The Chant of Savant

Monday 3 January 2022

Muda wa Kukomesha Wasabaya ni Sasa

Hivi karibuni kulikuwa na kesi ya mmoja wa wateule waliowahi kutumia madaraka vibaya, wakajisahau, wakajivuna, wakaamini binadamu wenzao huku wakimtelekeza Mungu na umma wake. Jamaa huyu ambaye bado ni kijana, japo ameishakaangika na kusulubika. Mwenyewe, anawakilisha wengine kama yeye waliogeuza uongozi wa umma sehemu ya kufanya ubabe, ujambazi hata upumbavu. Hawa kwa vile siwezi kuwaorodhesha hapa kwa kuogopa kulisababishia kesi, nitawaita WASABAYA yaani Watu wa Ajabu, Songombingo Ambao Bora Angalau Yawakute watie Akilini. Wasomaji wangu wengi wanawajua malimbukeni hawa waliopewa ulaji wakaaminiwa madaraka wakajisahau na kusahau kuwa kuna kesho na Mungu.
        Maskini aliyewaamini walimuangusha vibaya mbali na vijana wengine kuwaonyesha kama viumbe ambao hawapaswi kuaminiwa madaraka makubwa ya umma. Hawa WASABAYA, mbali na kutumia madaraka vibaya, kuuibia, kuaibisha umma, pia waliumiza watu wengi wasio na hatia.Walivuruga na kuibia biashara za watu wasio na hatia. Walidhulumu haki za wanyonge bila kujua kuna kesho tena yenye mashaka kama ilivyo sasa kwa wao baada ya kuona mmojawapo akilipia uovu wake. Wapo waliosingizia watu huku wakiwatoa fedha na kutokea kuwa matajiri bin vu. Wapo walioonea watu kwa vile walikuwa na bifu nao au kuonyesha kujikomba na kujipendekeza kwa wakubwa waliojitahidi kuwafurahisha hadi wakawaudhi. Je hawa tunangoja nini kuwakamata lau warejeshe kilicho chetu? Je kuna majambazi, mafisadi na wezi kama hawa ambao ukwasi wao hauna maelezo? Kweli, kama jamii na taifa tuendelee kuwaona wakitanua mali walizopata kwa kutuhujumu na kutuibia nab ado tuendelee kujiona watu wenye busara na wenye kujitendea haki ukiachia mbali wahanga wa uovu huu? Je tunahitaji ushahidi gani wakati walikuwa wakifanya USABAYA wao mchana kweupe? Je tunangoja nini na kwanini ili iwe nini wakati kila kitu kiko wazi? Je tukiendelea kutowashughulikia haiwezi kujenga picha kuwa kuna wakubwa walikuwa wakiwatuma na kuwatumia?
        WASABAYA si watu wa kuaminiwa madaraka tena. Utawaaminije watu wanaotumia kanuni na sheria za matumbo yao huku wakizivunja na kuzitelekeza sheria za nchi? Tutawaaminije watu hatari kwa umma ambao mtaji wao mkubwa ni kujipendekeza, kujihudumia ukiachia mbali kutumia mamlaka ya umma kujinufaisha binafsi? Utawaaminije watu waroho kuliko fisi na wenye kufikiri kwa matumbo au tuseme makalio badala ya vichwa? Wangapi tuliwaona wakinyanyasa watu wetu, wakisingizia watu wetu kwa makosa ya hatari kama vile uuzaji mihadarati huku wakijigeuza wafalme ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Walivamia maofisi, kuteka hata kutesa mbali na kuumiza wenzao wasijue za mwizi ni arobaini na aliyeko juu huna ya kumgoja chini asikuangukie wala kumpandia mkaanguka pamoja zaidi kukaa pembeni ili atakapopomoka apige makelele umsikie ushuhudie kilio chake na maanguko yake.
        Kuepuka kuonekana napiga chuku au kuzua umbea, jikumbusheni mmoja aliyekuwa mkubwa wa jiji fulani kubwa tu nchini ambaye alisifika kwa matumizi mabaya madaraka akijifanya muungu mtu asijue kuna kesho. Tujikumbushe alivyokuwa akitumia michuma ya bei mbaya ambayo hatujui huo ukwasi wa kuinunua aliutengeza lini wakati alikotwa kwenye majalala kama yule msomi fulani aliyepewa ulaji akakufuru kwa kumsifia Kaisari hadi akaidhalilisha taaluma yake adimu ukiachia mbali kuwa alipata cheti cha juu japo hakuelimika vilivyo. Jamaa huyu aliyetuhumiwa kughushi hata vyeti vya kitaaluma akachuniwa na Kaisari kabla ya kufarakana naye anajulikana na anapaswa apelekwe mbele ya pilato kulipia USABAYA wake kama MSABAYA mwenzake ambaye ameishanyolewa bila maji. Je kwanini tusifungue makabrasha yake tukamshughulikia kama wengine walioshughulikiwa kwa makosa kama yake huku tukimdai arejeshe fedha na vyote alivyopata kwani hakustahiki kuvipata kwa vile alighushi?
        Kipindi kile cha makamuzi yaliyokuja kuisha ghafla aliogopwa na kila mtu. Nani amesahau wahanga wake tena wengine wakiwa na ulaji mkubwa kuliko wake? Nani amesahau waziri aliyetaka kumchunguza akatishiwa bastola kabla ya kuonyeshwa mlango wa kutokea kwenye mazingira yenye kutia utata na kuonyesha uonevu na upendeleo wa wazi kabisa? Kwani hatukuyaona? Nani huyu ambaye hakuyaona wala hayakumbuki haya kana kwamba hakuwapo ili tumkumbushe na kumfunza umuhimu wa kuwapatiliza WASABAYA lau liwe somo kwa wenye mawazo na tabia za KISABAYA? Kwanini tusimbane akarejesha kilicho chetu lau tuwafidie wahanga wa uovu na jinai yake?
WASABAYA walitoa picha iliyoungua na mifano mibaya ambayo tunapaswa kurekebisha ili tusiendelee kuonekana kama tunaunga mkono USABAYA au tunaadhibu WASABAYA fulani na kuwaacha wengine. Hawa lazima tuwaadhibu ili kutoa fundisho na onyo kwa WASABAYA ambao hawajaaminiwa ofisi za umma au wanazo ili hawajaanza USABAYA wao. Nchi yetu siyo shamba la bibi kuruhusu kila kenge na nyani kufanya USABAYA.
        Tumalize kwa kuwaomba wenye mamlaka wawashughulie WASABAYA lau turejeshe heshima ya taifa huku tukitenda haki kwa yale tuliyofanyiwa mchana kweupe. Tupambane USABAYA wa jana, juzi, leo hata kesho ili wenye kudhani wanaweza kutuchezea, kutudhulumu, kutuhujumu, kutuibia, kutunyanyasa, kututesa hata kutudhalilike yawakute na kuwarudia waliyotutenza. Hakika saa ya kuwakomesha WASABAYA ni sasa.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: