The Chant of Savant

Thursday 17 March 2022

Barua kwa Hayati Dk John Pombe Magufuli

Mpendwa Hayati Dk John Magufuli,
Sikuwahi kukuandikia barua ulipo kuwa nasi. Hata hivyo, japo kimwili uliondoka mwaka mmoja uliopita, kiroho bado tuko nawe. Matendo yako bado yanakuwakilisha, yanaongea na kutufariji kwa ukiwa uliotuachia ukiachia mbali pengo kubwa. Kwa muda ambao hukuwepo, naomba nitumie barua hii kukuhabarisha na kukujuza hali ya mambo japo kwa ufupi. Hivyo, unaposoma barua hii naomba nikujuze yafuatayo:
            Mosi, Makamu wako Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alichukua nafasi yako kwa mujibu wa katiba. Kimsingi, Samia hakuchukua nafasi tu bali anaanza kutosha kwenye viatu vikubwa ulivyoacha. Mwanzoni, kulitokea ukakasi kwa baadhi ya watu ambao hawakuamini kuwa mwanamke angeweza kuwa Rais achilia mbali kutosha kwenye viatu vyako vikubwa. Hata hivyo, naomba nikutoe wasi wasi. Mama anaendelea kuenea kwenye viatu vyako barabara.
            Pili, pamoja na kuchukua nafasi yako, mrithi wako ameendeleza mema yote uliyoacha ukiachia kufanya mabadiriko na marekebisho kidogo ambayo ni mambo ya kawaida kiutawala. Mfano, miradi yote mikubwa ya maendeleo bado inaendelea kwa kasi ya kuridhisha. Mbali na hilo, kwa mara ya kwanza, Tanzania tumeweza kuwauzia bidhaa nyingi kuliko wanazotuuzia. Hii mana yake ni kwamba uchumi wa viwanda unawezekana inaanza kutimia tena haraka sana. Tunakukumbuka na kukushukuru sana kwa kazi pevu uliyofanya. Kila tunapokwenda tunaheshimika kweli kweli kutokana na rekodi na uchapakazi wako.
            Tatu, mbali na kuendeleza miradi kwa kasi ya kutosha, Mheshimiwa Rais alibadili kauli mbiu yako kidogo. Hata bajeti mwaka huu imepanda kutoka Sh36.66 trilioni hadi kufikia Sh37.98 trilioni ili kuwezesha miradi kuendelea kwa kasi inayotakiwa. Badala ya “Hapa Kazi tu”, aliinogesha kwa kuja na “Kazi Iendelee” akimaanisha kazi pevu uliyoasisi na kuacha isikwame wala kukwamishwa. Cha mno, alipunguza ukali kidogo kwenye baadhi ya masuala kama kuongea na wapinzani. Hata hivyo, hii haikuja kirahisi. Una habari kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisoteshwa ndani kwa takriban miezi minane baada a kufunguliwa kesi uchwara ya ugaidi. Kama siyo viongozi wa dini kuingilia kati mbona angeumia zaidi.  Kwa vile mrithi wako ni msikivu kama wewe na ameendelea kuwaheshimu viongozi wa dini wa kweli (si matapeli wanaojifanya kutenda miujiza wakati ni utapeli na wizi) aliwasikiliza walipomuomba amfutie kesi Mbowe. Na baada ya kufanya hivyo, siku moja aliaachiwa na wawili walikutana ikulu na kupiga picha za pamoja na kutuaminisha kuwa sasa wako pamoja. Tunangoja kuona matokeo zaidi.
        Nne, suala la uwajibikaji limeendelezwa japo ukali wa kutumbua siyo kama wako. Anayetumbua sana ni Dk Hussein Mwinyi ambaye unajua kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa sasa. Naamini baada ya kusoma barua hii ya kumbukizi, Mheshimiwa Rais ataongeza kasi ya kutumbua. Pia, nichukue fursa hii kukupa habari mbaya kidogo. Unakumbuka baadhi ya mafisadi uliokuwa umesweka ndani kama wale walanguaji wa umeme wa AIPTIELO? Wote washaachiwa. Wako wanatumbua chumo la wizi,. Hata hatujui vigezo vilivyotumika kuwaachia. Mbali ya kushangaa na kuudhika, sijui undani wa kuachiwa kwao.
        Tano, nadhani unakumbuka kadhia ya Ukovi-19. Kumbe ulikuwa unajua mengi ambayo hatukujua. Kwa taarifa yako ni kwamba nchi nyingi sasa zimelegeza masharti baada ya kuja na kile wanachoitwa kwa kimombo tough it out. Ulipotoka watu waliachana na kujifukiza wakaelekea kwenye chanjo na kuvaa barakoa ambazo, hata hivyo, huku Ulaya tutaachana nazo siku mbili kuanzia leo. Huu ni ushahidi kuwa utabiri wako kuwa miili yetu itazoea ulikuwa wa kisayansi na kweli japo wajinga wengi hawakukuelewa. Wazungu wana mizungu. Ndo maana hukuwaamini. Unaweza kuamini kuwa kuna vita inaendelea kati ya Urusi na Ukraine ambayo imefunika Ukovi-19? Basi kaka, vita ilipoanza waswahili walibaguliwa katika harakati za kuokoa maisha yao sina mfano. Ungekuwapo ungesema kitu bila shaka. Ajabu waukraine waliokwama huko Kenya wanalala na kula bure bila hata kulazimishwa waende UNHCR. Tumeonyeshwa kuwa watu weupe ni bora kuliko watu wote duniani na ubaguzi na dharau vya wazi.
        Mpendwa Dk Magufuli, najua ulipenda sana vijana kiasi cha kuwapa madaraka makubwa huku wengine wakikuangusha wazi wazi kama yule aliyekuwa akituhumiwa kughushi vyetu vya kidato cha nne uliyemminyia lakini ujuaji na ujinga wake ukamfanya apuuzie ushauri wako hadi ukamtupa nje. Yupo anahangaika kwa sasa. Juzi nilisikia akilalamika kuwa amedhulumiwa kiwanja huko Regent. Mpaka leo, sijajua alivyopata pesa kununua uwanja eneo aghali kama hilo wakati hata wewe hukuwa na kiwanja pale. Cha mnno, Mheshimiwa Rais, ameendelea kuwaamini vijana huku akiweka kando wazee. Marafiki zako kama vile profesa Palamagamba Kabudi na William Lukuvi si mawaziri tena.
        Kabla ya kusahau, ilitokea kasheshe hadi yule Spika wa Bunge uliyemauacha Job Ndugai akatemeshwa ulaji na naibu wake akaangukia. Si alimlaumu Rais kuwa anakopa na nchi ingepigwa mnada siku moja. Wacha azongwe hadi pale alipobwaga manyanga na kujikalia kimya. Siku hizi ni backbencher. Haonekani wala hasikiki tena. Kweli cheo ni dhamana na kila chenye mwanzo kina mwisho.
        Habari njema kwako ni kwamba rafiki yako Raila Amolo Odinga asipokuwa Rais wa Kenya basi Mungu hakumwandikia. Najua unajua kuwa aliingia maelewano na hasidi wake Uhuru Kenyatta ambaye juzi alitangaza wazi wazi kumuunga mkono kupeperusha bendera ya chama chake na vyama vingine kikikwemo cha Kenyatta dhidi ya makamu wake William Ruto ambaye tuhuma za ufisadi zitamuangusha bila shaka ukiachia mbali kuwa hana uzoefu sawa na Odinga. Kuhusu bi Mkubwa wako Janet na familia. Bado wapo ila ameandimika tokana na kuendelea kukuomboleza. Hata mama yako bado yupo japo sina taarifa zake za karibuni. Lakini naamini hali sim baya hata kama uzee hauna tiba.
Mpendwa John, nimalizie, kwa vile sijui kinachoendelea huko uliko, naona nisikuchoshe wala kukata usingizi wako. Kwa ufupi, kama Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Benjamin Mkapa na mashujaa wengine mliotangulia, tunakukumbuka na kuku-miss sana kipenzi na shujaa wetu uliyeonyesha namna ya kuendesha nchi kisayansi na kiuhakika.
Chanzo: Raia Mwema jana.

No comments: