How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday 20 October 2024

Maisha, Ndoa, na Thamani Yake


Pamoja na ubunifu, ujasiri, usiri, na upekee wa binadamu, hakuna kitu chenye thamani na kinacho mhangaisha binadamu kama maisha yake ya kibinafsi na kijamii. Baada ya uhai, kinachofuatia ni ndoa hata kabla ya madaraka, ukwasi, umaarufu na usomi. Kila mtu anautaka ukwasi, umaarufu, na mafanikio hata kwa kudhulumu, kuumiza wengine hata kuvunja sheria. Wapo wanaowaibia wenzao hasa wafanyakazi wa umma wasio waaminifu, ili kufanikisha ndoa zao. Wapo wanaofikia hata kuhatarisha usalama wa ajira zao kwa sababu ya ndoa. Mfano, chukulia rais anayerubuniwa na mkewe kuwa fisadi. Au chukulia mtu anayeibia wengine ili kuwasomesha watoto wake au kumfurahisha mwenzi wake. Kwani haya hayapo? Chukulia mtu anayepata ajira anaamua kuwajaza ndugu wakiwamo upande wa mwenzi wake.

Baada ya kufungwa ndoa, inachofuata ni kupata watoto ingawa siku hizi, hasa kwenye mataifa ya magharibi, watoto si shemu ya ndoa. Watoto nao wanakuja na mitahani yao hasa wakati huu ambapo utandawazi umetanda na kuchukua nafasi za wazazi kimaadili na kimalezi. Unapopata watoto unafanikisha familia yako. Unawapo wapatia elimu tena wengine aghali kwa fedha za dhuluma, lengo ni kufanikisha na kuleta furaha kwa familia yako ambayo chanzo chake ni ndoa. Vyote hivi ni muhimu kwa binadamu walio wengi. Pamoja na umuhimu wake, vyote hivi hurejea kwenye mhimili mmoja uitwao ndoa.

Ndoa ina thamani ya ajabu hata zaidi ya utajiri. Unaweza kuwaamini wafanyakazi wako biashara yako hata magari ya thamani lakini huwezi kuwaamini ndoa yako. Chukulia jogoo na jike au mbuzi hata ng’ombe zizini mwako. Beberu, dume au mwenzake wa jirani akionekana anavizia vizia nyumba yako, hatashuku kingine zaidi ya kuibiwa mpenzi wake. Hatahofia kuibiwa vifaranga, vitoto au ndama wao. Hatahofia kupigwa bali kuibiwa mwenzi wake ambaye ni jike uliowafuga pamoja. Tumeshuhudia mabeberu ya mbuzi hata madume ya ng’ombe yakipigana hata kutoana mapembe. Yote ni juu ya kulinda tunu iitwayo mapenzi yaliyo katika ndoa ambayo inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote hata ikibidi kupoteza maisha ili kulinda heshima na thamani yake.

Je kama wanyama wanaweza kuhatarisha maisha yao na ya wenzao, hali iko kwa wanadamu wenye mifumo na akili vya hali ya juu? Tukubaline bila kufichana. Ukipasua moyo wa kila mwanamke au mwanaume, utakuta sehemu kubwa inahangaishwa inatawaliwa na mapenzi, madaraka, mafanikio na umri mrefu vyote vyenye kuleta furaha na ridhiko ambayo hutua kwenye ndoa.

Wandishi wa kitabu hiki ni wanandoa ambao, kama wengine wamepitia, kukwazwa, na hatimaye kujinausua kutokana na masahibu ya ndoa kiasi cha kupata ujuzi na uzoefu wa kuweza kuwamegea wengine. Miaka zaidi ya 27 katika taasisi hii tena kwa furaha na upendo si lelemama wala vitu vidogo vya kufutikwa chini ya busati au kaburi la sahau. Kwanini tunatumia uzoefu wetu wa ndoa? Ni kwa sababu ndicho kitu cha maana kwetu zaidi ya vingine tulivyo navyo. Tuna magari, majumba, mashamba, na fedha. Vyote hatuvielezei zaidi ya ndoa yetu. Kwetu ndoa yetu imekuwa ni utajiri usio na mfano. Ndoa yetu imefungiwa Afrika lakini tumeishi Amerika ya Kaskazini kwa mingi ya miaka yake. Tumepata watoto wetu wa kwanza Afrika na wa mwisho Amerika ya Kaskazini nchini Kanada. Tumesoma kule kadhalika watoto wetu.

Kabla ya kukubaliana au kupingana nasi, kwanza jiulize. Ni nini kivutio cha mafanikio na maanguko yako? Ni nani hupenda akuelewe, akuthamini, akujali, na kukutambua kuliko wengine wote waliokuzunguka kuanzia wazazi, watoto, marafiki, wafanyakazi wenzako hata majirani kama siyo mwenzi wako ambaye anaweza hata kukufanya ubadilishe nguo au kiatu ulivyopanga kuvalia kwenye mtoko wako wa maana? Bila shaka ni yule uliyemchagua ndiye anaweza kukuchagulia hata uonekane au kutokaje. Nkwazi alipokuwa anapata shahada yake ya uzamivu (PhD) alipanga kuvaa shuti ya kijivu. Nesaa alipinga chaguo hili la suti katika siku yake muhimu na kumchagulia suti ya samawi. Hakuna aliyechagua watoto, ndugu wala majirani. Lakini yupo mmoja atokanaye na mipango na makusudio yako ya dhati. Naye si mwingine ni mwenzi awe mke au mume.

Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: