The Chant of Savant

Sunday 21 February 2021

Tuzalishe Wabunifu na Si Wasaka Ajira

Hivi karibuni, kulikuwa na mjadala mkali bungeni juu ya wasomi tuzalishao siku hizi kutoweza kuwa na ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa. Tukiachana na kujisahaulisha, kipi kilichobadilika kwenye mfumo wetu wa elimu tangu kupata uhuru? Je hawa wanaolalamika si matunda ya mfumo huu huu ambao walishindwa kuubadili?  Je nini kifanyike?  Je tuanzie wapi na lini kuzalisha wale kwa kimombo naweza kuita thinkers and inventors but not job seekers, yaani wenye kufikiri sawa sawa na wawekezaji na si wasaka ajira.
        Katika kujaribu kutoa mapendekezo juu ya namna ya kubadili mfumo wetu, nilisikia baadhi ya wabunge–––hasa wale waliokata tamaa na kushindwa kubuni mbinu mbadala–––wakipendekeza kuwa tupunguze usajili wa vyuo vinginevyo watakaotaka kuvisajili watuhakikishie ajira. Hii ililenga kuandaa watu ambao tayari vyuo vitakuwa vimeishawatafutia kazi. Je hili ni endelevu? Kwanza,  kazi ya vyuo si kuwatafutia watu ajira bali kuwapa elimu waliyoridhika nayo hadi wakaomba kujiunga na vyuo husika. Vyuo haviwaiti watu kuja kusoma bali watu huomba viwapokee na kuwaelimisha. Pili, si lazima kila huduma imhakikishie mafanikio kila anayoipata toka kwa anayoitoa. Vyuo si sawa na majiko au hoteli. Hutoa ujuzi unaoweza kumfaa mtu maisha yake.
        Wengine wangependekeza hili la kuwatafutia wahitimu wa vyuo kazi lakini si wabunge. Wao wabunge wanatuhakikishia nini tunapowachagua? Ni wangapi wamekaa bungeni makumi ya miaka bila kuleta mabadiliko kwenye majimbo yao? Kwanini hawapitishwi kwa kutuhakikishia watatimiza ahadi na malengo ya kuchaguliwa kwao? Mfumo wa kuzalisha wasaka ajira utaweza kujibadili kirahisi bila kuwapo na ving’ang’anizi? Kuubadili, tunahitaji mawazo yenye siha na si ya kukata tamaa au kufikiri juu ya visivyofikirika. 
        Je madaktari ambao wagonjwa wao watakufa nao wafukuzwe kazi au walimu ambao wanafunzi wao watashindwa? Je polisi ambao maeneo yao yatakumbwa na uhalifu itakuwaje?
        Nadhani badala ya kuanza kulaumu kifaa, tuanze kufikiri. Hata hivyo, sishangai wanaotoa mapendekezo kama haya ya kichovu. Wengi wao si wasomi, wanachukia usomi na wasomi–––kama baadhi yao walivyoonyesha kwenye michango yao–––na hawapendi hata kujiendeleza mbali na kuchukia wasomi. Wapo waliosikika wakisema kuwa watu wenye PhD au shahada nyingine za vyuo wasiajiriwe kwa vile wamewaangusha. Je Magufuli naye na PhD yake amewaangusha? 
        Tuache mjumuisho ambao, kisomi, ni dalili ya uvivu wa kutafiti na kuelewa mambo. Tatizo, kwa mfano, matatizo kama vile majungu, rushwa, uvivu, udokozi, ukosefu wa uzalendo, wizi na mengine kama hayo si ya la wasomi wala vihiyo. Ni tatizo la watu binafsi. Kuna wasomi mafisadi sawa na vihiyo. Kadhalika kuna vihiyo waadilifu sawa na wasomi. Huwezi kuchukia au kuharamisha utuli eti kwa sababu unasababisha mafua badala yake ukaamua kutumia samadi, pamoja na harufu yake mbaya, eti kwe vile haisababishi mafua. Hapa dawa ni kutafuta namna ya kutumia utuli na kuzuia mafua na siyo vinginevyo. 
        Swali kuu na la kufikirisha hata kama ni gumu tunalopaswa kujiuliza na kulitafutia jibu sahihi haraka ni kwanini wenzetu waliweza kufanikiwa kwa kutumia wasomi badala ya kuanza kufikiria kwa kurudi nyuma badala ya kwenda mbele. 
        Tuhitimishe;  dawa nyingine ya kuondokana na wasomi au wananchi wezi bila kujalisha usomi wao ni kuwa na nchi yenye mfumo unaohimiza maadili kisheria na kimila. Nimekuwa mpiga kelele mkubwa wa dhana nzima ya kuhakiki mali za watumishi wetu wa umma na watanzania kwa ujumla. Hii, licha ya kutia nidhamu, huleta uwajibikaji na uchumaji wa halali na kupunguza tamaa za mali na wizi vilivyotamalaki nchini kiasi cha watu kusoma au kutosoma ili kutafuta nafasi ya kulihujumu taifa. Hata hawa wanaopiga kelele kuwa wasomi wameangusha taifa hili, ukiwauliza–––pamoja na kujisifia na ukihiyo wao–––wameifanyia nini nchi zaidi ya hao wanaowalaumu. Kwanza, kutotaka kujielimisha ni dhambi ukiachia mbali kuwa kikwazo cha maendeleo hasa kama dhana nzima ya kusoma ni kumkomboa mwenye kuelimika au kupokea elimu. 
        Ni kweli. Tunao wasomi wa hovyo walioshindwa kujikomboa wao na jamii yao sambamba na vihiyo. Hata hivyo, mateso ya asiyesoma katika maisha ni tofauti na aliyesoma. Elimu, hata isipoleta ajira, humfanya aliye nayo angalau kujiamini akilinganishwa na asiye nayo. Ndiyo maana, watu wanaghushi shahada au kujipatia shahada za vyuo za juu hata kama hawajazisomea. Hii ni kutokana na kutaka wapewe heshima ambayo wenye shahada husika hufaidi au kupewa na jamii. Mfano, mtu mwenye shahada ya uzamivu (PhD), siyo sawa na tajiri mwenye cheti cha darasa la saba. Asiyejua kusoma na kuandika halingani na asiyejua kusoma na kuandika. Asiyeona ajuaye kusoma na kuandika ni bora kuliko mwenye macho asiye na ujuzi huo. 
Chanzo: Nipashe J'pili.

No comments: