The Chant of Savant

Thursday 6 January 2022

Barua ya Wazi kwa CCM:Msiwaendekeze Kijani wapingao ndani

Japo mimi si mwanachama wa chama chochote, bado ninavitazama vyama vyote kwa jicho sawa hasa ikizingatiwa kuwa ndivyo wenye dhamana ya kuongoza taifa letu pale chochote kinapopewa ridhaa na watanzania. Leo nawasiliana na CCM kwa mara ya kwanza. Sijawahi kuwa na ushabiki wa kuviandikia vyama au vikundi vya watu. Ila nikiangalia mambo yafuatayo, najikuta nikikiandikia chama tena tawala:
        Kwanza, CCM ni chama tawala ambacho kwa njia moja au nyingine kinanihusu kama mtanzania yeyote. Kwani, uwepo madarakani unagusa maslahi mapana ya taifa ukiachia ya chama. Hivyo, CCM si chama tu bali chama tawala kilichopewa madaraka na watanzania wengi kikaunda serikali na kukamata dola kwa niaba yao.
        Pili, nashangaa kunani watu wazima kuvuana nguo hadharani! Je ni kwa sababu gani na faida ya nani na kwanini? Je kuna bifu baina ya wakubwa wa chama au kuna kitu kimepungua au kinakwenda ndivyo sivyo? Kwa wanaojua namna CCM mnavyofanya mambo yenu kwa mshikamano wa pamoja, inashangaza sana. Pia, hii ni hatari kwa chama ukiachia mbali aibu na hatari.
        Tatu, naangalia hata kile kinachowagombanisha ambacho kiko wazi hasa mkirejea mipango na sera zenu kwa makini. Je, kama alivyosema Mheshimiwa Rais, hiki kinachowakuta ndiyo siasa za kuelekea mwaka 2025? Je ili iweje na kwanini? Haraka ya nini? Je huu ndiyo utaratibu wenu?
        Nne, najaribu kuangalia madhara yanayoweza kutokana na mnyukano wenu kama chama tawala hasa linapokuja suala la uendeshaji wa taifa letu hasa kiuchumi. Mheshimiwa Rais–––ambaye ndiye mkuu wa mhimili wa utawala na mwenye mamlaka makubwa kuliko wengine na Mwenyekiti wa CCM–––hivi karibuni aliingia kwenye mtiafuano na mkuu wa mhimili wa Bunge Mheshimiwa Job Ndugai aliyetahadharisha watanzania na dunia kuwa nchi itapigwa mnada tokana na kukopa.              Wakati Ndugai akipinga kukopa, Mheshimwa Rais anasema Tanzania itakopa kwa vile haikopi kwenda kufuja bali kuwekeza kwenye maendeleo tena kwa mikopo isiyo na riba. Nani anapenda nchi yake iuzwe? Je Ndugai alipitiwa au kuna kitu nyuma ya pazia kuelekea 2025? Je Ndugai ni wa kupuuza, kuadhibu au kusikiliza? Je inawezekana Ndugui akasikilizwa na kueleweka akiwa ndani ya chama kile kile anachopingana na serikali yake? Je hapa anangoja nini kufanya maamuzi magumu japo kulinda heshima yake na kuonyesha kuwa alimaanisha alichosema?
        Tano, nikiangalia namna Ndugai alivyo’omba’ kinachoitwa msamaha bila kukanusha madai yake ya kupinga kukopakopa na kupiga nchi mnada, naona kama kuna zaidi ya kile waingereza huita more than meets the eye. Je sasa nini mfanye? Nadhani kama chama kikongwe na tawala, fanyeni maamuzi magumu tena haraka ili kulinda heshima yenu. Na hapa niseme wazi kuwa msimchukulie Ndugai hatua peke yake bali na wengine wote wanaokinzana na mipango na sera zenu. Wafukuzeni uanachama baada ya kuwaita wajitete na kusikiliza mashiko ya hoja na madai yao. Mfano, Ndugai, kwa kukinzana na Mwenyekiti wa chama chake, amepoteza udhu wa kukiwakilisha chama chake kwenye mhimili husika kama kilivyoaminiwa na wapiga kura wa Tanzania.              Hivyo, ningekuwa mimi, ningeishapeleka barua kwa katibu wa Bunge kuanzisha mchakato wa kumtafuta wa kufanya kazi ya uspika. Ndugai akifanya hivi, hatajisaidia yeye kubaki na heshima yake tu bali hata chama na mhimili wa Bunge. Hata huu mchezo unaoendelea wa kumshambulia Ndugai hauna afya wala tija kwa chama. Bila kufanya maamuzi magumu, mtaendelea kushambuliana na kuvuana nguo hadharani kwa hasara na hatari yenu baadaye. Lazima muonyesha uongozi hapa. 
        Sita, suala la Ndugai ni fursa kwa CCM kuwashuhgulikia wote wanaopayukapayuka huku wakiendelea kuwa ndani ya chama au kuwa wabunge chini ya tiketi ya chama. Mfano, Josephat Gwajima (Kawe), Jerru Silaa (Ukonga) na Humphrey Polepole (Kuteuliwa) ambao wamekuwa wakionyesha wazi kukinzana na mipango, misimamo na sera za chama hasa kuhusiana na namna ya kupambana na Uviko-19. Kama watanzania wengine, wote wanaotajwa hapo juu, wana uhuru wa kutoa maoni yao lakini hawana haki ya kupinga mipango, misimamo na sera za chama chao kinachoongoza nchi wakabaki na uhalali wa kuendelea kuwa ndani ya chama wanachokipinga. Wanapaswa wajiondoe au kuondolewa ili waendelee kuhubiri na kutetea kile wanachokiamini kama kweli wana kiamini na kina mashiko kwao na wengine.
        Saba, najikumbusha historia ya matukio kama haya ndani ya CCM. Hebu jikumbushe kilichotuma Waziri Mkuu wa zamani mzee John Malecela kujiuzulu. Pale aliposhindwa kutetea sera ya CCM ya Muungano mbali na kumshauri vibaya Mheshimiwa Rais kuhusiana na kujiunga na Jumuia ya Nchi za Kiislam (OIC), aliambiwa arejeshe kadi au aachie ngazi na Hayati Baba wa Taifa, Mwl Julius Nyerere na akaachia ngazi kulinda heshima yake na ya chama jambo wanalopaswa kufanya wahusika hapo juu. Wakiendelea kutaka kula huku na kule, wafukuzeni uanachama nyadhifa zao zitayeyuka zenyewe.
        Tumalizie. Ili kutoa onyo kwa wengine wanaotaka kula huku n akule, watimueni haraka sana ili wanaojiandaa kuthubutu washike adabu mbali na kujenga utamaduni wa watu kuwajibika kwa matamshi na misimamo yao na kile wanachoamini. Hakuna awezaye kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Pia, tumshauri Mwenyekiti akunjue makucha yake na kuparura ili wale wanaotaka kumhujumu washike adabu. Kama alivyoahidi kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri ili kuwaweka huru wanaohangaika na 2025, awaruhusu pia wanachama wanaoanza kuhangaishwa na 2025. Kwani –––tukitafsiri maneno ya kimombo–––huwezi kuoka mkate wako na ukaula mwenyewe. Pia, mshika mbili lazima moja imponyoke atake asitake. Isitoshe, hawa ni watu wazima wenye akili na maamuzi ya kiutu uzima wanaopaswa kufanya maamuzi magumu na ya kiutu uzima. Ila kama watashindwa kufanya hivyo, si vibaya chama kikawasaidia kufanya maamuzi haya tena mapema hata kabla ya 2025.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: