Hivi karibuni, kwa mara nyingine,
rais John Pombe Magufuli alifanya kilichokuwa kimewashinda wengi tangu
kung’atuka baba wa taifa Mwl Julius Nyerere. Magufuli aliamua kuwaondolea uvivu
wachafuzi wa maadili ya kitanzania ambao, mara nyingi, ni matokeo ya utawala
mbovu, ujinga, ulimbukeni na tamaa miongoni mwa watanzania. Tunachukua fursa
hii kumpongeza kipekee kwa kuona zahma hii ambayo ilikuwa ikitishia uhai wa
taifa kimaadili.
Kama taifa, bila maadili, hatuna
tofauti na wanyama. Taifa lisilo na maadili, halina utambulisho wake na
linaelekea pabaya. Hivyo basi, rais Magufuli aungwe mkono na watanzania wote
kuhakikisha tunapambana na yeyote anayetaka kuchezea mila na utamaduni wetu kwa
gharama yoyote. Katika kufanya hivi, kuna mambo kadhaa ya kuzingatia.
Mosi, tusingoje serikali wala
kulinda mila na tamaduni zetu kwa hofu ya serikali wala kulamika. Maana, kwa
wenzetu, mila na tamaduni ni uchumi. Mfano mdogo ni toka taifa la Marekani
ambalo linatangaza na kuuza utamaduni wake dunia nzima kama njia mojawapo ya
kuzitawala nchi nyingine. Chukulia mavazi, mitindo, vinywaji na vyakula vya
kimarekani vinavyouzwa ulimwenguni kweli kupitia maabala yake ya Holywood na
biashara nyingine. Mwl Nyerere aliwahi kusema “utamaduni kuwa ni chombo cha
maendeleo.”
Pili, kama jamii, tuonyesha maadili
yetu kama njia ya kututambulisha na kututofautisha na watu wengine. Hivyo, tusichuuze
utu wetu kwa kisingizio cha kutengeneza fedha. Hakuna ubishi kuwa kwa sasa
filamu na miziki mingi vinavyozalishwa nchini ni vichafu tokana na kukinzana na
maadili ya kitanzania. Tumekuwa watumwa wa mila chafu toka mataifa mengine
yasiyo na mwelekeo hasa katika sanaa ya muziki ambapo ima tunaigiza Marekani au
DRC bila sababu zozote za msingi.
Tatu, kwa vile serikali yetu
imejitofautisha na serikali za hovyo zilizopita zilizoruhusu uoza kimaadili
kutokana na kuongozwa na watu ambao hawakuwa na maadili kwa kisingizio cha
usasa na kusaka fedha chafu. Tunapaswa tujionyeshe kama watanzania wenye
maadili ikiwa ni sehemu ya urathi wetu kama jamii ya watu wenye akili. Mambo ya
kucheza miziki au kupiga picha za uchi ni ya kishamba na kilimbukeni. Milegezo,
kutoga masikio na upuuzi mwingine lazima vipigwe vita kulhali. Maana vinawekwa
wazi wazi kana kwamba ni jambo la maana.
Nne, tunapopambana na kadhia ua
uchafuzi wa maadili tusiangalie sanaa tu. Twende mbali zaidi. Kwa mfano, katika
hatua hii, lazima tushughulikie vyombo vya habari vinavyoeneza uchafu kama vile
magazeti ya udaku. Kwani, nayo hayana
tofauti na watembea na waonyesha uchi wao ukiachia malimbukeni wa mila chafu za
kigeni. Magazeti ya udaku na radio na runinga za kidaku ndivyo vyombo vikuu vya
kueneza uchafu huu kwa kisingizio cha kutengeneza fedha. Ni bahati nzuri kuwa
Magufuli ameelewa na kufanya mambo ambayo wengi wa waliomtangulia ukiondoa
marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere yaliwashinda tokana na kutoona mbali
ukiachia mbali kuwa bize kwa mambo ya kipuuzi au kuyashiriki. Ukiangalia mema
mengi aliyotenda Magufuli unashangaa kugundua kuwa amepitia kwenye mfumo mchafu
kama huu. Hakika huu ni ushahidi kuwa Tanzania bado ina watu wema na wenye
kuthamini taifa lao.
Baada ya kupambana na vyombo
vinavyoeneza uchafu, twende mbali na kushughulikia watu has wale wanaoeneza
uongo na uchafu kama vile mahubiri ya uongo yanayowaaminisha watu kuwa wanatenda
miujiza au kutibu magonjwa yasiyotibika, kuleta bahati na upuuzi mwingine ambao
umesababisha taifa letu lichafuke tokana na matokeo ya mahubiri na utapeli huu
kama vile mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe kiasi cha kuliacha
taifa letu halina sifa kimataifa.
Kwa uzoefu wangu ni kwamba katika
Jumuia ya Afrika Mashariki, ni Tanzania pekee yenye vyombo vya habari vya
kidaku na vyenye kuvunja maadili ukiachia mbali utitiri wa waganga wa kienyeji
ambao wengi ni matapeli wa kawaida. Kama ambavyo rais Magufuli amekuwa
akishangaa na kujiuliza nani alituroga hadi tukageuzwa shamba la bibi. Kwani,
tuna watu tena matapeli wa kawaida ambao wametokea kuwa na utajiri wa kutisha
tokana na kuwaibia watu wetu ima kupitia dini za kitapeli, uuzaji na usambazaji
wa habari chafu ukiachia mbali waganga wa kienyeji. Huwa napendekeza taifa letu
kuanzisha sera ya zamani ya kuuliza watu binafsi wanaoibuka na utajiri usio
kuwa na maelezo ili kuondoa motisha kwa wengine wenye kutaka kuuibia umma
kitapeli. Nchi ilikuwa imefikia pabaya hadi machizi fulani kuanzisha madhehebu
ya dini yanayohimiza watu kutenda maovu kana kwamba hakuna serikali. Kwa vile
rais Magufuli ameamua kujitofautisha na malimbukeni waliopewa madaraka wakaachi
nchi itopee kwenye ufunjifu wa maadili, tumuunge mkono kama wananchi na jamii
ili tuondoe kadhia hii ya uchafuzi wa maadili kwa faida na heshima yetu kama
jamii ya watu. Maana, ilifikia mahali watu wakaanza kuogopa hata kutazama
runinga kwa hofu ya kuonyeshwa uchafu wakiwa na watoto na jamaa zao. Hongera
kwa mara nyingine rais Magufuli kwa kuanza kurejesha na kutetea maadili ya
kitanzania.
Chanzo: Tanzania Daima, J'tano, Jan., 31, 2018.
No comments:
Post a Comment