The Chant of Savant

Tuesday 25 January 2022

Barua Rais, badili mfumo wetu wa elimu wa kikoloni na kukariri

Mheshimiwa Rais, nakusalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Japo zimepita siku nyingi bila kuwasiliana nawe, kuna mambo yaliingilia kati ambayo sitaki kuyataja. Hata hivyo, leo narejea kuwasiliana nawe kuhusiana na suala zima la ujinga unaoitwa elimu katika taifa letu.  Naenda moja kwa moja kwenye mada. Juzi niliona baadhi ya watanznaia wakisherehekea ‘ushindi’ wa watoto wao waliomaliza kidato cha nne. Wale ambao watoto 3ao waliongoza au kupata madaraja ya juu, bila shaka walishangilia na kuona kama nusu ya njia ya mafanikio wameitimiza wakati si kweli.
        Leo naandika kutoa mfano kwa taifa ambalo, kwa sasa, linashikilia nafasi ya kwanza kuwa na wananchi wengi waliopiga shule kweli kweli na pia rekodi ya maisha mazuri kuliko mataifa yote duniani kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la US.News. Hivyo, naongea toka kwenye nchi ambayo hata bila ya utafiti huu, inasifika kwa maisha yake ya hali ya juu. Hata hivyo, leo siongelei ubora wa maisha kama vile huduma za hali ya juu za afya kwa kila mwananchi na mkazi, elimu, ajira, na mambo mengine mengi. Leo naongelea elimu. Hapa Kanada, hakuna mambo ya divisheni one au zero. Watoto wanasoma kuanzia darasa la kwanza hadi 12 na wakishatimiza idadi fulani ya vipindi wanaruhusiwa kujiunga na vyuo vikuu wanavyochagua. Hapa, hakuna mtihani wa kumaliza darasa la 12 bali kusoma na kufikia sifa zinazohitajika kujiunga na chuo kikuu. 
        Kihistoria, mtindo wa sasa tulio nao tuliurithi kwa wakoloni kwa nia ya kutuchelewesha. Sababu ya pili ni umaskini.  Kwani, tulikuwa na chuo kimoja kikuu cha umma.  Hivyo, kuepuka kuoneana, tuliendeleza utaratibu wa kuwakaririsha watoto wetu mambo mengine hata yasiyo wasaidia ili washinde na kwenda chuo kikuu. Je tunapaswa kuendelea na utaratibu huu wa kizamani wakati tuna vyuo vingi vikuu au kuubadilisha mfumo wet una kuanza kutoa elimu yenye mashiko badala ya kushindanisha ujinga?
        Kuna watu wengi nawafahamu waliopata alama za juu kwenye mitihani yao ya kidato cha nne na cha sita wakaingia chuo kikuu na kushindwa vibaya sana. Hii ni kutokana na mazingira na vigezo vilivyowekwa kujenga tabaka la watu wanaosoma ili wakariri na kushinda lakini wasioweza kujisaidia hata kimaisha wanapotoka vyuoni hata mashuleni. Kwanini tusibadili utaratibu huu ili kuwapa watoto wetu fursa za kusoma bila presha ya mitihani ili waelewe wanachopaswa kufanya baada ya kumaliza elimu zao hata angalau wajiajiri na kuwaajiri wenzao.
Mheshimiwa Rais, nakumbuka siku moja ukiwafunda baadhi ya watanzania ulisema kuwa shuleni ulikuwa mwanafunzi wa wastani na hukuwa umesoma sana mwanzoni ulipoajiriwa ukiwa mdogo. Lakini kwa sasa uko wapi? Je wewe ulipata daraja gani? Tukichulia mfano wako, madaraja ya ushindi maana yake ni mgawanyiko. Tunamgawanya nani kupata nini?
        Hapa Kanada mambo ya mshindi na mshindwa yalishazikwa. Mwanafunzi akimaliza darasa la 12 anakwenda chuo kikuu siyo kwa ushindi bali kumaliza idadi ya masomo yanayotakiwa.
Hawa waliofanikiwa hata bila kufikia kidato cha nne walipata division gani? Japo siungi mkono ukihiyo kama nilioshuhudia juzi mbunge fulani akipewa shahada ya uzamili feki, tokana ujinga wake, akajisifu yeye ni daktarin wakati si kweli, niseme wazi kuwa siyo shabiki wa madaraja na utaratibu wa sasa wa elimu nchini. Mie nakumbuka nilipata daraja la pili sekondari kwenda kidato cha sita. Wale waliokuwa wamepata daraja la kwanza pointi za mwanzo mwanzo walituona sisi kama waliofeli japo wengi tuliwashinda vibaya sana.
Je imekuwaje nchi zilizoendelea zimeachana na mambo ya ushindani wa kukariri badala ya uelewa? Jibu ni rahisi kuwa tunashindanisha ujinga badala ya ujuzi kama jamii na taifa. Tutamalizwa na kujimaliza wenyewe kwa kuendeleza mawazo mgando.
Leo sitaandika mengi. Nitaandika machache ili upate fursa ya kutafakari na kufanya uamuzi wa kuondokana na ukale na ujinga wa sasa ambapo tunaendekeza kukariri badala ya kuelewa na kuelimika. Ndiyo maana unakuta watu wana shahada nyingi lakini wakiingia kwenye utendaji wanaboronga. Nadhani, kama rais unakumbuka kisa cha mzee Abeid Karume aliyejenga majengo ya Michenzani yakawashinda madaktari hata kuyapaka rangi.
Naomba nimalize kwa kukuomba uangalie namna ya kubadili mfumo wetu wa elimu kutoka kwenye kukariri na kwenda kwenye kuwapa sifa zinazotakiwa vijana ili waweze kupambana na maisha. Nadhani mfano toka Kanada unatosha kukufungua macho. Unaweza hata ukafanya utafiti wako mwenyewe kwenye nchi nyingi za magharibi. Mie ninayeandika, nilikuja hapa na stashahada. Nilikwenda kuomba nafasi ya kusoma, wakanipa mtihani wa kupima upeo wangu wa kuelewa na kiingereza nikakubaliwa. Na ninapoandika, niko nafanya utafiti andiko la tasnifu yangu ya shahada ya uzamili ambayo nimeifanya kwa miaka mitatu badala ya minne. Kwa mfumo wetu wangenikatalia kusoma chuo kikuu. Mfano mwingine, niliwahi kuomba kusoma chuo kikuu huria wananikatalia eti kwa vile sina cheti cha kidato cha nne! Ajabu hapa hawakuniuliza upuuzi wa cheti cha sekondari wala nini zaidi ya kuniingiza chuoni na kufanya shahada ya kwanza na pili za miaka minne minne nilizofanya ndani ya miaka mitatu mitatu. Mbali na kutegemea kupata shahada ya uzamivu, ni mwandishi wa vitabu zaidi ya 20 tena ndani ya miaka saba vingi vikiwa vya kiada. Je ni watanzania wangapi wana rekodi kama hii? Kama kuna nilichojifunza hapa, ni kuwa elimu siyo madaraja ya juu bali mfumo mzuri wa elimu.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: