The Chant of Savant

Tuesday 4 January 2022

Janga la Ukovi-19 Litufumbue Macho

Mwaka 2019, dunia iliamkia kwenye mstuko pale, kwa mara ya kwanza, ilipotangaziwa kuwa kulikuwa na janga liitwalo Ukovi-19 au Corona Virus-19 tokana na mwaka wa ‘ugunduzi’ wa janga hili. Wengi ambao hatukuujua mji wa Wuhan China–––ambao unaaminika kuwa kitovu balaa hili–––tulianza kuutafuta kwenye mitandao lau tujue kunani hasa pale Rais wa zamani wa Marekani mbaguzi Donald Trump aliposema gonjwa hili lilikuwa limetengenezwa kwenye maabara ima kama silaha ya kibailojia au kutokea makosa gonjwa likatoka nje. Dunia ilitetemeka. Ila taratibu, ilianza kuzoea hasa pale bara la Afrika liliposimama imara kuliko mabara yote na kutotetemeka. Hii ni kutokana na vifo vingi vilivyotokea kwenye nchi za magharibi zinazojidai kuwa na huduma bora na ujuzi wa hali ya juu vya kuhimili kila tishio. Hata hivyo, Ukovi-19 imetikisa ‘miamba’ hii ya kila kitu isipokuwa umaskini japo ndiyo chanzo chake kwa wengine.  Kwa wale wasiojua nini chanzo cha nchi za Magharibi kuumia sana, kuna hisia kuwa miili ya wenzetu siyo imara kama yetu mbali na mazingira waishiyo ukiachia mbali kuwa na idadi kubwa ya wazee wanaopata huduma mbovu. Hili tuliache.
Sasa ngoja tuzame kwenye ubaguzi wa kimfumo kimataifa wa Ukovi-19 kama kiashiria cha mfumo mzima. Ukovi-19–––huwezi kuamini––––ilipogundulika kwao, wachina walianza kutafuta jinsi ya kuunganisha janga hili na bara la Afrika. Mara wapo wabaguzi waliosema eti gonjwa hili lilitokana na popo aliyetokea Afrika kana kwamba Uchina hakuna popo wakati wako wengi tu. Hata hivyo, sayansi ilikataa. Sambamba na kutafuta namna ya kusukumia Afrika upuuzi wao, waswahili waliokuwa wakiishi China na India walianza kubaguliwa wakituhumiwa kuwa wana Ukovi-19 kana kwamba wao ni popo au wala popo kama wachina! Mungu si Athuman. Wakati waasia wakiwabugua Waafrika, huku Amerika, walianza kubaguliwa huku Ukovi-19 ukiitwa gonjwa la waasia. Walilalamika sana wakisahau; nao walijaribu kuwabagua na kuwazushia Waafrika. Hii ni ngwe ya kwanza ya ubaguzi wa kimfumo wa hovyo wa kimataifa unaotawala dunia kwa kukandamiza wengi hasa Waafrika.
Ngwe ya pili ya ubaguzi ilijitokeza na kujionyesha wazi pale kirusi cha Ukovi-19 kiitwacho delta kilipogunduliwa nchini Marekani. Pamoja na kuwa tishio kuliko virusi vyote vya Ukovi-19, dunia ilitahadharishwa lakini bila kuitenga Marekani kwa kiwango tutakachoona baada kugunduliwa kwa kirusi kingine kisicho na madhara. Makubwa kama delta kiitwacho Omicron–––kilichogunduliwa huko Afrika Kusini na kufanya nchi hii na majirani zake kutengwa mara moja na ‘wenye stahiki ya kuishi’ yaani mataifa ya magharibi hata ya mashariki ya kati. Kweli Mungu si Athuman. Baada ya nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani kupiga kelele juu ya Omicron na tishio lake, iligundulika kuwa kumbe kirusi chenyewe si hatari kama delta ya iliyogunduliwa Marekani. Je hapa hatari ilitokana na virusi au vilipogunduliwa? Inakuwaje kile cha hatari kilichogunduliwa Marekani kikaonekana kinahimilika kuliko kile ambacho si hatari cha Omicron?
Mungu si Athuman. Baada ya kugundulika Omicron, tuliambiwa tuanze kujiandaa kupata booster–––chanjo ya tatu–––bila kujali kuwa wengine hawajapata hata moja. Hata hivyo, tunashukuru. Wanasayansi–––tena wa huko huko magharibi–––wanasema hatuna haja ya kupata chanjo ya tatu.  Kwani, Omicron si tishio kama delta. Je iliuwaje delta haikutulazimisha kupata chanjo ya tatu au makampuni kuanza kutangaza yana kinga mpya dhidi yake? Hapa unaweza kujiuliza. Kama kweli Omicron imegunduliwa jana, hizi dawa walitengeneza lini kama hakuna namna? Je kweli kuna kinga ya Omicron au wahusika wanataka kupiga fedha hapa? Je walijuaje kuwa itakuja Omicron au ni uzushi au waliitengeneza? Je hawa hachochei uwepo wa nadharia njama? 
Mwanzoni, tuliambiwa Omicron ni balaa kweli kweli tukakubali na kutishika. Sasa tunaambiwa kuwa kumbe ni cha mtoto ikilinganishwa na delta. Je huu siyo ubabaishaji unaosababisha wengi–––hasa Afrika–––kushuku kuna namna hata kama wanafanya hivyo kwa kukosa hoja zinazojisimamia kama nilivyosikia ‘askofu’ wa kujipachika anayepinga chanjo akipayuka bila hoja za mashiko? Maswali mengine unayoweza kujiuliza ni: je kwanini Afrika inaendelea kuwa na waathirika wachache ikilinganishwa na nchi tajiri yenye fedha, mifumo bora na kuchanja watu wengi? Je ni kutokana na kuwa na kinga ya asili ambayo imewezesha Waafrika kunusurika majanga kama vile Ebola na Ukimwi hata pale dunia iliponyamaza ili waangamie wasiangamie? Je ni kutokana na mazingira safi ikilinganishwa na nchi tajiri? Je ni lishe ya asili wanayotumia Waafrika? Je ni aina ya maisha ambayo huwalazimisha kufanya mazoezi bila kujua kiasi cha kuwa na miili yenye kinga imara? Je hii ni neema ya umaskini ikilinganishwa na laana ya utajiri? Je ni mipango ya Mungu au miungu yetu?
Tumalizie kwa kusema wazi kuwa hata wale tulioaminishwa kuwa wanaweza kila kitu, ni uongo wa kujikweza ili waendelee kuwatawala wengine. Kwa tunaoishi huku, siyo siri, tofauti ni mazingira na rangi na kipato. Lakini inapokuja kwenye udhaifu wa binadamu, hakuna tofauti. Mfano, wengi hawajui kuwa Afrika ina nchi zaidi ya 50 pamoja na wao kuchora ramani ya dunia. Wanadhani Afrika ni nchi moja. Pia wengi wanatapeliwa kwa kuchangishwa fedha eti za kusaidia Waafrika wote ambao–––kwa macho ya wajinga wa huku––––ni maskini, wajinga, wagonjwa na wasiojua kitu chochote ila shida wakati si kweli. Mfano, kwa sasa miji mingi ya Kiafrika inaanza kuwa kama ya kichina kwa kuwa ya kisasa ikilinganishwa na ya huku ukiachia mbali chumi nyingi za Kiafrika kufanya vizuri. Huu ni ushahidi na motisha kuwa kama–––kama tutajitambua na kujiamini–––Waafrika tunaweza kufika mbali bila msaada wa yeyote. Mbona tuliweza kuishi bila kuwategemea kabla hawajatuvamia, kutuhadaa, kututapeli na kutawala?  Ubabaishaji, ubaguzi na utapeli katika Ukovi-19 utufumbue macho.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: