Mwaka huu, inshallah, nitagombea urahis. Kwa vile kaya yetu ni ya vyama vingi, natimiza wajibu wangu. Kwanza, nataka nilete siasa mbadala ambapo kipaumbele change kitakuwa ni kuwakomboa mafyatu kiuchumi na kijamii kwa kuwawezesha kula na kushiba na kujidai kama fyatu yeyote aliye huru kwelikweli. Pili, mimi ni mpenzi wa maendeleo shirikishi ambapo kila fyatu lazima aonje keki ya kaya yake na kuifaidi. Pia, naamini kuwa uhuru halisi na wa kweli maana yake ni kwa mafyatu wote kufurahia maisha yatokanayo na uhuru walioupata baada ya kuupigania hadi wengine kumwaga damu. Huwa naamini pia, katika usawa wa mafyatu wote iwe katika kufanya kazi au kula. Hatuwezi kufanya kazi pamoja halafu kwenye kula, wale wachache na wengi waendelee kufa au kulala njaa. Hivyo, mikakati yangu ya kutaka mnichague niwafyatue, sorry, niwatumikie na si kuwatumikisha ndiyo hii hapa. Hivyo, jueni. Sasa mie ni rahis mtarajiwa. Aaamina. Nionye. Sera zangu nimezisajili na nina hati milki yake. Hivyo, atakayedukua sera zangu, nitamfanyia kitu mbaya kuliko anavyoweza kudhania.
Nikichaguliwa kuwa rahisi wa kaya, sirkal yagu haitapoteza mabiioni kununua mashangingi na mashankupe kwa ajili ya wanene kujienjoy na kufaidi wakati mafyatu tukifyatuliwa na shida. Ninunue mashangingi na mashankupe ya nini wakati tunayo ardhi lakini hatuitumii vilivyo zaidi ya kuikalia? Sambamba, tuna walaji lakini hakuna la maana wanalofikiria wala kupanga zaidi ya kula, kula, na kula zaidi. Mataifa mengi kama yale ya Mashariki ya kati hawana ardhi japo wanakula tena sana tu. Hivyo, nitanunua matrekta na kuwakopesha wakulima ili walime tuwalishe walaji hawa wenye ukwasi wa kutisha utokanao na wese.
Nitanunua mitambo ya kuchimba madini yetu ili yaweze kunufaisha mafyatu wote na vizazi vyao badala ya kunufaisha wachukuaji. Cha mno, nitasomesha vitegemezi vyetu hasa elimu ya uchimbaji gasi na madini ili faida ibaki kwetu badala ya kwenda nje kuwanufaisha wengine tena wasioyatolea jasho zaidi ya kusaini mikataba uchwara.
Juzi, nilipiga mahesabu na kugundua kuwa trekta moja ni bei chee na kidogo kuliko shangingi na shumbwengu. Je njuluku inayofujwa kwenye mashangingi ingeweza kununua matrekta, vitabu au kulipa madaktari na maticha wangapi? Hiyo njuluku ingetengeza ajira ngapi? Ingeondoa au kupunguza ukapuku kiasi gani? Ingeleta usalama kiasi gani? Zingeondoa au kupunguza ujinga kiasi gani? Zingeokoa maisha ya mafyatu wangapi? Je mnapoifuja zaidi ya kuongeza magonjwa ya moyo, ulahibu, unene, dhambi, na woga wa wale mnaowafyatua, mnapata nini? Don’t buy land cruisers. Instead, invest on land. Let tractors till the land instead of cruisers to cruise the land.
Msipoteze njuluku kununua takataka kama midude ya bei mbaya aka magari ya starehe inayowafilisi kwa kunywa mafuta mengi na kuzidi kufilisi mafyatu wenu, vidani na upuuzi mwingine kwa ajili ya wake na washikaji zenu. Hiyo midude inachafua mazingira hata mifuko mbali na jamii ya mafyatu wachovu wanaoona kama wanaenjoiwa na wachache waliofanya kosa kuwaamini maulaji yao yaliyobinafsishwa na genge dogo. Kwani, mkistaafu au kupoteza ulaji wala hawawezi kuvivaa na kujidai na kujienjoy bila vibaka kuwang’oa masikio kwa upande wa vidani. Kwa mashangingi, mtayasikia bombani.
Angalia mnavyoishi kwenye magereza yaliyozungushiwa mikuta kwa kuwaogopa mnaowafyatua kwa mauti yenu. Mimi sitaigiza ufujaji kama ule unaofanywa na matajiri wa Du Buy wanaoendesha vijikaya vile kama maduka yao binafsi tokana na kuendeshwa kifalme. Wao wanatanua na wako salama tokana na mifumo yao. Wana uhaba wa mvua lakini si akili kama sisi wenye uhaba wa ubunifu, ukweli, upendo, na uoni wa kesho. Siku mkifyatuliwa na kuzama kaburini hamtachukua hata picha zake. Umekuja bure, utarudi bure. Hata ukijenga uwanja wa njiwa kijijini kwako, ukifa, unageuka jiwe wazi la kuanikia mazao ya wale uliowafilisi. Badala ya kujiangalia, nitawaangalia waliniamini na kunipa ulaji wao. Sitaufanya ulaji wa mafyatu kuwa wangu, marafiki au familia yangu. Mie nitanunua vitabu ya kiada tena vinavyofaa badala ya vile vinavyotungwa na mafyatu wezi wanaojuana na wenye kuvipitisha ili watoto wa mafyatu wapate elimu safi. Nitanunua madawa ili kupambana na magonjwa. Zaidi ya hapo, nitawalipa matabibu na maticha vilivyo ili kuwaelimisha na kuwatibu mafyatu watakaoniamini na kunipa ulaji wao.
Kabla sijasahau, nitahakikisha nanunua magari ya wagonjwa. Je nitafanyaje hivi? Kama ninavyopanga kuyapiga kalamu mashangingi na mashumbwengu, nitapiga kalamu ndinga za ndata. Kwanini, kununua zana za maangamizi badala ya zana za kunusuru maisha?
Namalizia. Naombeni mafyatu mnipe kura ya kula ili nile. Sorry, nimesemaje? Natania. Sitakula bali kulisha wale wenye njaa walionipa ulaji wao. Tumeelewana? Basi, fanyeni kweli tulete mapinduzi ya kweli kwetu na mafyatu wooooote. Hizo ndizo sera zangu. Kumbe naota! Hii mibangi na mipombe, we acha tu.
Chanzo: Mwananchi leo.
No comments:
Post a Comment