The Chant of Savant

Wednesday 10 January 2024

Hatuhitaji siasa majitaka, uviwawa, na uchumiatumbo


Tangu Bi Mkubwa, almaarufu maza, afyatue kijibwa kiitwacho Chihuahua au Chiwawa kwa Waswahili aka pet, kayani hakukaliki. Nimefyatuliwa. Kijibwa chenyewe kinabwekabweka sina mfano! Kinabwekea hata jua. Ila kwa woga, sina hamu. Akiruka inzi, kinatoka mkuku! Kakipa majina mengi. Mara kiitwe Mwamba, Tamba, Gilo, Jerome, Stanley, Ray, Kiemenaa, mara Miki. Taabu tupu. Ameigiza utasha kuipa mimbwa majina ya mafyatu kuonyesha walivyo smart na wa maana kuliko hata mafyatu weusi wanaowabagua. Chiwawa kanibandua. Akirejea kazini, ni chiwawa, chiwawa naye. Tuyaache. Ila amejua kututenda na kututenza!
        Leo nafyatua siasa za majitaka, uchiwawa, na uchumiastomach. Juzi nilimsikia fyatu wa upingaji ulogeuka upigaji, Mzito (mvivu kifikra) Zobahili Kabwela akifyatuka kama chiwawa eti vyata vya siasa na visasi vipewe ruzuku 10% ya njuluku za ruzuku! Akili au matope? Thubutu! Tunawaruzukia nini? Are you serious or seriously mentally sick? Huu nao ni upigaji wa kisiasa. Ulisomea nini na wapi veve dugu yangu kumbaff sana? Eti mzawadiwe na kufyatua 10% kwa kupiga domo na fitina mfyatue nyumba ndogo na kupanua matumbo siyo! Kama zipo za kumwaga, wapeni wakulima, wafugaji, au wastaafu tuliowatufyatua na kuwafyatulia huu utamu mnaofyatua sasa tuliofyatuliwa na kuzeeka na kufa kabla ya wakati. Au wapeni mafyatu wote basi mnaowatoza kodi na tozo bila kuwaonyesha mtumiavyo mbali na kutanua.
            Zikiwazidieni, nipeni nianzishe runinga nifyatue ukweli bila woga, au wapeni matabibu na wazoa taka wanaotuepusha na magonjwa, au wajawazito wanaojifungulia barabarani, au wagonjwa wasioweza kulipia matibabu. Zikizidi, wagawieni mafyatu mliowafyatua kwa miaka nenda rudi badala ya kujenga vyama visivyo na faida ala!
        Acha nifundishe uchumi. Kaya yetu haiendelei siyo kwa sababu tu wavivu. La. Inakosa waongozaji wabunifu na wachapikazi kama mimi au Jiwe aliyeibadili kwa muda mfupi japo alikuwa na mauzauza yake, mfano Chatolite. Waijua? Kaulize Gbadolite kule DRC kwa jambazi Mobuti Seseseka aliyefilisi kaya naye akafilisika na kuzikwa kama dog. Wajua? Siri-kali ya kaya kapuku inayobomubomu inakuwa kubwa na wanene wanaofyatua njuluku wasifanye lolote la maana wakiwa chanzo cha ukapuku wetu kwa sababu:
         Mosi, wana longolongo. Hawafyatui kazi bali ngonjera, kusifiana, usanii, na maigizo kibao kama kutaka 10% ya bajeti iwe ruzuku. Hamtosheki!!!? Mikataba feki na hovyo 10%, kupata huduma kwa mafyatu yanayofyatua rushua 10%.
            Pili, zaidi, wanene wanasifika kwa matanuzi ya hovyo na ulimbakeni. Mfano, maza na wenzake wanakwea Dreamliner kwenda Mbea au Ng’waanza. Hasara kiasi gani drimulaina kugeuzwa nkokoteni au taxii? Bado utitiri wa pangu-pakavu-fyatua mchuzi wajazanao kwenye haya matanuzi mbali na usiri wa misafara ya wanene wakati wanatumia njuluku zetu. Badilikeni vinginevvyo tutafia kwenye umaskini wa kujifyatulia. Sanasana, mnaongeza deni la kaya na kushindwa kufyatua maelezo ya kina mkidai linahimilika. Inshu inayotufyatua ni kuhimilika au kuumka? Mzito Kabwela kaniudhi kama yule Mwegulu Mwehuu Nchembi aka Madilu wa kughushi anayejitiatia mchumi kumbe mchumiatumbo. Natamami PhDii na tasnifu yake aifichue tumsasambue madoktari origijinali wa economia. Akijitia kujibu, ajue, shahada zangu 13 nimesomea zote ughaibuni mbali na kuandika vitabu zaidi ya 100 vya ufyatuaji.
            Tatu, akina Mzito wafungwe kwa kutaka kuhujumu uchumi. China hawa hula shaba. Hatuli politiki bali chakula. Hiyo 10% wapewe wakulima wafyatuao chakula au walimu wafyatuao elimu. Simpo, bila mitobozano wala utata. Ikizidi wapewe wazazi wafyatuao vitegemezi vya kesho.
            Nne, kwa vile natoa suluhu sio Sami.. we..koma! Nashauri yafuatayo kwa Mzito na wafilisika wenzake:
        Mosi, wasipewe njuluku. Wakauze nyanya. Tufyatuliwe tozo, wapewe wauza maneno wasitotupa suluhu ya matatizo yetu?
        Pili, tufutilie mbali vyama vyao vya mifukoni vinavyotamani vikiondoe chata twawala wale  wao na siyo kufanya lolote la maana kwa mafyatu. Chata gani cha maana kina mkiti mmoja kwa miaka zaidi ya mia? Kwani wanachata wake wote ni mataahira?
        Tatu, wapimwe akili au kuhojiwa na Takokuru kwa uhujumu.
        Nne, vyata vitozwe kodi hata kwa mapato ya kuuza kadi au misaada watoayo washitiri wake sawa na matapeli wa kiroho waliojaa roho mtakakitu wanaowaibia mazwazwa wakiwaahidi miujiza wakati ni kuwaibia tu. Mafyatu hatuli siasa wala neno. Tunakula msosi wafyatuao wakulima.
        Tano, tumechoka na vyata vya kisanii. Amerikani, pamoja na ukwasi, wana vyata viwili. Sijui  tunavyo gizilioni ngapi?
Sita, 10% itumike kwenye maendeleo siyo politiki. Mahospitali na zahanati hazina dawa japo hawa mavuvuzela hawayaoni bali mitumbo yao! Shame on you!
        Mwisho, sie si vyura! Kila fyatu anautaka urahisi au ukiti wa chata ili kuchumia tumbo kwenye siasa za uchumiatumbo au chiwawa kama siyo majitaka. Mkitaka kufanya kweli, unganeni mtengeze chata nene likibandue chata twawala kilichochoka na kuchakaa kulihali hadi kinategemea vichiwawa, wasanii, na chawa wanaotushambulia, kutupotezea muda kufua, kujikuna, na kutujaza magonjwa tusiwafyatue wawafugao.
        Hivi nami nina Chata cha Mafyatu (CcM)? Napendekeza nipewa 50% ya pato la Tanzatozo ya Sa100. Nikipewa, nitampongeza kama sina akili nzuri.
Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: