How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 16 February 2021

WAHESHIMIWA WABUNGE WAFANYE UTAFITI KABLA YA KUJISEMEA


Siku ya kwanza ya mkutano wa Bunge unaoendelea, ilianza kama kawaida. Waheshimiwa wabunge waliuliza maswali. Mawaziri wakijibu hoja na maswali ya Wabunge. Kupitia mitandao, tuliweza kuona mkutano wa Bunge. Kitu kimoja kilinivutia kuandika makala hii.  Ni mchango wa Mbunge wa Vunjo Dkt. Charles Kimei–––licha ya kuunga mkono mipango ya serikali na kuchangia kirefu kwenye uchumi wa taifa–––alitoa ushauri uliwavutia wengi kuwa uwekezaji katika elimu, kwa sasa, usijikite kwenye utitiri wa shahada bali stadi za kazi zinazojibu mahitaji ya sasa. Mfano  Kimei alisema kuwa ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu ni mkubwa kuliko wa wahitimu wa vyuo vya stadi mbali mbali. Kimei alishauri serikali kuliangalia hili ili kuepuka kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ambayo hayatawawezesha kupata ajira na kurejesha mikopo. Sambamba–––bila kutaja masomo husika–––mheshimiwa Spika alimuunga mkono Kimei kuwa kuna baadhi ya kozi zinazofundishwa kwa sasa vyuoni zilizopitwa na wakati jambo ambalo ni kweli. Yote haya ni mambo ya kawaida ya kibunge. Hata hivyo, kilichotufanya kuandika makala hii na kichwa chake ni ile hali ya Mbunge wa Geita  Vijijini Joseph Kasheku (Msukuma) kuomba kumpa taarifa Kimei. Kawaida, taarifa hutolewa pale ambapo kuna jambo halikubaliwi na mtoa taarifa au lenye kupewa au kuhitaji ufafanuzi zaidi. Kasheku alimpa taarifa mheshimiwa Kimei kuwa matajiri wote duniani hawana shahada. Hii si kweli. Ni matajiri gani mheshimiwa alimaanisha? Je hili linawafundisha nini watoto wetu zaidi ya imani potofu kuwa ukiwa na elimu kubwa huwezi kuwa tajiri au utajiri na elimu haviendani? 
Tukianzia Tanzania, tajiri mkubwa kuliko wote, Mohamed Dewji ana shahada. Matajiri waliotangulia mbele ya haki: Ali Mfuruki na Reginald Mengi wote walikuwa na shahada au elimu inayokabiribiana na shahada. Kimataifa, matajiri wanaoongoza kwa sasa yaani Elon Musk ana shahada mbili BA na BS toka chuo kikuu cha Pennsylvania na  Jeff Bizos  ana BSE toka chuo kikuu cha Princenton. Lazima tukubali. Hata hao matajiri ambao hawana shahada kama Bill Gates na Mark Zuckerberg ni wasomi ambao walitokea vyuoni walikokatiza masomo yao na wengine bado wanajisomea ili kupata maarifa.  Hivyo, licha ya kuwa uongo, ni upotoshaji mkubwa kujumlisha matajiri wote kwenye kapu la ujinga kwa sababu eti wengi wao hawana shahada. Tunachopaswa kuwaambia watu wetu ni kwamba watafute maarifa yatakayowasaidia kupambana na matatizo yao. 
Mahitaji ya elimu yanatofautiana tokana na wakati na nyanja. Kwa mfano, mtu aliyezaliwa pindi tu baada ya kupata uhuru, alihitaji elimu kwa ajili ya kujitambua na kutambua mchango wake katika kuutimia na kuudumisha uhuru wetu. Ndiyo maana wale walisoma miaka ya 60 hadi 70 walijikita sana kwenye fasihi na masomo ya namna hii kwa sana. Baada ya hapo yalianza kuibuka masomo kama vile uhasibu, uinjinia, udaktari, uanasheria bila kusahau ualimu ambao hata hivyo ulikuwa big deal pindi tu tulipopata uhuru. Kwa sasa masomo mengi yanapaswa kuhusiana na mahitaji ya sasa kama vile jinsi ya kwenda na utandawazi, mitandao, electroniki, uchumi wa kijani, ugaidi na masuala kama haya. Pamoja na mahitaji tofauti ya elimu na ujuzi kwa nyakati na malengo tofauti, bado elimu ni muhimu. Hili halina mjadala. Ndiyo maana ukiangalia teuzi nyingi anazofanya rais Dkt. John Magufuli zinahusisha watu wenye shahada za juu. Kwanini asiteua tu watu bila kujali viwango vyao vya elimu?
Tokana na kukua kwa elimu ya taifa letu, tungependekeza hata wabunge wawe na angalau shahada moja ili kuwamotisha vijana kujua umuhimu wa elimu na siyo utajiri. Sidhani kama tutawaaminisha kuwa unaweza kuwaaminisha vijana wetu kuwa unaweza kuwa tajiri bila elimu tutakuwa hatutoi motisha kwao kujiingiza kwenye njia haramu za kupata utajiri wa haraka kama vile uuzaji na usafirishaji mihadarati, ujambazi, utapeli na kadhia nyingine. Hakuna nchi iliyoweza kuendelea bila kuwa na jamii ya watu wasomi hata kama hawana ajira. Nadhani tujifunze kuwa elimu iwasaidie walioipata kutatua matatizo yao mojawapo likiwa ni tatizo la ajira. Kanada inasifika kama nchi yenye wasomi wengi. Kwa udogo wa taifa hili kwa idadi ya watu, lisingekuwa na wakazi na wananchi wasomi, lisingeweza kujulikana kwenye ramani ya dunia sawa na mataifa makubwa yenye idadi kubwa ya watu.
Ukiuangalia utajiri au kipato kikubwa kirahisirahisi, utagundua ni kwanini watu kama mheshimiwa Kasheku wana imani kuwa elimu haina uhusiano na utajiri. Kwa watanzania wa kawaida kama Kasheku, mshahara anaoupata¬¬–––ikilinganishwa na kiwango cha elimu na ujuzi vyake–––ni mkubwa sana. Hivyo, kwa mtu ambaye malipo yake kila mwezi ni makubwa kuliko ya wengi wenye shahada za juu, humfanya asione faida ya kuwa na elimu ya juu. Hata hivyo, kosa la watu wenye elimu za juu wasio na ajira au ajira zenye kipato cha juu si kosa lao bali kosa la mfumo mbovu tuliourithi toka kwa wakoloni. Ndiyo maana hatuoni mantiki, kwa mfano, ya kutowalazimisha wanaogombea ubunge angalau kuwa na shahada ili waeze kuwa mchango mzuri bungeni.
Tumalizie kwa kuwaomba waheshimiwa wabunge kuhakikisha wanafanya utafiti wanapotoa matamko au taarifa, kwa vile wao ni kioo cha jamii. Pia tuwahimize kujisomea hata kama siyo lazima wawe na shahada. Angalau wawe na welewa kwa kawaida unaowawezesha kujenga hoja na mahitimisho bila mijumuisho isiyo na ulazima kama ilivyo kwenye hoja hii ya elimu na utajiri.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: