Niende kwenye inshu. Japo sina takwimu, yangefanyika mashindano ya vituko kikaya, kaya yetu ingeshika namba ya juu kwani huwa na vimbwanga, vituko, visa, na mikasa usipime. Naweza kuiita kaya ya mikasa hasa siasa zake. Juzi nilitumiwa clip ya video ikidau kuwa dini fulani inazuia wanawake kuwa viongozi!
Katika kudurusu kadhia hii, nitajikita kwenye mambo kadhaa. Mosi, kaya yetu haina dini wala jinsia ingawa wanakaya wanavyo vyote viwili na mengine kama hayo kama mali binafsi. Kwa sababu hizo, kaya yetu inaongozwa na katiba siyo misahafu ingawa wakati wa kuapishana huwa tunaitumia. Kisheria, bila kujali dini, jinsi, eneo, ukoo, na mengine kama hayo, kila mwanakaya awe mke au mme ana haki za kuiongoza ilmradi afuate katiba, kanuni, sheria, na taratibu. Kinachotakiwa ni kuwa na sifa husika kuwashawishi wapiga kura kumchagua au kutomchagua kulingana na malengo na matakwa yao ya pamoja kama jamii na kaya.
Kikatiba na mila tuliyojiwekea, rahis wetu ni rahisi, ni alama ya kaya, ni mtumishi wa kaya kinadharia hata kama kivitendo ni bosi na mkuu wetu mwenye madaraka makubwa kuliko sote tuliyompa kwa muda fulani. Kifalsafa na kisheria, rahis ni rahis. Si mwananke wala mwanaume japo ana jinsia haituhusu. Rahis wa kaya ya mafyatu si kiongozi wa dini bali wa kaya. Hivyo, sifa za kuwa kiongozi au rahis hazihitaji wala kufuata sifa za kidini.
Wakati tukitafakari haya, tujiulize. Nani hakuzaliwa, kulelewa, kufunzwa, kutunzwa na kukuzwa na mwanamke? Kama wanaume wako ni mali sana, kwanini usijizae au kudondoka toka mbinguni au kuota kama mti? Hata mti una mama. Kama wanaume wako ni dili, kwanini usiende ukaishi kwenye hiyo kaya ya ndotoni ya wanaume watupu uone mtakavyogeuziana mitutu. Kama mwanamke hafai kuwa kiongozi, mnaoa wa nini na inakuwaje tuamini kuwa kila mwanaume aliyefanikiwa, kuna wanawake wawili nyuma yake yaani mama yake na mkewe? Kumbaff kabisa. Mafyatu wazima mnashindwa jambo dogo kama hili ambalo hata inzi wanalifahamu uzuri? Msituletee bangi zenu tuvurugane mtuibie. Nenda Somaliya mkajifunze. Msitumie dini na udini uchwara kuhalalisha uchochezi, ujinsia, na ukumbaff. Kama mwanamke hafai hivi, kwanini huyo Mungu wenu alimuumba? Kama msingekuwa wachonganisha, wachovu, na wakumbaff, basi mngegomea vitu anavyofanya mwanake kama vile kupika, kubeba mimba, kuzaa, mbali na urodi anaotoa. Nyambaff zenu kabisa.
Je kuna uongozi wa msingi na muhimu kama huu? Kama tunataka kutenda haki, tumhukumu fyatu kwa tabia zake na si kwa jinsia wala atokako, umri, imani, wala mbari yake. Kaya haina haya mambo ijapokuwa wanakaya wanayo kama mambo binafsi yanayopoteza umuhimu linapokuja kwenye masuala ya pamoja. Hivyo, hawa wanaotaka kutuletea dini, udini, ujinsia, wakivichanganya na siasa, tuwazomee, tuwakemee, na ikibidi tuwaadhibu. Kama wana hoja au hata kutafuta kiki, basi wajitokeze. Wajenge hoja zao wakizingatia misingi na shuruti za katiba ya kaya tuwasikilize lau tupate nafasi ya kujadiliana nao. Vinginevyo, huu ni uchochezi, uchovu, ukale, na ukumbaff vilivyopindukia.
Hawa wakumbaff, kama ni wanaume kweli, walishawahi kujiuliza namna walivyopata huo uume wao? Je walituma maombi au kufanya na kushinda mtihani wa kuwa wanaume? Tupo kama tulivyo, pale tulipozaliwa, jinsia tuliyopewa, vipawa na uwezo tulivyo navyo hatujui ni kwanini tulipewa. Mifyatu mipuuzi na mikumbaff kama hii ilifaa iumbike mbu au hizi kama si chawa. Hivyo, wanaotaka kutumia falsafa na mawazo chonganishi na mfu, wasipewe nafasi katika kaya yetu.
Leo nina hasira. Ngoja niachie hapa nisije nikateka, kupoteza, na kunyotoa mafyatu wakumbaff roho. Hivi leo ni siku gani?