The Chant of Savant

Wednesday 31 January 2024

Kumbe Mirirani Imefamilishwa kwa akina Riz One! na Nduguze Sasa


Katika kujimwambafy, kuwatapeli na kuwafyatua mafyatu, si chawa wa maza aitwaye David Albat Bashiti alitinga Mirerani ili kuwafyatua mafyatu waufyate na kuamini wana viongozi wanaowafaa wasijue sanaa. Kama kawaida ya mbwembwe na sanaa zake, alijifanya kuwa na uchungu na mafyatu kusikiliza matatizo ya mafyatu wakati naye ni tatizo tena jipu kubwa linalonuka tu. Huu uchungu kweli au uchangu wa kisiasa na uchuro? Huyu chawa mwenye cheo cha Katibua propaganda, uchawa, na urongo bila itikadi anaongea utadhani maza mwenyewe. Nashangaa si chata wala maza anayeona madhara wanayatengeneza kwa kutaka kutumia utapeli na kamera kujitia wanatatua matatizo ya mafyatu wakati si kweli. Chawa anajijenga kwa kuwabomoa wao japo anapoteza muda asijue wanaweza kumpoteza.

Akiwa anatazama kamera na kutabasamu apigwe picha na kuwafyatua mafyatu kuwa ana uchungu nao, si njemba moja ikamfyatua swali tata na gumu. Njemba ilieleza mgogoro kati ya kampuni moja aliyosema ni ya akina Riz One iliyowatimua wafanyakazi kinamna. Alitaja wazi kuwa kampuni hii yenye ubia na siri kali, ni mzuka kama si mzimu japo inamilikiwa na akina Riz One. Kuona hana la kujibu, alisema “wewe ungekuwa mimi ungefanyaje?” Kanywe poizoni au jinyongwe.

Kama huna la kufanya, kwanini kuwatapeli mafyatu kwa kujimwambafy kuwa unalenga kutatua matatizo yao? Hujui kuwa matatizo ya mafyatu ni nyinyi mnaowala na kupeana ulaji kwa kujuana kifamilia, kiukoo, na kichama kama wewe?

            Nadhani wote tunamjua Riz One ni nani. Ni kitegemezi cha Njaa Kaya. We! Koma. Hii si mara ya kwanza kutajwa kwenye ulafi na uoza ambapo kaya imefishwa na kuoza na kuwa mzoga kama wa tembo ambapo mainzi na mipanya na mipanyabuku tena michafu bila kunawa ikiurarua na kuutafuna kwa mikono na miguu wakivimbiwa kutapika, na kujisaidia humo. Wakati haya yote yakifanyika, wanatokea mafyatu wanaosema eti home kunogile wakati kunugulu (tafsiri muulize njomba). Kuna kunoga au kurogwa? Huyu kidhabu bingwa wa kula na kukufuru bado ana jeuri ya kuwatia mafyatu vidole machoni. Kama akina Kinjekitile Bokero Ngwale, Mtwa Mkwawa wa Mwinyigumba Mwamuyinga, Mtyera Kasanda Milambo, Nyungu ya Mawe, Isike hata mzee Mchonga Kambarage wa Burito wangefufuka, kama siyo kuchapa mafyatu bakora, huenda wangejinyonga kwa makufuru, ulafi, na uoza vinavyoendelea.

Ufamilia, uchawa, ukoo, upanya, na ufisadi wa kimfumo vilivyohalalishwa vinavyoendelea vingefanya mafyatu hawa wakongwe wajinyotoe roho. Hivi kama hakuna ukweli, inakuwaje majina ya vigogo yatajwe kwenye kila ufyatuaji na kaya iache kuitwa kaya ya famila au koo fulani? Inakuwaje wengi wa wanafyatua vyeo vya ulaji mnene ima wana majina manene au ni marafiki, ndugu, au jamaa za wanene au wenye majina manene? Je tukifyatuka na kudai kuwa hii kaya iitwe Wanene country ni matusi au uchokozi?

Mafyatu nasi ni wa kulaumiwa. Hivi unaposikia kuwa mfano Riz One na wenzake wana kampuni mzimu kama ilivyofyatuliwa huko Mirirani, unafyatua hatua gani? Je yapo makampuni mengi mengine kama haya hayajulikani au hayajavuliwa nguo? Je yana mitandao yake Mirirani tu au kaya nzima kila palipo na ulaji?  Je kaya imeishatiwa na itatiwa hasara kiasi gani tangu mchezo huu mchafu uanze na itapata hasara kiasi gani kama mafyatu wanaendelea kufyata na kuwa watazamaji utadhani hayawahusu?  

Niwaase akina Riz One na walafi wengine kama wao. Hata mngeuza kaya nzima

kapata njuluku kuliko akina Elon na Bill mnadhani mtaishi milele  wajalaana nyie?

awaulize vitegemezi wa akina nonihino waliofilisi NBC na kuibuka matajiri wa kunuka.

Si wamekufa na kucha kila kitu kikianza kusambaratika? Fyatu ni nani na ana nini

duniani kama siyo ukumbaff na tamaa za kikumbaff?

            Katika kudurusu na kufanyia uchambuzi wa kina shutuma dhidi ya akina Riz One kuwa na kampuni mzuka na kufanya biashara na siri kali ambayo nayo ni chafu, nimegundua yafuatayo:

Kwanza, kuna ukweli usiopingika. Kama sIvyo, wahusika wangejitokeza na kukanusha. Wanavyopenda sifa na kuonekana wema, naamini wasingeufyata bali kufyatuka lau ngonjera. Hata huyu chiwawa wao angejitahidi kufanya utetezi. Hapa naona, kuna mitandao ya ulaji inayochukiana na kutaka kumalizana. Chiwawa, inavyoonekana, hayumo kwenye mtandao wa akina Riz One. Kutokana na jibu la kukata tamaa alilotoa, ingawa hata hayo mengine anayotoa ni changa la macho na rongorongo, linasema kila kitu kuwa hali katika wizii huu si shwari baina ya majiziii.

            Pili, wenye hilo kampuni ni wanene pamoja na wanufaika wao. Maana, msemaji amesema wazi kuwa waziri Bitek siyo yule Okot wa Song of Lawino, alishindwa. Maza naye inasemekana ameshindwa. Je kweli maza kashindwa pamoja na mamlaka hayo yote, au naye anaogopa wanene wake asiwaguse pabaya kabla hata ya kufika twenty twenty-five au naye yumo? Je kama ameshindwa na jikampuni mzuka, ataiweza kaya kweli? Anaifaa kaya kweli au ni yale yale kuwa mnatoa mbovu moja mnaweka nyengine? Je nanyi mafyatu mmeshindwa wakati mtama ushamwagwa kwa kuku? Basi hapa bila mafyatu kuamua kutia guu, mtaliwa hadi mkome. Mie simo. Nani aliwe?

            Du! Nimesahau? Nimeandika eti kaya imefamilishwa kwa akina Riz One?

Soma taratibu wasisikie na usimwambie fyatu yoyote hata mshirika wako wa bedroom.

Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: