Mwishoni mwa mwaka jana, rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, kwa mamlala aliyo nayo
kisheria, alifanya kilichowastua wengi kwa kutoa msamaha kwa wafungwa katika
kuadhimisha kumbukukumbu ya uhuru wa Tanganyika. Katika msamaha huu wa rais,
ulihusisha hata wale waliokuwa hawatarajii acha kutarajiwa kuachiwa kama vile
wale waliokuwa wamepatikana na hatia ya kubaka, ambayo kisheria, hawakupaswa
kusamehewe. Hili lilizua malalamiko toka kwa watetezi wa haki za binadamu hasa
baada ya wasamehewa kuonekana wakijivinjari kwenye viwanja vya ikulu. Wanaopinga
hili walisema kuwa linawapa ujasiri waliotenda makosa ya ubakaji.
Hata hivyo, si lengo la makala hii kujadili uhalali au mamlaka ya kufanya
hivyo. Niseme wazi kuwa rais alitumia mamlaka yake kuwaachia alioona wanafaa
kuachiwa baada ya kujiridhisha, kupitia vyombo vyake kuwa havunji sheria, hasa
katiba aliyoapa kuilinda, kuhifadhi na kuitetea kama mkuu wa nchi. Pia, si nia ya safu hii kuhoji kama rais
alizingatia maslahi mapana ya wahanga wa baadhi ya jinai ambazo zikitendeka na
mtuhumiwa akakutwa na hatia hapaswi, kisheria, kupewa msamaha kama ubakaji.
Kwanini nagusia hili? Ni kuepusha kuonekana kama rais amefanya makosa kutokana
kufanya ambacho kisheria hakiruhusiwa wala kukubalika hasa tukizingatia sheria
kama sheria na heshima na haki za waathirika wa baadhi ya makosa. Wapo ambao
wameishaanza kutumia kuachiwa kama mtaji wakizunguka huku na huku wakivutia
vyombo vya habari kuwahoji. Wapo wanaodai kuwa wanafanya waliyofanya kama
ishara ya kumuunga mkono na kumshukuru rais. Rais keshawaachia inatosha. Hana
haja ya kuendelea kusikia mambo yenu. Heri mkae kimya na kumshukuru Mungu na
rais kimya kimya badala ya kutafuta usupastaa unaoweza kuwaponza baadaye.
Makala ya leo inajikita kwenye
kadhia mbili, yaani wasamehewa kutaka kutumia fursa hii ama kutafuta umaarufu
wakisahau kuwa msamaha hauondoi kosa la jinai walilopatikana nalo na ile ya
wasamehewa kurudia kutenda makosa ya jinai kiasi cha kuonyesha kuwa msamaha wa
rais ni kama dhihaka au una makosa kwa kuachia watu ambao hawakupaswa. Hivyo,
ushauri wa kwanza, ni hawa wahusika kujua kuwa kusamehewa na rais, siyo fursa
ya kutafutia umaarufu au kurejea kwenye maisha ya jinai bali kujrekebisha na
kuomba Mungu wasiburuzwe tena mahakamani. Pia wahusika wajue kuwa msamaha wa rais ni
jambo ambalo ni sawa na bahati nasibu. Katika nchi inayofuata sheria vilivyo na
kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa misamaha kwa wahusika, kusamehewa na
rais tena kwa makosa yasiyosameheka, saa nyingine ni jambo ambalo linaweza
kuitwa muujiza hasa ikizingatiwa kuwa kufanya hivyo, kunaweza kuleta madhara kwa
mamlaka au kuifanya iangalie upya uamuzi wake na kuziba mwanya wa makosa kama
yalitokea ima katika kuchunguza tabia za wahusika na mazingira ya kuhukumiwa au
sheria.
Hakuna kilichoshangaza safu hii kama
kuona baadhi ya wahusika ambao si raia wa Tanzania, kuonyesha kaubabe fulani
ambapo kwa nchi za wenzetu siku walipoachiwa wangefukuzwa nchini. Ni ajabu kuwa
Tanzania haikufanya hivyo kwa sababu ambazo mamlaka inajua yenyewe. Kitu
kingine kilichonisukumba kudurusu wazo hili ni ile hali ya wasamehewa kutokana
kosa walilofungwa nalo. Tumeona wengine wakisema hadi kutoa machozi kuwa ima
walionewa au kubambikizwa kesi tofauti na hawa wanaosaka umaarufu kwa sababu tu
wameachiwa na rais.
Wahusika wanapaswa kujua kuwa rais
aliwasamehe si kwa mamlaka tu bali tokana na huruma yake. Hata kitendo cha
baadhi kukaribishwa ikulu kilizua utata hasa kwa waathirika wa kadhia waliyoshitakiwa
nayo wasamehewa na kupatikana na hatia na kufungwa maisha. Sijui wazazi wa
watoto na watoto waliofanyiwa vitendo hivyo, huko waliko, wanajisikiaje? Je
hawa wasamehewa wangetaka nini kifanyike kama vitendo walivyokutwa navyo hatia
vingetendwa kwa wapendwa wao, watoto, dada, shangazi au ndugu zao? Japo naweza
kuonyesha kama nawabagua wahusika, kwa vitendo walivyopatikana navyo hatia na
kufungwa, wajue kuwa Tanzania ni taifa lenye huruma. Maana kwenye nchi nyingine
ikiwamo yao, ukishafungwa imetoka.
Kusema ukweli, kuna kipindi Tanzania tunakuwa wakarimu sana kiasi cha
kutia shaka kama kweli tunajua thamani ya utaifa wetu.
Mbali na wanaosaka umaarufu na
kushindwa kuomba msamaha au kuonyesha kuwa wamejutia makosa yao, wapo
wanaotumia fursa ya kusamahewa kama kuitukana mamlaka iliyowapa upendeleo huu.
Kwani, tayari wengi wameisharejeshwa kule wakiwa wametenda makosa ya jinai
kuiachia mbali baadhi kuwa mikononi mwa vyombo vya dola wakisubilia kufikishwa
mbele ya vyombo vya sheria baada ya kupatiakana na ima silaha au kujihusisha
kwa njia moja au nyingine na jinai.
Tumalizie kwa kuwataka wasamehewa
kuwa na fadhila. Watende mambo mema. Wale walioachiwa kama nilivyioanza kwa
makosa yasiyosameheka, wasijione ni wajanja au wasitumie msamaha wa rais
kutafutia umaarufu na kuonyesha ubabe. Kwani, wale waliowakosea, licha ya kuwa
watu, wana makovu ya mateso yao. Kwa wale ambao si raia wa Tanzania, wazidi
kumshukuru Mungu. Kwani ingekuwa nchi
nyingine, jambo kama hili lisingefanyika tena bila serikali za kwao kuiomba
serikali lau kufikiria kuchukua uamuzi kama huu wa ajabu. Pia, tumshukuru rais
kwa kuwa na huruma muhimu afuate sheria na taratibu ili kuondoa malalamiko.
Chanzo: Tanzania Daima, Jan., 24, 2018.
No comments:
Post a Comment