu mtuhumiwa–jambo ambalo ni haki–kuna haja ya kujiuliza: serikali ilikuwa wapi siku zote wakati hujuma hii kwa taifa ikifanyika? Je mtuhumiwa aliwezeshwa na mazingira au alijijengea mazingira ya kufanikisha wizi wake? Hapa ndipo unapopata utata kusikia baadhi ya wakubwa wakisema kuwa wanaotaka wakubwa wenzao washitakiwe kwa kuhujumu nchi ni mambo ya hovyo. Wakati mwingine unashindwa kuelewa hata maana ya hovyo. Je hapa wanaotaka wakubwa washitakiwe kweli wanasema mambo ya hovyo kweli au hawa wanaowakingia kifua watu wenye madhambi–ambayo wengine wamekuwa wakiyalalamikia–ndiyo wa hovyo hovyo na wanaofanya mambo ya hovyo? Inashangaza mambo ya hovyo yanapofanywa ya maana na ya maana kugeuzwa vya hovyo. Sidhani kama kutoa taarifa kuhusiana na maovu fulani ni jambo la hovyo au kutopokea taarifa hizo na kuzifanyia kazi ndilo suala la hovyo. Haiwezekani watu wakawa wanajiibia wakati serikali ipo na wale waliokuwa wakisimamia wizi huu au kuzembea na kuuruhusu bado wakawa watu wa kukingiwa kifua au kupewa kinga kisheria. Huku ni kujipinga, kujichanganya na kuwachanganya watanzania; nalo ni jipu linalopaswa kutumbuliwa ingawa linawahusu hao hao wanaopaswa kutumbua.
Tumalizie kwa kushauri kuwa–kama kweli serikali imedhamiria kupambana na uovu hasa ufisadi na uhujumu wa nchi–basi irejeshe maadili ya utumishi wa umma; na ifanye hivyo bila ubaguzi wala upendeleo. China wanaonekana kufanikiwa kutokana na kutokuwa na mambo ya hovyo kama vile kulindana, kuogopana au kufichiana majina.
Chanzo: Mwanahalisi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment