Bila shaka wengi–––hasa watumiaji wa mitandao–––wameona picha kibao zikionyesha watu weusi walivyobaguliwa nchini Ukraine wakati–––sawa na watu wengine–––– wakijaribu kuokoa maisha yao baada ya Urusi kuivamia Ukraine hivi karibuni. Vita haina macho. Hata hivyo, hii ya sasa inayoendelea nchini Ukraine ina macho. Inajua rangi bora na dhaifu. Nani angeamini kuwa watu wanaoiingizia nchi mabilioni ya fedha kwa kwenda kusomea kule wangebaguliwa kiasi hiki? Ilitokea.
Makala hii haitaongelea vita hii ya kikoloni ambapo taifa la Urusi limetunisha misuli yake kutaka kurejea zama zake za vita baridi pale lilipokuwa limesimama uso kwa uso na Marekani kabla ya kuingizwa mkenge na kuvunjwa mwaka 1992. Badala yake tutaongelea tulichoshuhudia ambapo askari wa Ukraine na walinzi wa mpaka wa Poland walipoonyesha dharau na ubaguzi wa wazi dhidi ya waafrika. Nani alijua kuwa polisi au walinzi wa mipaka walioapa kulinda watu na mali zao wangewazuia wanafunzi wa kiafrika waliokuwa wakisoma Ukraine kupanda mabasi au treni au kuvuka mpaka kuokoa maisha yao kisa si weupe? Je haya yangefanywa na waafrika dhidi ya wazungu dunia ingakaa kimya kama ilivyofanya? Je hii inatoa somo gani kwa waafrika?
Hakuna picha inaumiza kama ile inayoonyesha mama mmoja wa kiafrika akiwa na kichanga chake akikataliwa kuingia kwenye kambi ya wanawake na watoto utadhani alikuwa mwanaume au mnyama. Nyingine inamwonyesha binti mmoja aliyekuwa akijaribu kuingia kwenye treni lakini akakatiliwa huku binti wa kizungu akiruhusiwa toka nyuma yake. Kosa la huyu nini? Weusi wa ngozi yake. Na yule aliyependelewa nyenzo yake nini? Weupe wake. Halafu watu hawa bado wanajiita au kuitwa wakristo au waislamu?
Tukiwa wakweli kwetu binafsi, matukio na tabia hizo juu zinaonyesha au kusema nini juu ya Afrika na waafrika? Majibu ni kwamba zinasema na kuonyesha yafuatayo:
Mosi, ubaguzi ulioonyeshwa wazi hapo juu unaonyesha kuwa watu weupe hawawathamini waafrika kama binadamu ndiyo maana wanabagua bila kificho japo hata wapo wengine kama waarabu, wachina, wafilipino na wahindi japo si wote wanawabugua ukiachia mbali wao kwa wao kubaguana. Nani asiyejua kuwa hata yale mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda yalisababishwa na ubaguzi baina ya waafrika kwa waafrika baada ya kulishwa upuuzi na wazungu waliotawala taifa lile? Nani hajui kuwa watusi waliaminishwa kuwa wao ni bora kuliko wahutu wakati wote ni sawa na wanabaguliwa na wabuguzi wote? Nani hajui kuwa baadhi ya jamii za kiafrika kama vile waethiopia, wasomali hata wasudani wanabagua waswahili wengine kwa sababu za kijinga na kipumbavu na wanaobaguliwa wanona ni sawa?
Pili, kitu kingine kilichojitokeza ni kwamba waafrika sisi kwa sisi hatuthaminiani na tunarahisisha ubaguzi dhidi yetu. Nani alidhani umoja wa Muungano wa Afrika na nchi za kiafrika vingekaa kimya hata baada ya watu wake kubaguliwa? Ajabu, wakati waswahili wakibaguliwa wazi wazi kulikuwa na mataifa vikaragosi ya kiafrika yakiahanikiza kuilaani Urusi huku mengine yakiulizwa ni kwanini hayajafanya hivyo. Hata wale waalimu wa haki za binadamu na usawa kama vile Umoja wa Mataifa hawakuona huu ubaguzi wa wazi wazi. Umoja wa Ulaya ulikana kabisa kuwa kilichofanyika Ukraine si ubaguzi bali uzalendo!
Tatu, kutokujali kwa AU na nchi za kiafrika ukiachia chache zilizolaani kitendo hiki ni ushahidi kuwa waafrika nao ni washirika wa ubaguzi dhidi yao. Hatubaguani kwa makabila yetu, dini na hata tutokako? Je hii inatusaidia nini? Je hatushirikiani na wabaguzi wengine miongoni mwetu ambao si waafrika wanaotubagua na kuwatesa wenzetu nasi tukajifanya kuwa si kazi yetu? Niliwahi kulalamikia ubaguzi wa waafrika waitwao Jarawa waishio kwenye kisiwa cha Andaman huko India wanavyotenzwa kama wanyama. Hakuna aliyejitokeza hata kufuatilia wala kukaripia! Nani amesahau jinai iliyotokea miaka mitatu iliyopita ambapo waswahili walikuwa wakiuzwa utumwani kwenye nchi za Libya, Tunisia, Mauritania na nyingine tena na waafrika wa kiarabu na AU haikuchukua hatua? Nani amesahau dada zetu wanaodhalilishwa, kunyonywa hata kuuawa Mashariki ya Kati na hakuna anayelaani zaidi ya kukaribisha wawekezaji hawa wabaguzi na kujiuza kama waafrika? Nani hajui kuwa ndugu zetu toka Ethiopia waliohadaiwa wakahamia Israel eti ni wayahudi al maarufu Mafalasha kama huku wakinana uafrika wao wanavyobaguliwa sasa huko? Je hapa tatizo ni ujinga, roho mbaya au kutojijali na kujaliana ukiachia mbali kujikana na kutojithamini na ili iweje au tupate nini zaidi ya kuchangia kwenye kuagamia kwetu kama jamii ya watu japo wa hovyo kwa tabia hizi? Kwa wale wanaoishi kwenye miji mingi ya Tanzania wanajua namna ubaguzi wa rangi unaofanywa na ndugu zetu walioletwa na wakoloni umehalalishwa kwa kuwaruhusu waishe kama wako kisiwani zaidi ya kushirikiana kwenye biashara.
Tukirejea Ukraine, hata kitendo cha waafrika kuzuiliwa kuingia ulaya huku waukraine u mipaka yote na kupewa kila huduma ni ushahidi wa ubaguzi wa kimataifa dhidi ya Afrika na waafrika. Wakati ndugu zetu wakiangamia baharini wakikimbia vita wanaitwa wahamiaji haram una kuzuiliwa kuingia Umoja wa Ulaya, waukraine wamefunguliwa milango yote kwa sababu ni weupe. Je mataifa yetu yanajifunza nini hapa? Jibu ni rahisi ni kwamba kama hujipendi hutapendwa. Kama hujijali hakuna atakayekujali wala kama hujiheshimu au kujithamini hakuna atakaye kuheshimu au kukuthaminiana.
Sasa nini kifanyike? Yapo mengi ya kufanya. Nchi za kiafrika zisiruhu wanafunzi waliobaguliwa kurudi Ukraine. Watafutiwe vyuo nchi nyingine. Pia, zianze kufikiria kuanzisha vyuo kwa ushirikiano ili kuachana na utegemezi usio wa lazima. Mbali na haya, AU itoe tamko rasmi la kulaani ubaguzi na ikiwezekana isiwe na upande katika pande mbili zinazopigana kwa vile haina maslahi yoyote. Ikiwezekana zishinikize Ukraine iombe msamaha wazi wazi badala ya kutaka iuingwe mkono kwa vile inatetewa na wakubwa waliokuwa wakoloni wetu.
Mwisho, waafrika tuache kuendelea na upambavu tuliojazwa na wakoloni wa kubaguana kikabila, kidini na upuuzi mwingine. Tunapofanya hivi, tunawafaidi watesi wetu wanaotudharau kuliko hata mbwa. Kuna njia moja ya kuwakomboa waafrika ambayo ni kuunganisha nchi zao kwa kukataa mipaka na mataifa yaliyoundwa na wakoloni hawa hawa wanaotubagua wazi wazi. Kama tutaendelea na ubinafsi na upogo huu, tutaumia sana hasa ikizingatiwa kuwa tuko nyuma karibu kwa kila kitu. Mfano, India pekee ilikuwa na wanafunzi wengi wakisomea udaktari wapatao 23,000 huku nchi yenye wanafunzi wengi kule Nigeria ikiwa na wanafunzi wasiofikia. Hata 1,000. Je kweli tutashindwa kubaguliwa na kujipeka India kwa matibabu wakati tunao uwezo wa kujenga taasisi kama hizi nyumbani? Tafakarini.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment