The Chant of Savant

Monday 3 January 2022

Barua kwa Mheshimiwa Spika Ndugai

Mheshimiwa Spika wa Bunge Job Ndugai, nakusalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sema kazi iendelee. Leo sitaki nikupotezee muda kwa kuzungusha. Juzi ulinishangaza sana. Nilishangaa siyo kwa sababu jambo lililonishangaza ni la kushangaza bali mkinzano wako na Mwenyekiti na Rais wako wa moja kwa moja. Japo wote tuna haki ya kueleza mawazo yetu bila kuzuiliwa, siyo kila mawazo ni ya kueleza kwa jamii yote. Mfano Mheshimiwa Spika ulikaririwa ukisema kuwa “juzi mama ameenda kukopa 1.3 trilioni. hivi ipi bora. Sisi Watanzania wa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa na madeni au tubanane banane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa makubwa haya yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe ‘and how’ (na kwa vipi?” Je una maana haya madeni hayaeleweki kweli na yanafichwa au kunani? Je ulishindwa kumpa ushauri huu mzuri Rais au ulimshauri akakataa hadi ukaamua kulipuka?
Kwa wanaojua sera za CCM na dhana ya uwajibikaji wa pamoja kwa serikali iliyoshikamana na kufanya kazi kwa pamoja, wanashangaa. Wapi kuna tatizo hadi mambo kama haya yanayopaswa kuwa ya ndani ya chama na serikali yake yanamwagwa hadharani? Kunani hapa? Je kati yako na Mwenyiti wa Chama chako ambaye ni Mheshimiwa Rais tumsikilize nani? Na nani anasimamia sera za chama na mipango ya serikali kama mlivyojipangia kwenye manifesto yenu?
        Mheshimiwa Spika, japo mawazo yako yanaonyesha au kulenga kuonekana kama ni ya kizalendo tena ya kujitegemea, je huoni hata hivyo yanalenga kuwaumiza watanzania hasa wa kipato cha chini unaotaka watazwe tozo watake wasitake ikilinganishwa nanyi mnaolipiwa simu zenu na hao hao kwa kodi zao? Kwanini kutoza na siyo kuhimiza ukusanyaji wa kodi au kubana mafisadi wanaojulikana mbali na kupunguza nyadhifa zisizo za lazima na marupurupu yake lukuki yanayovutia hadi matapeli waliojificha vyeo vya kidini kuziwania? Je baada ya Mheshimiwa Rais kukujibu utachukua hatua gani? Ngoja ni kukumbushe alivyosema “fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo wala kwenye kodi tunazokusanya ndani ni lazima tutakopa ili kukamilisha mradi huu. Ni lazima tukope twende tumalize huu mradi.”
        Mheshimiwa Spika, je ulipoanza ubunge ulikopeshwa shangingi lako au uliwachangisha kama siyo wananchi wako basi familia yako? Je kama ujuavyo hali ya sasa yenye maendeleo makubwa ya miundo mbinu, kweli wabunge na maafisa wengine wa serikali hata wasiostahiki kweli bado mnastahiki kuendelea kutumia mashangingi huku walipa kodi wakilipia ukiachia mbali kuchafua mazingira?
        Mheshimiwa Spika, usemayo ni kweli; hakuna anayependa nchi inayokopakopa kama inafanya hivyo kutanua. Je umejiuliza inakopa kwa sababu gani iwapo, kama anavyosema Mheshimiwa Rais kuwa hata hayo mataifa yaliyoendelea yanaendelea kwa kukopa?
    Mheshimiwa Spika, kweli kama mnaipenda sana Tanzania kiasi cha kuhofia itazama kwenye madeni, kwanini hamtaki kupunguza marupurupu yenu mbali na ukubwa wa serikali hasa matumizi mabaya na ya kizembe kama utitiri wa wakubwa na namna wanavyohudumiwa bila kuwajali walipa kodi maskini tokana na mifumo ya hovyo tuliyorithi toka kwa wakoloni? Je mmeona kuwa kutoza watu simu ndiyo jibu wakati kuna makampuni ya simu hata haya ya kubeti ambayo ni tajiri? Kwanini hamuyatozi hayo makampuni tajiri na kuwaacha maskini waendelee kuwabeba bila kuwatesa zaidi? Kwanini msitoze hata tozo au kodi hata taasisi za kidini ambazo viongozi wake wanajisifia na kuonyesha utajiri ambao hauna maelezo kiasi cha kuwa na viburi vya hata kuishambulia serikali?
        Mheshimiwa Spika, je wewe na mheshimiwa Rais nani zaidi katika kutoa maamuzi na kuyasimamia? Yeye anasema tutakopa; wewe unasema tuwatoze watumiaji wa simu kama nani na kwa mamlaka gani?  Kama vile anakukumbusha au tuseme kukujibu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alikaririwa akisema kuwa “hakuna nchi isiyokopa…. Hata nchi zilizoendelea zinakopa.” Katika kinachoonekana kama kujibizana baina yako na Rais ulikaririwa ukisema “pitisha tozo anayetaka asiye taka pitisha tozo, lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.” Huu ni ushauri wa maana. Kinachokosa maana ni eneo ambapo unataka kuweka tozo.
Mheshimiwa Spika, tumalizie. Ulikaririwa ukisema ““sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo nayo sawa waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo namna ya ku-run nchi (kuongoza nchi) hivi sasa deni letu ‘seventy trilioni’ (Sh70 trilioni). hivi nyinyi si wasomi ‘is that healthy’ (hiyo ni afya). Kuna siku nchi itapigwa mnada hii.” Hao watakaotolewa mwaka 2025 ni akina nani na nani atawatoa na nani atachukua nafasi yao? Unaposema hii namna ya kuongoza nchi kwa madeni na nchi inaweza kuuzwa unamaanisha nini wakati juzi juzi ulikuwa ukiupigia debe mradi wa Bagamoyo ambao Hayati Magufuli alisema hata chizi hawezi kuupitisha?Je nani ataiuza na nani atainunua kati ya anayekopa fedha za miradi na wanaohudumiwa tena wengine bila kufanya hata lolote zaidi ya kula kwa mikono na miguu?
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: