The Chant of Savant

Sunday 14 February 2021

HATUNA HAJA WALA SABABU KUONEA AIBU KISWAHILI

Mwl. J.K Nyerere alipoamua Kiswahili kuwa lugha ya taifa la Tanzania huru, wengi hasa majirani zetu–––tena wengine waliopigania uhuru naye–––walimcheka. Hata hivyo, Nyerere alishikilia uzi ule ule ingawa naye hakukitangaza Kiswahili vizuri. Hakukitumia  zirani nje au kuhutubia vikao vya kimataifa kama wafanyavyo viongozi wa mataifa yanayotumia lugha zao asilia kama lugha za taifa.  Leo tuna mataifa yanayojivunia kujua Kiingereza bila kukijua huku yakisema Kiswahili ni lugha zao za taifa. Lugha ni nyenzo ya mtu kuiona na kuielezea dunia yake. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa watu wanaelewa zaidi kwenye lugha mama kuliko lugha za kigeni. Najua Kiswahili si lugha mama ya watanzania wote. Angalau ni lugha ya pili yenye kukaribiana na lugha mama ikilinganishwa na lugha za watawala wetu wa kikoloni ambao hatuna ukaribu kimila au kwa lolote.
        Uhuru maana yake ni ile haki ya binadamu kujiamria bila woga kufanya kile unachoona kinafaa kisheria kama mtu binafsi, jamii au nchi. Kwa kuzingatia dhana hii, Rais John Pombe Magufuli alipoingia madarakani aliamua kukanyaga nyayo za Mwalimu bila aibu wala woga tena kindakindaki kwa kuamua kutumia Kiswahili kama lugha yake ya mawasiliano katika kila shughuli ya kitaifa anayofanya kama  rais. Hata hivyo, uamuzi huu–––tokana na mabaki na mtindio wa kikoloni–––haukupokelewa na watanzania wote.  Wapo waliombeza kwa maneno mengine wakidai hajui kiingereza. Magufuli aliwashangaa hawa kwa kuhoji aliwezaje kupata shahada mbili za juu moja ya uzamili na nyingine ya uzamivu bila kujua kiingereza wakati masomo yote yalifanyika kwenye lugha hii?
  Hivi karibuni, akihutubia sherehe za kuadhimisha miaka 100 ya mahakama, alisema wazi alivyojiamini na kuisimamia lugha ya Kiswahili pamoja na kukejeliwa kuwa hajui kiingereza. Kuonyesha alivyodhamiria, Magufuli alimpandisha cheo jaji wa mahakama kuu kanda ya Musoma, Zephrine Galeba kuwa jaji wa mahakama ya rufaa kwa uzalendo wake wa kutoa hukumu kwa Kiswahili jambo ambalo, licha ya kumvutia rais, lilimpa imani kuwa idara ya mahakama itaweza kubadilika na kuanza kuenzi na kutumia Kiswahili katika kazi zake. Je hili litawezekana bila kutungiwa sheria?
        Nchi za kiafrika kuogopa kutumia lugha zao ni aina fulani ya ukoloni ambayo inapaswa kuangaliwa upya. Nadhani haya ndiyo matokeo ya dini za kigeni zilizowafundisha waswahili kuwa karibu kila kitu chao ni cha shetani isipokuwa vyakula vyao na wanyama wao. Ndiyo maana watu wenye mawazo ya kikoloni tena ya kujitakia wanaogopa lugha na majina yao. Ndiyo, tunahitaji kiingereza kama lugha inayotumika sana duniani. Hili lisitupe unyonge wa kuogopa lugha zetu asilia au za taifa zenye asili ya Afrika kama Kiswahili. Nikiwa Kenya kipindi fulani, majirani zangu walisema mimi si mtanzania kwa vile naongea kiingereza kizuri. Niliwajibu mbona marehemu baba wa taifa alikiongea vizuri kuliko rais wao wa awamau ya pili hata wa awamu ya kwanza? Niliwasuta kuwa nawasikitikia kwa vile hwakuwa wakijua ima kiingereza au Kiswahili wakati mie navimudu vyote bila wasi wasi.
        Kama tutakuwa wakweli, watu wetu wengi kiingereza kinawapa taabu si kwa sababu hawakijui bali hawakuandaliwa kukijua tokana na fikra huru za baba wa taifa. Juzi nilimsikia mkuu fulani wa wilaya akisema visibility studies badala ya feasibility studies. Hii inaweza kuonyesha ni kwanini tunahitaji lugha yetu ambayo watu wataitumia kwa kujiamini. Hata wanaojifisia kujua kimombo wana matatizo kibao. Mfano, ukimwambia mkikuyu pale Kenya aseme neno pond atakwambia pod. Ukimwambia mmeru aseme neno pond atasema mpond. Uganda nako utasiki exichuse me badala ya excuse me. Pale Nigeria wanasema  broda badala ya brother. Afrika Kusini wanasema struggal wakimaanisha struggle. Hii ni kuonyesha namna waswahili tunavyoweza kutumia lugha zetu na mambo yakaenda. Ni ushahidi tosha kuwa, pamoja na kutumia lugha za wenzetu, bado tunazibukanya au kuboronga huku tukijisifu tunazimanya. Huku Ulaya ukiongea mfano kiingereza, hutaacha kusikia kuwa una accent au lafudhi kukuonyesha kuwa hii si lugha yako na huwezi kuimilki kama wao. Huwa najiuliza. Kama nina lafudhi na unajua, una haja gani ya kuniambia kama siyo ubaguzi tu wa kawaida na kujiamini kwa wale wanaojiona ndiyo wenye lugha?
        Kama tutajivunia lugha za watawala wetu wa kikoloni basi tujivunie na zetu. Hii inanikumbusha wasudan ya Kaskazini ambao huonea fahari kiarabu hadi kujiita waarabu wakati waarabu wakiwaita watumwa yaani abid kutokana na kujikana na mila na lugha zao. Naamini kuwa unapojikana na wengine watakukana. Usiopojiamini hutaaminiwa na usipojipenda hutapendwa. Kimsingi, utachuliwa na wengine kama unavyojichukulia. Na hii ndiyo siri ya nchi za magharibi kujiamini hata pale zinapokuwa zinatufunza vitu visivyoendana na utamaduni na  imani zetu waka kuingia akilini. Ndiyo maana Wasudan hata wanaposhiriki kwenye mikutano ya nchi za kiarabu au kwenda kufanya kazi kwenye nchi hizo wanaonyeshwa wazi kuwa wao ni waswahili na si waarabu. Ukitaka kujua mbuzi au kondoo ni kondoo au mbuzi, mpeleke kwa wale wanaosema ni mbuzi au kondoo wenzake. Wakimpokea basi ni mwenzao. Hata hivyo, hata wanyama pamoja na ufinyu wao wa akili bado hawawezi kumkubali mnyama ambaye si mwenzao. Mbuzi watamkubali mbuzi na kumkataa kondoo na kondoo kadhalika watamkubali kondoo na kumkataa mbuzi kama ambavyo waarabu hufanya kwa wasudani. 
        Tumalizie kwa angalizo na ushauri. Kuenzi lugha zetu hakuna maana ya kuzikimbia lugha za watawala wetu hasa kutokana na ukubalikaji wake duniani. Tunaweza tukaendelea kuzitumia bila kukimbia lugha zetu. Mbona mataifa kama Japan Korea Kusini na Uchina yaliyoendelea yanatumia lugha zao asili na yameendelea? Hatuna haja ya kuogopa kutumia Kiswahili katika mambo yetu ya kitaifa; ni lugha sawa na nyingine yenye uwezo kuwa na dhana zote tunazodhani zinapatikana kwenye lugha za kigeni tu.
Chanzo: Nipashe Jpili.

No comments: