How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 9 March 2022

Barua kwa Rais Samia na Mbowe, wenzake na Wapambe

Kwanza nikiri wazi. Kiakili, kisheria, na kulhali kesi ya ugaidi iliyokuwa ikiwakabili M/kiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu, haikuwa na umuhimu wala sababu–––kwa yeyote mwenye kujua sheria na kutenda haki.  Kimsingi, kesi hii ya kubambikiwa ilimpotezea muda na wenzake, ukiachia mbali kuchafua jina la Tanzania na kuonyesha shaka kubwa juu ya dhana nzima ya utawala bora. Pia, kesi hii ilionyesha namna sheria zetu na vyombo vya dola vinaweza kutumika kisiasa tena na wapambe wanaojipendekeza kwa viongozi wakuu waonekane wanafanya kazi vizuri. Cha mno, kesi hii ilionyesha wazi namna Tanzania ilivyo na demokrasia changa, feki au ya ajabu kama haitabadilishwa. Inakuwaje watu wasio na kesi ya kujibu wanasota bila dhamana kwa muda mrefu hivi tuseme hii ni demokrasia na utawala bora na wa haki? Unashangaa mtu kama Mbowe na wenzake wanafunguliwa mashtaka yasiyo na dhamana wakati wapayukaji wanaopinga wazi wazi sera za chama chao wakiachiwa kwa vile siyo wapinzani wala tishio kwa ulaji. Kwa ufupi, kesi ya Mbowe na wenzake wawili ina mambo mengi ambayo imeyafichua kama vile siasa za kubabaisha, kukomoana, na visasi ambazo Rais Samia Suluhu Hassan hana haja ya kuzikumbatia. Kwani, hazitamjenga zaidi ya kumbomboa kama siyo kumdhoofisha.

            Licha ya kumpongeza kwa kukubali kushindwa na kufanya maamuzi magumu, niseme wazi. Mheshimiwa Rais Samia ameishi kwa maana ya jina lake. Waswahili husema kuwa jina baya humuumiza mwenye nalo. Pia, mwenye jina zuri, humuokoa mwenye nalo. Waingereza husema: what’s in the name? Kunani kwenye jina?

            Leo kama mshauri asiye rasmi wa mheshimiwa Rais, nitajikita kwenye jina Samia. Nitajitahidi kadri nitakavyoweza. Japo siyo mtaalamu wa lugha ya kiarabu, neno Samia linamaanisha usikivu au msikivu. Chanzo cha jina Samia kinaweza kupatikana kwenye mstari usema Sami Allahu Liman Hamidah, Allah humsikia yeyote amsifuye (al-Bhukhari, Muslim). Neno hili husikika kila baada ya rukuu (sina Kiswahili chake hasa ikizingatiwa kuwa dini za kigeni zilitulazimisha kutumia misamiati na mantiki yake). Nisingependa kurudia mandhari yote ya salat japo ndivyo ilivyo. Hivyo, sami, bado linamaanisha kusikia. Sasa Samia, sijui ni kwa sababu ya jinsia akaitwa Samia. Je angekuwa mwanaume angeitwa Sami? Hili–––niwe mkweli–––sijui mantiki yake.

            Nirejee kwenye kesi ya Mbowe na wenzake. Kwanza, niseme wazi, sina nia ya kuwatetea wahusika hasa ikizingatiwa kuwa mie sifungamani na yeyote katika siasa za nchi yetu ukiachia mbali kuwa magazeti ya Mbowe (mkewe) yalinidhulumu fedha zangu. Naandika haya kama mchambuzi na mwanafunzi wa mambo ya kidunia.  Kama nilivyodurusu hapo juu, kesi hii haikuwa na uhalali kiakili na kisheria.  Ni upotezaji muda na ukatili utokanao na ujinga na visasi visiweza kulisaidia taifa hata waliofanya hivyo binafsi. Mbowe na wenzake wamesota ndani. Je watesi wake wamepata nini zaidi ya aibu na dhambi?

            Nampongeza mheshimiwa Rais kwa kutokuwa kipofu. Kwanza, kama mke wa mtu anajua madhara ya mume kutokuwa nyumbani kwake. Kama binadamu, anajua madhara yampatayo binadamu anafungwa tena bila kuwa na hatia. Hili halihitaji majaribio ya kufungwa ndiposa mtu ajue madhira ya kadhia hii. Ukitaka kujua anachopitia mheshimiwa Rais, jiulize, angekuwa yeye ndiye Mbowe au mume/mkewe Mbowe na wenzake, angejisikiaje?

            Kwa wapambe waliosababisha uvujaji huu wa haki na sheria, badala ya kushanglia mateso ya wenzenu. Fanyeni tafakuri japo kiduchu. Ungekuwa wewe au nduguyo ungetaka atenzwe au utenzwe vipi? Kwa kitendo cha mheshimiwa Rais kumkaribisha Mbowe ikulu kutetea naye, ni juhudi na njia sahihi katika kuelekea usuluhisho wa kweli. Mheshimwa Rais Sami anamhitaji Mbowe na Mbowe anamhitaji mheshimiwa Rais. Tanzania ni kubwa kuliko wao na wao wanaihitaji wao hata kama Tanzania haiwahitaji hasa ikizingatiwa kuwa viongozi wanapita lakini taifa lipo siku zote.

            Je tunajifunza nini? Mosi, tunajifunza kuwa sheria zetu zinatumika ndivyo sivyo. Pili, kuwa wanasiasa na viongozi wa kiroho wana nguvu kuliko wanasheria. Rejea namna viongozi wa dini walivyomuomba Rais kufuta kesi na baada ya siku moja ikafutwa. Tatu, tunajifunza kuwa upinzani nchi, licha ya kutotendewa haki, una safari ndefu. Nne, tunajifunza kuwa kuta za gereza haziwezi kuponda na kushinda nafsi na nia ya binadamu aliyedhamiria kufanya jambo analoamini. Tano, mheshimiwa Rais Samia ni msikivu anayekubali kukosolewa ukiachia mbali kutopenda kutukuzwa. Niliwahi kumuonya asiwakilize wanaopenda kumuita mama yao hata wengine wazee kuliko yeye wakimdanganya na kumzeesha ukichia mbali kumfanya atende dhambi ya kutukuzwa. Namshukuru kuwa amesema wazi hapendi kutukuzwa. Natamani aseme pia kuwa hapendi kuonea wala kulipiza visasi. Nafasi za kisiasa zina mwisho ila utanzania na utu havina mwisho hata wahusika tukifa. Vitakuwaje na mwisho wakati tunaacha vizazi vyetu tupotoweka?

            Leo sisemi mengi. Nawapongeza Mbowe ambaye jina lake Freeman, linamaanisha mtu aliye huru kwa kuonyesha kuwa kweli yuko huru na hana kinyongo hadi akakubali kukutana na yule ambaye serikali yake ilimfunga bila sababu tena wazi wazi na siyo kisirisiri. Pia, nampongeza mheshimiwa Rais kwa kujishusha na kutafuta suluhu hata baina yake na wale ambao anaweza kuwafunga hata bila sababu kisheria. Hivyo, nimalizie kwa kuwataka wahusika na watanzania kuanza ngwe mpya ya maelewano na mshirikiano ili kujenga Tanzania yetu. Kwa wapambe, acheni ujinga na ukatili. Kuna kesho. Nyinyi mtapita lakini Tanzania haitapita hadi dahari. Bwana Mbowe na wenzako, msamehe mheshimiwa Rais. Kwa mheshimiwa Rais, nawe wasamehe Mbowe na wenzake hata wale waliowatia majaribuni. Namuonea huruma classmate wangu Sylvester Mwakitalu. Hata hivyo, si vibaya, sisi kama waja na viumbe dhaifu, hujifunza tokana na makosa yetu hata ya wengine kama tutakuwa tayari kujifunza.

Chanzo: Raia Mwema.

No comments: