How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday 13 October 2024

Garagaring Mbinu Rahisi ya Kuula Kirahisi

Juzi nilikumbuka msemo kuwa wajumbe si mafyatu. Nikiwa najivinjari na kutafuta namna ya kufyatua njuluku au unene bila kuhangaishwa kuandika application au kutaja sifa za kufanya hivyo, niliwakumbuka wanafalsafa watatu. Hawa jamaa, kwa wakati tofauti, waligundua kuwa wanene wanapenda sifa na kuabudiwa. Hivyo, kama unatafuta cheo au njuluku toka kwao, wewe jishushe, garagara chini na kuwaramba miguu, watakupa utakacho bila kutoa jasho zaidi ya sanaa. Kifyatu, hii inaitwa garagaring au sanaa ya kuula kirahisi bila kujihangaisha au kuhagaishwa.
Katika kusoma saikolojia, nimegundua kuwa wenye power wanapenda sana kuliwazwa, kuduwazwa, hata kufyatuliwa kisanii. Unawapa wanachotaka, unapata unachotaka. Unakumbuka kisa cha mfalme zwazwa aliyehadaiwa na mganga wake kuwa akitoka uchi, atangudua namna wajoli wake wanavyomgwaya. Bila hata chembe ya aibu, mfalme aliwaita wajoli wake hekaluni akavua nguo zote na kuamuru atembezwe macherani ili aone wajoli wake watafanya nini.  Na kweli, amri ya mfalme ilitimizwa. Alibebwa uchi wa mnyama na kuzungushwa mbele ya kadamnasi akiwa mwenye furaha na mashawasha kujua nini kitatokea.
Kwa vile tabia ya wajoli ni ndiyo mzee au ndiyo mama, walianza kumshangilia kwa nguvu. Mfalme, bila kujua sanaa na unafiki wa wajoli alifurahi na kuamini alikuwa amevalia vazi la kupendeza asijue walikuwa wanamchora na kumuingiza kichaka ili wajaze matumbo yao. Ukiondoa Fyatu Mfyatuzi na watoto wachanga, nani angemwambia ukweli mfalme kuwa alikuwa uchi? Nani angemwambia wakati wengi waliomzunguka na kumsifia walikuwa ni wachumia tumbo waliokataa kutumia vichwa na ubongo wakaamua kutumia matumbo na utumbo? Nani angemwambia ukweli mchungu wakati alikuwa amezungukwa na wanafiki, wasanii, na wasasi wa ngawira wanaoweza kuuza utu wao ilimradi tonge liingie kinywani? Angeabiwa na nani wakati alikuwa amezungukwa na wanyonya damu kama chawa?
Ukiachia kisa cha mfalme juha, kuna kisa kingine. Baada ya watu wa kaya ya kombaland kujikuta hawana hakaki na majaliwa yao hasa wale waliokuwa wamepewa ulaji tokana na usanii wa kugaragara chini, waligundua kuwa bila kumsoma dingi na kujua apendacho, unaula wa chuya. Hivyo, walikuja na usanii mmoja. Kila walipomuona dingi, walianguka chini wengine kupiga magoti, wengine kusujudu, wengine kuita ‘baba baba’ kila fyatu lake ilmradi apate mradi wake. Kwa wanafalsafa kama mimi, kilichokuwa kikitokea ni utapeli ambapo mmoja hununua dhahabu feki kwa fedha feki wote wawili wakiamini wamempata mwenzao. Sasa nini faida za mchezo huu? Faida ya kwanza, ni kupata usichostahiki kwa kutumia mbinu zisizostahili. Faida ya pili, ni kupata dezo bila kuhenyeka japo kujigaragaza si kuhenyeka tu bali kujidhalilisha na yule unayemgaragaria.
Je nini hasara za usanii huu unaonuka? Kwanza, ni kupata stahiki bila ya stahiki. Pili, ni kwa mtoaji kuamini wasioaminika, kuwadhalilisha na hata kujidhalilisha bila kujua. Tatu, ni kujenga tabaka la wababaishaji, waganganjaa, na wasanii ambao ukwasi ukikutoka wanakutosa kimasomaso bila aibu kwa vile hawana aibu. Nne, ni kutopea katika udhalilishaji wa mafyatu japo nao wanajidhalilisha kwa kutumikia matumbo badala ya jamii.
Japo mbinu hii inaweza kuonekana rahisi, si rahisi. Maana, wahusika, kwanza lazima wajidanganye na kudanganyana. Pili, lazima wadhalilishane na kuhadaana. Waswahili husema kuwa hii ni sanaa ya kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa au kukumbatiana wakati mmeshika visu au mikuki. Tatu, ni kuibuka tabaka la kupe hata chawa wasiojiamini au kuaminika. Ukizungukwa na mafyatu, wasaidizi, au watumishi wa namna hii, licha ya wao kutojiamini, nawe huwezi kujiamini au kuwaamini. Maana, kila aliye na tonge yeye ni wao na asiye nalo si wao hata kama alikuwa wao jana. Viumbe wa namna hii ni kama chawa. Hawana kumbukumbu wala hisia zaidi ya hamu na nia ya kufyonza damu. Bila kunyonya, hawaishi. Na bila kunyonywa huwapati. Unaweza kuwapata, mwishowe watakupata udhani umewapata. Bwana Mkubwa Mwana wa Maria alipoingia Jerusalemu, alitandikiwa mitandio, vikoi, vitenge na matawi akiimbiwa kila nyimbo za sifa. Siku ya kusululubiwa ilipofika, hao hao waliomkweza, kumsifu na kumshangilia walikuwa wa kwanza kusema ‘asulubiwe asulubiwe.’ Na kweli alisulubiwa wakamuona mshamba!
Je inakuwaje fyatu mwenye akili na madaraka akaangukia mtego huu? Kwanza, lazima akubali kujirahisisha au kurahisishwa ili apatikane kirahisi. Pili, lazima apende au kuwa mlevi wa sifa hata zipatikane kwa njia haramu na zisizo na sifa kitu zaidi ya rongorongo. Pili, lazima ujidanganye ili wakudanganye. Tatu, lazima upende vitu vya rahisi rahisi ambavyo mwisho wake ni kukurahisishia maanguko yako. Tano, lazima ushindwe kujua kuwa unaodhani wanakupenda na kukuogopa hawakupendi bali kukuponda na kukudharau. Kuna mfalme mmoja alikuwa na wajoli aliowateua kuwa wasaidizi wake na kufanya kosa kuwaamini. Siku moja, shushu wake akipita kwenye kigwena chao, aliwasikia wakimnanga mfalme. Aliamua kuwarekodi na kumpeleke mfalme mpenda kuabudiwa. Mfalme hakuamini hadi anakufa kuwa kumbe rahisi inaweza kuwa aghali.
Tumalizie. Rahisi rahisi yaweza kuwa aghali na hatari. Hilo ndilo somo la leo. Hivi, ninaongelea nini?
Chanzo: Mimi.

No comments: