How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 28 July 2016

Kijiwe champongeza Dk Kanwyaji


          Baada ya Dokta Joni Kanywaji Makomeo kupewa rungu la pili ili atumie kutumbua majipu, Kijiwe kinampongeza na kumtega. Kwani, sasa wachovu wanategemea kuona akifanya vitu vyake bila ya woga wowote hasa ikizingatiwa kuwa ana marungu yote.
Mpemba anaingia akiwa amevalia kofia yake nzuri ya tarabushi na kuamkua na kusema, “Yakhe mlokuwa mkisema sana kuhusiana na rahis Dokta Joni Kanywaji Makomeo sasa jiandaeni kusuka au kunyolewa tena bila maji.”
Mheshimiwa Bwege anamchomekea, “Yakhe wamaanisha nini? Unadhani kuna mabadiliko hapa au yale yale ya CcM?”
Mpemba anajibu, “Unakuwa kama wewe si mtu wa pwani? Kwani mie namaanisha nini? Basi ngoja nrudie. Nasema, mlokuwa mkisema sana sasa ntihani kwenu. Ombeni Subhanna huyu jamaa afanye kweli. Lakini asipofanya kweli mtaumbuka kweli kweli kiasi cha kuonekana kama mwalimwa mwajiona.”
Mgosi Makamba anakula mic, “Sisi tinampongeza dokta Kanywaji; pia tinamuombea afanye  kwei ii asijeonekana kanyabwoya kama siyo sanaa na kamba. Maana, sisi tiiofuatiia nchakato nzima tinaona kama kuna namna hasa tikikumbuka  waiovyosifiana.”
Mipawa anakula mic, “Kumbe nawe umeiona namna alivyowasifia wale anaowatuhumu kuwauza wachovu tokana na uzembe wao? Hata mie hapa nashangaa kiasi cha kuanza kuona kama usanii mwingine.”
Kapende, “Ulitegemea nini? Kwani hujui kuwa kambare wote wana sharubu au unadhani watabadilika usawa huu? Nasema wazi wazi tena kwa kinywa kipana; wanaotegemea mabadiliko basi walie tu. Kama yapo ni yale ya kutumbua vidagaa na kulala kitanda kimoja na nyangumi. Jiulize ni kwanini kushitaki mafisadi imekuwa kama aina fulani ya picha.  Mie kusema ukweli sitegemei lolote jipya zaidi ya kuwekana sawa na kufungana kamba kama kawa. Dk Kanywaji akitaka kunishawishi awakamate waliogeuza kaya yetu shamba la chizi.”
“Kaka hapo umetoboa. Hata mie atanitosheleza kama atakamata mafisadi bila kubagua. Nashangaa madudu kama Escrow, EPA, kuficha njuluku ughaibuni hayaguswi. Huoni hata mafisadi wa sukari wamemalizana naye; na sasa wanapeta? Unacheza na Danganyika nini?” anasema da Sofia Lion aka Kanungaembe.
Mbwamwitu ansema, “Da Sofi acha nikuchomekee. Unasema atakutosheleza kama atafanya nini?”
Sofia anajibu, “Wewe unaonaje kama swali hili angeulizwa mama yako? Wenzako wako seriously wewe unaleta utani hapa!  Acheni kucheza makidamakida kama Lyatongolwa Mlemavu aliyekwenda Idodomya kujikomba na kujivua nguo kwa sababu ya tonge la ugali.”
Mijjinga anatia guu, “Usinikumbushe huyu meku ambaye anaonekana hakuumbwa na aibu hata chembe hasa anapobanwa na njaa. Yote tisa, sikujua kuwa kumbe kile kizee cha kigosi bado kipo. Kijamaa kwa kamba. Eti kiliingia na gea ya uhubiri wakati nacho ni yale yale kutafuta ulaji wa dezo. Hakuna kiliponiudhi kama kuwasifia Njaa Kaya na Denjaman wakati waliuza kaya yetu.”
Mzee Maneno anakwanyua mic, “Unashangaa hiki kizee cha mikamba siyo! Ulitegemea kiseme nini wakati huu ambapo mtandao wao wa wizi uko hatarini chini ya Dokta Kanywaji? Pamoja na uhovyo wake, kilinifurahisha kilipomtolea uvivu mchunaji Jose Gwaijumaa aliyejitiatia kumkana Eddy Ewassa akidhani atawaingiza mkenge magamba asijue nao ni kama yeye ni wapigaji na wasanii wazoefu.”
Msomi aliyekuwa akibukua jarida moja la kimataifa akionyesha wazi kutokuwa na hamu na mjadala anaamua kuchomekea, “Hivi kamandoo wa Zenj yuko wapi;maana sikumtia machoni.”
Mpemba anajibu, “Unaulizia shuka matangani. Alikuwa kamandoo zama zile akiua wapemba. Baada ya Nyazi Mungu kuntia laana untegemeani?”
Kanji naye anachomekea, “Veve Somi iko fanya juri sana dugu yangu. Hata mimi iko wazi iko wapi ile kamandoo natingisa sana zama ile.”
Msomi anaamua kuigia jumla, “Nimesikiliza pwenti zenu nyote. Wapo wanaotegemea kuwa Dokta Kanywaji atatumia marungu yake kuwaponga kila nyani wanao na waliohujumu kaya. Mwenzenu nachelea kuamini hivyo hasa nikizingatia kuwa jamaa ni mwanasiasa. Pili, kwa alivyowamwagia ujiko wahujumu viongozi wa kaya hii, sitegemei lolote wala muujiza. Nashangaa amekuwa akilalamika kuwa kaya yetu ililiwa jambo ambalo ni kweli. Je ililiwa chini ya nani kama si hao anaowasifia kwa kumuumba na kumfundisha mengi? Nadhani–kwanza sitaki nionekana nawanga–tutarajie kipindi cha kushangaza ambapo mambo yatakuwa yakienda kutegemea anayeshughulikiwa ni nani. Sitaki kujipa matumaini yasiyokuwepo hasa nikijua namna wanasiasa wetu walivyo. Nadhani lao laweza kuwa moja hasa usawa huu ambapo siasa ni sehemu ya kutengenezea utajiri wa haraka hata kama ni mchafu.”
Anapiga chafya na kuendelea, “Japo namuaminia Dokta Kanywaji, napata shaka japo bado nakuwa na matumaini kuwa mara nyingine siasa za majukwaani huwa ni za kupakana mafuta kwa mgogo wa chupa; hivyo, lolote lawezekana.”
Mgosi Machungi anadandia, “Hapa timekueewa. Nikikumbua aivyomifukuza Ombeeni Sifuwi, naweza kusema loote laweza kutokea kwa Dokta Kanywaji. Hivyo, timpe moyo asiangalie nyani au tumbii usoni atakapoanza kutumia maungu haya aiyopewa juzi.”
Mchunguliaji naye anaamua kuzoza. “Hapo kaka nimekupata tena vizuri sana.”
Kabla ya kuendelea Mgosi anaamua kutaka kumkwida.
Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita manzi chuma kweli kiasi cha kutufanya wote tumkatie shingo!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano.

No comments: