Baada ya
kuona waumini hata matapeli wakiendesha mikesha ya kuombea kaya, Kijiwe, kwa
vile kina wanachama ambao ni waumini wa kweli–na si wasaka ngawira na wachumia
tumbo–kimeamua kuendesha mkesha wa bara zima la Afrika kumuombea shujaa wa
ukweli aliye tayari kuufia ukweli kama Plato, Tunduni mwana wa Lissu
aliyeumizwa na majembuzi na wapinga maendeleo na uhuru wa kujieleza waliotaka
kumnyotoa roho.
Mgoshi Machungi
baada ya kurejea kutoka kwa king’ang’anizi Bob Mugabe anakwanyua mic baada ya
kuamkua. Anaronga “wagoshi nina ushongo
na kijiwe na mic hasa ikizingatiwa kuwa timekaa
miezi mitatu bia kukwanyua waa kubusu mic.” Anatugeukia na kutuangalia na
kuendelea ‘au shiyo wagoshi? Mwenzenu
nina uchungu sana. Hapa manaponiona nina mpango wa kwenda Uhoanzi kumjuia hai Tunduni mwana wa Issu aiyetaka kunyotoewa
roho na wajaaana wasiojuikana ambao mpaka sasa wameendeea kutojuikana wakati wanajuikana.”
Kabla ya
uendelea, Mijjinga anampoka mic na kudema “kaka usinikumbushe shujaa huyu
anayeendelea kusota kitandani. Hata hivyo, namshukuru Muumba kwani waliotaka
kumnyotoa roho wameshindwa na kuadhirika.
Kama uchache utaruhusu, tutakwea pipa pamoja kwenda kumpa kampani shujaa
huyu wa aina yake kaya nzima.”
Mgoshi hangoji aendelee kufaidi
mic. Anampoka mic na kuendelea “bashi
mwenzenu nina wazo kuwa tiitishe mkesha wa baa zima la Afiika ili timuombee
apone haaka arejee kuja kuendeleeza mapambano au siyo?”
Kapende ambaye alikuwa akimnong’oneza
jambo da Sofia Lion Kanugaembe anaamua kula mic. Anazoza “kwa vile kwenye kaya
yetu tunapendana na wote ni ndugu, hili si jambo baya. Hukuna mama makamu
alivyokwenda kumpa tafu kule Nairoberry kwa wakora juzi juzi kabla ya kukwea
pipa kuelekea Uholanzini? Huu ni mfano wa kuigwa.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anamnyang’anya
mic na kudema “hili la bibi wa makamu kwenda kumdeku mie sioni kama ni dili
iwapo baba mwenyewe na kipaza sauti wamekula pini ukiachia mbali kutohimiza
waliotaka kumsokoine kushindwa kupatikana kwa kisingizio cha kutojulikana. Hivi
kweli hawa wajalaana hawafahamiki? Au ni kuzinguana na sanaa ukiachia mbali
kuwa na mkono wa mtu?”
Msomi Mkata Tamaa anaamua kutia guu
na mapema “kaka paha umeibua hoja na maswali mazito na muhimu. Haiwezekani kaya
yenye ndata na ndutu na kila ghasia za usalama kushindwa kuwabaini na
kuwashughulikia hawa wajalaana kama hamna namna. Kama kaya haiwezi kuwabaini na
kuwachukulia hatua stahiki hawa wahalifu basi ni hatari kwa maisha ya wana kaya
wote na hakuna haja ya kuwa na lisilikali ambalo kwa kizaramo huitwa sitting
duck or do nothing powers that be.’
Kabla ya kuendelea mzee Maneno
anampoka mic na kuchonga “Msomi angalia hicho kikameruni. Hujui kuwa nasi tuna
lugha ya kaya ambayo mnene ameamua kuipigia chapuo kiasi cha kuanza kujulikana
na kuheshimika? Hivyo, kaka zoza Kiswahili au siyo Msomi?”
Msomi anatabasamu na kuendelea “kaka
usemayo ni kweli tupu. Hata hivyo, nisamehe. Kwani nilipitiwa. Hata hivyo, si
vibaya kujikumbusha madude na lugha niliyokuwa natumia wakati nikisomea PhD
zangu nyingi. Hayo tuyaache. Naunga mkono wazo la kumuombea Tunduni ila nina
sharti. Sitataka tuwahusishe wachunaji wanaojiita wachungaji na mashehena
wasije kutia laana dua yetu. Nitapendekeza tuombe sisi wenyewe na walevi wote
barani tena kwa kutumia Mulungu na si miungu ya kigeni na ya kikoloni.”
Mpemba hangoji amalize “yakhe mie
sikuelewi ati. Uniposema Mulungu
wamaanishani? Wadhani wote matwahuti wasio na dini wanaowezaomba kwa miungu ya
kishenzi siyo?” Kanji anaamua kula mic “mimi ungakono na guu Somi. Vote iko na dini yetu ya asili dugu yangu. Kama veve zarau dini yako basi vote
nacheka veve. Sisi takwenda omba Brahma asaidie hii Tundu ipone haraka
sana.”
Msomi anakatua mic tena ‘leo Kanji
umenifurahisha sana. Afadhali umesema wewe. Maana, waswahili wakati mwingine ni
viumbe wa ajabu. Wanadharau na kudhalilisha mila zao huku wakipwakia za wengine
hadi kufikia hata kutoana roho kama ilivyo kwa Tunduni ambaye ameumizwa kwa
kutetea wana kaya dhidi ya mambo ya ajabu ajabu. Unaweza kuzunguka jiji zima. Hutakuta nyumba
ya ibada ya Kiswahili bali za kiarabu, kizungu, kihindi, na juzi juzi nilisikia
za shetani kule Idodomya ambapo chizi mmoja alitaka kuanzisha. Tunajidanganya na
kudanganywa bila kujua kuwa huwezi kuheshimika kama hujiheshimu na kuheshimu
chako. Hili ni somo la siku nyingine hasa nikizingatia kuwa ni pana hasa
kutokana na kutamalaki kwa matapeliw anaodai watenda miujiza wakati ni wezi
watupu. Hawa–mnasisitiza–washirikishwe kwenye kumuombea Tunduni. Watamwombea nini
wakati wana madhambi zaidi ya shetani mwenyewe? Wataomba kwa Mulungu gani
wakati miungu yao ni fedha na utajiri?”
Sofi aliyekuwa akisikiliza kwa
makini anaamua kula mic “mwenzenu nikimkumbaka Tunduni huwa machozi yananitoka.
Sijui tunaelekea au kupelekwa wapi ambapo udugu tuliorithi umegeuka uhasama wa
kutoana roho? Tulizoea kupingana kwa hoja siyo ngumi na risasi wala kesi za
kubambikiziwa”
Kijiwe kikiwa kinanoga si mvua
ikaanza kunyesha! Acha tutimke mbio utadhani mvua inaua! Waswahili kwa kuogopa
mvua lakini wasiogope miwaya, sina hamu!
Chanzo: Tanzania Daima leo, Jan., 31, 2018.
No comments:
Post a Comment