The Chant of Savant

Thursday 13 June 2019

Suala la uraia pacha linahitaji akili, busara, maarifa na ujasiri, ukweli na uwazi


Image result for photos of uraia pacha         

Kama kuna suala linaichanganya Tanzania dhidi ya nchi za Afrika Mashariki hata zile tajiri na zilizoendelea si jingine bali la uraia pacha. Hivi karibuni mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (CHADEMA) alifichua roho mbaya, ujinga, ukale na unafiki wa baadhi ya wale wanaojiita wawakilishi wa wananchi baada ya kuanzisha mjadala wa kutaka uraia pacha nchini uruhusiwe. Ahmed Rajab wa the Pan-African Strategic Studies  anasema kuwa kinachoendelea ni mizengwe kwani faida za uraia pacha ni nyingi kuliko hasara zake. Katika nchi zote za Kiafrika, ni nchi kumi tu yaani   Cameroon, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Liberia, Malawi, Tanzania na Zambia ndizo zinakataa uraia pacha
Nchi nyingine za  Afrika ya Kusini, Botswana, Ivory  Coast, Guinea, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Lesotho, Libya, Madagascar, Misri, Namibia,  Senegal na Togo zina namna ya kutambua uraia pacha. Zilizobakia zinaruhusu uraia pacha. Kwa majirani zetu ni Malawi na Zambia tu ambao hawaukubali uraia pacha.
Mbunge wa Namtumbo Edwin Ngonyani (CCM), bila hata chembe ya ushahidi, alisema waliokana uraia wa Tanzania ni wasaliti bila kujiuliza ni kwanini. Wabunge wa CCM na serikali vilishikwa na kigugumizi na kuua hoja hii.  Sijui kama mhusika anajua maana ya usaliti. Na sijui wanaoogopa kulijadili suala hili wanamwakilisha nani na kwanini? Ajabu, hao hao ndiyo wanaohimiza watanzania wanaoishi nje yaani diaspora wakiwamo na walio na uraia pacha wawekeze nchini!
 Mbunge Sugu alisema kuwa waliokana uraia wa Tanzania walilazimishwa na sheria kutokuruhusu uraia pacha jambo ambalo ni kweli tupu. Kimsingi, uraia pacha ulionekana tishio la usalama wa taifa wakati wa vita baridi baina ya Marekani na uliokuwa Umoja wa Kisovieti wa Urusi jambo ambalo pia lilikuwa ni ukoloni mamboleo kwa Afrika baada ya kugawanywa katika makundi haya mawili kwa nyongeza ya mgawanyiko wa mkutano wa Berlin 1884 ulioligawa bara la Afrika kwenye viinchi dhaifu na vidogo vya sasa ambavyo vimeendelea kukumbatia kadhia hii kwa hasara zake. Je na makuwadi wa mabeberu nao wana uraia pacha? Mbona ndiyo hao hao wanaowazuia wenzao wasiwe na uraia pacha kwa visingizio vya kijinga na kutafuta? Wanaotoa ahadi za uongo kwenye chaguzi zetu nao wana uraia pacha? Wanaochezea raslimali zetu wakaishia kutembeza bakuli ughaibuni nao wana uraia pacha? Je mbona serikali zetu zinazokataa uraia pacha zinaendeshwa na fedha za wafadhili? Kuna jambo baya kuliko hili likilinganishwa na uraia pacha kweli? Kama wafadhili ambao nchi zao zimetoa uraia kwa maskini wetu si hatari na tishio, kwanini watu wetu tena wazawa wawe hatari na tishio kwa usalama wa taifa? Huu zaidi kuwa usalama wa kundi la watu, ni usalama gani wa taifa na taifa gani? Je uraia pacha ni nini na nini faida na madhara yake?
Uraia pacha ni ile hali ya mtu kuwa na uraia wa nchi mbili. Sijui mwenye uraia wa nchi tatu au zaidi anaitwaje. Madhara yake nini kwa nchi zinazomtambua au kumzuia kama raia wake? Hakuna utaifiti ulioonyesha madhara yoyote zaidi ya faida.
Mfano, kuna nchi tena tajiri na zilizoendelea zinaruhusu uraia pacha. Sijui nazo hazina tishio lolote? Hii ni kutokana na nchi hizo kutoona tishio lolote liwe la kiuchumi wala kiusalama. Hivyo wanaodai kuwa uraia pacha ni tishio kwa usalama wa taifa hawana hoja zaidi ya fitina na roho mbaya. Hivi kungekuwa na tishio la usalama nchi kama Marekani au Kanada zingeruhusu uraia pacha tena unaoshikilia na wengi wat u wanaotoka kwenye nchi maskini huku zikiwaruhusu kupata elimu na utajiri na kuupeleka kwenye nchi maskini?
         Tuache roho mbaya na ushamba. Rais Baraka Obama ambaye, kama zingetumika sheria za kikoloni zinaong’ang’aniwa na baadhi ya mataifa ya kiafrika ni mkenya ambaye hakupaswa kuwa rais wa Marekani. Kwanza, kwa sababu baba yake hakuwa  raia wa Marekani. Pili, kwa vile baba yake hakuzaliwa Marekani. 
         Mbali na rais Obama, hata rais wa zamani wa Ufaransa,  Nicolas Sarkozy asingefuzu kugombea na kushinda na kuwa rais wa Ufaransa kwa vile baba yake Pál István Ernő Sárközy de Nagy-Bócsa hukuwa amezaliwa Ufaransa.
         Pamoja na utajiri na sensitivities kwa usalama wake wa taifa, Marekani na  Ufaransa ziliruhusu raia wake ambao wazazi wao hawakuwa wazaliwa na wengine raia kugombea na kushinda urais.
Kimsingi, kinachozuia baadhi ya nchi za kiafrika kuruhusu uraia pacha ni ule ukale, woga na kung’ang’ania sheria na mawazo ya kikoloni ambayo baadhi ya watawala walitumia kuwazuia wenzao walidhani walikuwa na uwezo kuliko wao kutogombea urais na sasa kutokuwa na uraia pacha.
Je waliosaini mikataba mibovu ya kuhujumu taifa na kuwaingiza watanzania kwenye umaskini wa kutengenezwa walikuwa na uraia pacha? Je wanaochafua mazingira kwa tamaa na upofu wao nao wana uraia pacha? Walioua mashirika ya umma walikuwa na uraia pacha? Je waliotoroshea fedha nje ya nchi nao wana uraia pacha? Wanaohujumu juhudi za serikali ya sasa nao wana uraia pacha? Walioiuza Afrika, na wanaoendelea kuiuza kwa wakoloni, hawana uraia pacha. Je waliogoma kuiunganisha Afrika na kuendelea kuigawanya ili inyonywe nao wana uraia pacha? Wanaouza uraia na passport zetu nao wana uraia pacha? Walioigeuza Tanzania uchochoro wa madawa ya kulevya hawana uraia pacha. Wanaoua watu wenye ulemavu wa Ngozi na vikongwe hawana uraia pacha. Wavivu na wahalifu wengine hawana uraia pacha. Uzalendo hauna cha uraia pacha wala uraia mmoja.
 Je wachina wanaouza mitumba Kariakoo hawana uraia pacha? Je wageni wale wanaosaidia wageni kuendelea kulihujumu taifa let una watu wake nao wana uraia pacha? Walioghushi vyeti vya kitaaluma au watoa rushwa, majambazi, majangili, wababaishaji, wwabadhilifu, wafanya magaendo, wahujumu uchumi, wauza unga, nao wana uraia pacha?
Simón José Antonio de la Santísima Trinidad Bolívar Palacios Ponte y Blanco Mvenezuela wa kuzaliwa, alikuwa ni rais wa nchi za Venezuela, Colombia, Panama, Ecuador, Peru na Bolivia (ambayo ilipewa jina lake) wakati hakuzaliwa huko. Hapa somo ni kwamba uzalendo haujali idadi ya uraia bali moyo wa mhusika.
Bolivar angekuwa muwafrika huenda angeishia kuwa mbeba zege kama siyo kibaka kutokana na kukatishwa tamaa vipaji na uwezo wake.
         Baada ya kuongelea usaliti wa kukoteza na woga wa uraia pacha, ngoja tuguse kwenye uzalendo. Uzalendo ni ile hali ya mtu kuipenda nchi yake na kuitumikia kwa vile nchi husika inamtumikia na kumthamini. Uzalendo hautoki hewani wala hauji bila sababu. Ndiyo maana kama taifa tunapaswa kujenga uzalendo kwa kuangalia namna mwalimu Julius Nyerere alivyoujenga kwa kupigania na kuleta uhuru na kuusimamia. Je baada ya Nyerere kung’atuka, kilifuata nini? Je hawa walioua mema yote aliyokuwa ameyajenga na kuyasimamia kama vile viwanda, elimu bure, udugu, umoja, usawa, amani na kuwajibikaji walikuwa na uraia pacha? Je wanaotorosha raslimali zetu wana uraia pacha? Je wanaohujumu miradi yetu ya kitaifa wana uraia pacha?
         Ukivuka mipaka ya Tanzania, je madikteta waliochafua sifa ya bara letu walikuwa na uraia pacha? Je vibaraka wa mabeberu na wakoloni wa kisasa wana uraia pacha? Je wanalioua mila na Imani zetu kwa kuleta za kigeni walikuwa na uraia pacha? Wanaowaumiza wananchi wenzao kwa namna yoyote iwe ni kwa madaraka, silaha, elimu, nafasi au vyovyote nao wana uraia pacha? Manesi wanaowatesa wagonjwa hawana uraia pacha wala watendaji wanaowatoa watanzania rushwa hawana uraia pacha. Wabunge wasiohudhuria vikao au kutumiwa na wawekezaji kupitisha mambo yao hawana uraia pacha. Walimu wanaovujisha mitihani na kuwapa mimba wanafunzi wao hawana uraia pacha. Majambazi na wezi hawana uraia pacha. Wavivu na wapika majungu hawana uraia pacha. Wanaoficha madawa na mbolea ili kuwalangua wananchi hawana uraia pacha. Waliohujumu korosho hawana uraia pacha. Wanaopitisha miradi mibovu kama vile barabara, majengo na vifaa visivyokidhi viwango au kupitisha madawa feki na yaliyokwisha muda wake hawana uraia pacha. Maafisaa wa ardhi, forodha, madini, mapato, mahakama, polisi, ushuru, viwango, viwanda na wengine kwenye nafasi nyeti wanaotumia nafasi zao kuwatoza fedha watanzania hawana uraia pacha. Vyangudoa wa kimaadili hawana uraia pacha. Wakwepa ushuru na wanaoiba kwa kalamu wala hawana uraia pacha.
         Wale wanaolazimika kuchukua uraia pacha wanaweza, ima kufanya hivyo kwa sababu ya kutojua sheria na katiba yetu, ukiachia mbali kulazimishwa na mazingira na sheria kandamizi na za kikoloni kwenye nchi zinazojiita huru. Mfano, mtu aliyekana uraia wake ili aweze kupata nafuu katika kupata elimu na ujuzi, kosa lake ni nini? Je aliyechukua uraia wa nchi nyingine ili aweze kuwa na nafuu kusomesha watoto wake kupata huduma za kijamii ikiwemo elimu na ujuzi ana kosa gani? Je mtu aliyechukua uraia wa nchi nyingine ili kupata kazi inayomlipa vizuri ili akawasaidie ndugu zake walioko nyumbani kosa au usaliti wake ni upi?
         Nihitimishe kwa kuwa kusema. Sitetei waliopata uraia pacha wala wale wanaowazuia. Ninachotaka kufanya hapa ni kutaka busara zitumike na sababu za msingi zitumike kuruhusu au kuzuia uraia pacha badala ya sababu za kijinga na roho mbaya kama nilivyoelezea hapo juu. Kwa wenye hofu ya usalama wa taifa, wajiulize vyanzo vya kuhatarisha usalama huu. Kimsingi, wanaokwamisha maendeleo na kuathiri usalama wa taifa letu ni wananchi wenyewe. Kwani mbomoa na mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe. Pia, tujifunze kutoka kwa nchi za kiafrika zilizoruhusu uraia pacha badala ya kuendelea na mawazo ya kikale huku wageni wenye uraia pacha wakiendelea kufumbiwa jicho na watanzani wenye nao wakipatilizwa na kuogopewa bila sababu zozote za msingi na zinaoingia akilini. 
Uchokozi, mbona Wazanzibari wana uraia pacha na hawabughudiwi wala kuonekana tishio kwa usalama wa taifa wala kuvunja katiba? Tia akilini basi.

No comments: