Baada ya Kijiwe kungojea bomba letu la bomba dear toka Ukanadani bila majibu, kiliamua
kunituma mimi kama Mkiti wake kwenda kudodosa kujua kunani lau kiweze kusaidia
kaya kulipata. Ndiyo maana kwa miezi minne hivi, hapakuwa na kitu ugani. Nilikwenda
kutafuta nondo. Nilianzia pale alipolianzishia totoTudu Lissu kuwa bomba letu
jipya la Bomba Dear lilikuwa limenyakwa kule Ukanada, wanoko walimuita mmbea
wengine msaliti na mambo mengine tu ya hovyo na matokeo yake akaishia
kumimiminiwa shaba kibao. Hao wameshindwa na watanyong’onyea kabla ya
kupukutika mmoja mmoja.
Sasa siku zinazidi kuyoyoma wala bomba letu kipenzi hatulioni. Je kunani;
mbona mabingwa wa kuzoza na kuzodoa hawasikiki? Zifuatazo ni adidu za rejea
nilizofanyia kazi. Je ni kweli kuwa kuna washenzi na matapeli wa kimataifa
walioingia kayani wakijifanya wanatafuta kazi kumbe kupiga njuluku zetu
waliotufanyia kitu mbaya? Kama ni kweli, inakuwaje wale wanene walioendekeza
upigaji huu tunaendelea kuwapa shavu badala ya kuwazomea hata kuwaonyesha
lupango? Tunawaengaenga kwa lipi wakati walituingiza kwenye matatizo tokana na
upogo na ubinafsi wao? Hamkusikia munene akisema wakati wa kuzindua taarifa
kuhusu mawe akilalalimika kuwa kaya ilikuwa imegeuzwa shamba la bibi kwa
wapigaji kuja kujipigia kama vile haina mwenyewe? Kaya ilikuwa ikiliwa mbele na
nyuma tokana na kuongozwa na machangu kimaadili . Unapowapa unene vilaza, hata
hivyo, unategemea nini?
Kwa vile majibu hayatoki; na inavyoonekana, hakuna mwenye ubavu wa kuyatoa,
kijiwe kiliamua kunilipia visa, nauli na malazi kwenda zangu Ukanadani kujua
kunani? Hii ni kutokana na uzalendo–na si usaliti–wa kijiwe. Hivyo, msishangae
kusoma mikakati hii hasa ikizingatiwa kuwa siku zilizopita niliipa kaya mbinu ya
kuepuka wapigaji wa kimataifa wanaotumia mahakama zao za kijambazi kukwamisha
maendeleo ya kaya kapuku hasa baada ya munene kusema kuwa hatakuwa tayari
kujidhalilisha kama waliomtangulia kukesha kiguu na njia akienda ughaibuni
kubomu kana kwamba yeye ni taahira. Haiwezekani kaya inayokalia utajiri wa
kutisha iendelee kubomubomu kama vile haina raslimali. Huwezi kuongoza kaya
vizuri wakati unapoteza muda kuzurura na kutanua bila sababu. Kama ingekuwa
amri yangu, wajalaana kama hawa ningewatia kitanzi lau liwe somo kwa wengine
wanaodhani kaya hii ni shamba la chizi.
Najua kaya yetu ilikosa raslimali moja kubwa inayoitwa kwa kisambaa smart
upstairs baada ya kung’atuka mzee Mchonga. Ni pale ilipopata wavivu wa
kufikiri, malimbukeni na wazuraraji kama viranja wake wakaishia kujisifia
kuzurura na kubomu ukiachia mbali kuiingiza kaya kwenye mikataba ya kipumbavu
na kijambazi inayoihangaisha kaya. Kama si upuuzi wao, bomba letu kipenzi wala
lisingekuwa gumzo hadi tunaitana majina mabaya ukiachia mbali kuonana wabaya
bila sababu zaidi ya upumbavu wa wajalaana hawa.
Kwa vile Mpayukaji si mgeni Ukandani, nilikwenda kukutana na washikaji zangu wa
zamani ambao ima niliwafundisha au kusoma nao ili tuone namna ya kuinasua kaya
na mkwamo huu. Niliwahi kutoa msaada na ushauri wa bure kuwa kaya
inapotaka kufanya mambo kama haya, inapaswa iwe inatuhusisha sisi wataalamu wa
mambo ili kuepusha hasara inayoweza kutokana na vitu kama hivi. Kitu kingine
nilichokwenda kufanya Ukanadani ni kuona kama kuna namna kaya yetu inaweza
kujitoa kwenye mahakama za kishenzi za kinyonyaji kama hizi ambazo zimekuwa
zikionea kaya za Kiswahili kwa sababu zilianzishwa na wakoloni waliotuibia bila
kuwafikisha kwa pilato wakalipia madhambi na uhalifu wao vizuri.
Kabla ya kuanza msafara huu mrefu kwenye kaya hii ya Ukanada inayosifika kwa
baridi, ukarimu na ukwasi wake, naomba wahusika wasiogope aibu kutokana na
nyodo walizoonyesha pale totoTundu aliposema Bomba Dear au Dear Bomba yetu
ilikuwa imenyakwa tokana na kudaiwa na waduwanzi na washenzi fulani matapeli
wanaotaka kutuingiza mkenge. Baada ya
kutia timu niligundua kuwa kweli bomba letu dear limenaswa. Maana,
unaposhughulikia tatizo kama hili lenye amri ya mahakama nyuma yake, lazima uwe
umejiandaa na zana zako zote. Huwezi ukavamia inshu kama hii kwa pupa
ukafanikiwa. Sana sana utalizwa kama inavyooanza kuonekana kwenye mazungumzo
yasiyo makini ya kimakinikia. Ndiyo maana, nashauri, siku zijazo, wanene wetu
wajitahidi kufanya mambo kwa kuyapima kabla ya kuingizwa mkenge tokana na
maamuzi na madili mengine ya kilevi levi ambayo kaya yetu ilizoea kuingizwa
ikiwa chini ya walevi wa madaraka na washamba wa mambo kiasi cha kupoteza muda
mwingi kwenye uzururaji bila sababu za msingi. Nampongeza sana dingi kwa
kukataa ujinga na ulimbukeni huu wa kujilisha pepo wakati walevi wakinyotolewa
roho na ukapa na ukata.
Kwa vile ninapaswa kufanya maandalizi ili kuepuka aibu ya kuingizwa mkenge kama
hawa wanaotaka kuingizwa mkenge, nilifanya utafiti wangu kisomi na kuona ukweli
ambao siku zijazo nitatoa namna ya kuufanyia kazi na kufanikiwa. Juzi nilipitia
zangu Brusels kum-breaf kumjulia hali na kumwombea dua totoTundu na kumpongeza
kwa kuweka mambo hadharani hata kama aliumizwa vibaya sana.
Kwa ufupi ni kwamba
bomba dear letu limenasa na sijui namna ya kulinasua.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano Jan., 24, 2018.
No comments:
Post a Comment