The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 26 February 2025

No reforms, no elections ilhali tushageuzwa na kuchakachuliwa!!

 

Mjini hakuna stori ya no reforms no elections, kwa kisambaa, hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi. Kwanza, sijui kama mafyatu waliofyatuliwa na shida wanaweza kufyatuka wakawafyatua wawafyatuao. Wapo wanaosema eti mafyatu watinge mitaani na kukinukisha! Loo! Mbona mwaota mchana! Mnategemea mafyatu waliofyatuliwa wakafyata wafyatuke watekwe na kupotezwa? Nani afyatuke afyatuliwe shaba kama Tunda Lishe? Waliokwishatekwa, kuteswa, na kupotezwa watoshe. Nasikia ngebe za mageuzi kutaka uchaguzi huru na wa haki. Nani kawambia duniani kuna haki au uhuru hasa kwa mafyatu wafyatuliwa? Hamjaambwa kuwa haki hupokwa na iko peponi au motoni? Acheni ufyatu. Mkikomaa, nateka na kupoteza mkapate haki huko mtakakoharakishiwa. Siwatishi au kufyatuka kifyatu. Wangapi weshatekwa na kupotezwa? Nini kimefanyika?
            Tukiwa wakweli, lini mliwahi kuwa na uchaguzi huru na wa haki au mnaita uchakachuaji uchaguzi? Mnataka kumfyatua nani? Uchaguzi ni dhana tata. Unaweza kuchagua hata kuchakachua ukajiaminisha umechagua. Waweza kutochagua ukapitisha bila kupingwa ukajiridhisha umechagua japo hukuchagua. Mnataka mageuzi. Nani anataka kugeuzwa kama pweza kikaangoni ilhali walaji weshajiandaa kumfyatua hata bila kumpika au kumgeuza?  Kubalini yaishe. Baada ya wenye kaya kufyatua na kupitisha ‘mpendeka na mkubalika’ bila kupingwa hata walipotaka kumpinga, wapingaji wamefyatuka. Wanataka wamfyatue kupitia mageuzi. Wanafyatuka eti watasusa uchakachuaji. Ebo! Mkisusa, wachakachuaji watachakachua, kufyatua, na kula. Mmesahau mazoea au mwajitoa akili? Mnakuwa kama hamjui inshu mafyatu wangu! Kwa taarifa yenu, hata muwange uchi, hakuna cha haki wala mageuzi.
            Mafyatu wangu mlofyatuka na kutaka kufyatua, mnataka kujifanya hamjui manufaa ya kupitisha bila kupingwa kwa kaya na mafyatu waliofyatuliwa wakagoma kufyatuka na kufyatua!? Nazoza na mafyatu mliofyatuka mkatishia kususa uchakachuaji. Kwani hamjui kuwa mpakwa mafuta aliyepitishwa bila kupingwa lazima apite, apete, na kutesa hata mkisusa? Nyie mafyatu msiofyatuka hadi mkafyatuliwa nani aliwaroga kudhani kuwa mageuzi yanaweza kuleta mageuzi ilhali gegezi? Mkitaka mageuzi, jigeuzeni mfyatuke muache kufyatuliwa. Haki haiombwi, hupokwa. Hivyo, kususa ni kusuasua na kufyatuliwa. Badala ya kusema no reforms no elections mseme we must fyatuka and fyatua them to grab our rights. Period.
            Tukubaliane hata kwa kupingana. Mnapingaje mteule wa Mungu mwenye maono na ndoto visivyo vya kifyatu? Hamjui kuwa wateule wa Mungu hupaswa kutawala milele kama Ngwazi wa kwa akina Bwinobwino? Hamuoni maajabu yalotendwa kama ‘kufungua’ kaya iliyomkuwa imefungwa kwa makufuli japo ‘mfunguaji’ alikuwa na walioifunga, kama kweli ilikuwa imefungwa? Sasa kaya ‘imefunguliwa.’ Mnataka nini kama siyo ufyatu uchwara unaowafyatua? Mnapingana na kazi ya Mungu iliyomuondoa Jiwe. Eti mwataka kitabu, sijui katibua, sijui katiba! Mshaambwa kitabu mnachotaka kibadilishwe ni makaratasi yasiyoweza kuzuia mteule kupeta hata kwa goli la mkono.
            Kwa vile kimeishaumana, ishajulikana. Mafyatu weshafyatuliwa wakafyata wasifyatuke. Napendekeza tuokoe njuluku za mafyatu. Tusifanye uchakachuaji, sorry uchaguzi. Isitoshe, tukipitisha mpakwa mafuta tena bila kupingwa na kupingana, tutaondoa hatari za kutekana na kupotezana. Kwa vile ‘anakubalika’ kwa kila kiumbe, mafyatu, ndege, hata wadudu kama chawa na kunguni waliotamalaki siku hizi tokana na maajabu na miujiza, nasema kwa kinywa kipana tena kwa herufi kubwa HAKUNA MAGEUZI. No chakachuaization. Si inampendeza?
            Wasusaji, chonde chonde. Msituvurugie amani kupinga visivyopingwa au kutaka kugeuza visivyogeuzwa. Mnadhani waliofyatuliwa wakapitisha hawakufanya mageuzi? Unaweza kufanya mageuzi bila mageuzi na yote ni mageuzi. Kama mligeuzana na kupinduana, hayo hatutaki. Mnadhani mlivyochafuana na kuvuana nguo, mngekuwa na dola, si mngetekana na kupotezana? Shukuruni hamna dola. Mafyatu tunataka mapinduzi si mageuzi. Mapinduzi huleta amani. Mageuzi huleta machafuko. Nani anataka shari? Kawaulize wenzenu wa kaya ya jirani waliofanya mageuzi. Kila siku, wanageuzana hadi inakera. Wamegeuzana hadi wakawageuka mafyatu. Najua wapingaji hamjakaribishwa kufyatua keki ya kaya. Hivyo, mwawaonea maya tu. Kwa anayetaka mageuzi, anapaswa kupoka haki ndo aje na lugha ‘isiyokubalika’ ya mageuzi. Mnageuza nini wakati tulishageuzwa tangu zama za zidumu fikra za mkiti? Anayebisha aniambie. Lini tulifanya uchaguzi zaidi ya uchakachuaji na uchaguzi?
         Mcheke, mnune, mfyatuke, mfyate, mzoze, mzuzuke hata kuzomea, lazima mpakwa mafuta apite kama alivyoingia. Sasa mnafyatukafyatu ili iweje? Ufyateni na kukubali kufyatuliwa au mfyatuke mfyatue tujue. Kwanini kutaka kugeuza ‘mageuzi’ makubwa ya kidemokrasia yaliyokwishafanyika? Nani haoni haya mageuzi na maendeleo? Kama mnayaona, basi yakubalini tuendelee kutesa pasina kutesana au kuteseka na mageuzi. Kama hamuyaoni, jifanyeni mnayaona. Kama hayapo, jifanyeni yapo, na kama hayafai, jifanye yanawafaa hata kama hayawafai. Mwataka tuwakaubalie mgeuze mipango iliyopitishwa bila kupingwa? Machawa, sorry mafyatu weshasema liwalo na liwe.
Lazima mpakwa mafuta wao apite. No fyatuka, no fyatuliwa. Nisisiteze. Unaweza kuchagua kwa kutochagua na kutochagua kwa kuchagua. Yote ni uchaguzi na uchaguzi ni demokrasia hata kama ghasia. Wanaotaka mageuzi, wangoje hadi Yesu arudi. Hivi leo nimekunywa ngapi?
Chanzo: Mwananchi Leo.

Chunga usiolewe majuu ukidhani umeoa!


Kisa cha jamaa yetu toka tena kwetu Tanzania (mji hatutaji) kinafikirisha na kufundisha kwa wale ambao hawajaingia mkenge kama huyu bwana. Akiwa amesikia mazuri mengi juu ya kuukata kwa kwenda majuu, jamaa alianza mipango ya kwenda majuu kwa njia yoyote ili mradi mambo yake yamnyokee. Alitaka kuukata asijue unaweza kumkata yakamkuta ya kumkuta kama yalivyomkuta. Sawa na vijana wetu wengi, baada ya mambo kuwa magumu na kuwepo misifa mingi juu ya majuu, kijana aliamua kuingia mawindoni kusaka fursa za kumwezesha kukamilisha mipango yake ya kuukata. Kwanza tukiri. Huyu jamaa alifanya utafiti japo si kwa makini. Hakuwe peke yake. Vijana wetu wamejikuta kwenye hatari mbali mbali kama vile kuingia kwenye mataifa ya watu kinyume cha sheria na kuishia kurudishwa hata kufungwa huku wakishuhudia ndoto zao zikiyeyeuka.
        Zamani walikuwa wakizamia kwenye meli. Siku hizi hii njia ni kama imezibwa. Wapo wanaoamua kuomba vyuo ng’ambo ili waweze kuingia kule. Wakishaingia, hukimbia vyuo na kutafuta vibarua lau wajikimu na kuanza pilika za kupata makaratasi ya kuwawezesha kuishi kule kihalali. Wengine huamua kuoa hata kuolewa ili waweze kuishi kule. Kutokana na hii, vijana wetu wengi wanaolewa na wanawake wa Kizungu ili iwe passport ya kupandia majuu. Katika kisa hiki, picha hii inajitokeza kama tutakavyoidurusu.
        Tupo kwenye supermarket na jamaa toka Sudani.  Bila hili wala lile, anatuijia mama Kizungu akiwa na watoto machotara wa Kiafrika na Kizungu.   Kwa kuona hivyo, tunajua huyu mama kaolewa na Mswahili mwenzetu. Tunajipa moyo kuwa yupo sehemu akifanhya manunuzi, hivyo, akimaliza, atatokea japo tujuane. Wakati tukiwaza hili, yule mama wa Kizungu atujongelea na kutusalimia kwa uchangamfu kana kwamba tunajua. Hatushangai. Ni shemeji yetu hata kama hatujui atokako mumewe. Maana, huwezi kujua. Anaweza kuwa mweusi lakini siyo Mwafrika hasa kama anatokea Caribbean au Amerika ya Kati. Baada ya kutumakua kwa Kiingereza, nasi, bila ajizi wala hatujivungi. Tunajibu salamu zake. Anatuuliza “nyie mnatokea Afrika?” Tunamjibu kwa bashasha “haswa.”
            Mama wa Kizungu anatuuliza swali ambalo si Wazungu wengi huuliza kwa vile, kama ilivyo kwa Waswahili kuwa kila Mzungu anatokea Ulaya, nao wanadhani kuwa kila mtu mweusi anatokea Afrika bila kujali nchi walizotengeneza wao. Anauliza “mnatoka nchi gani Afrika?” Swali lake linanishangaza na kunifikirisha. Nami nauliza “umewahi kwenda Afrika? Anajibu “ndiyo, naijua Tanzania ambako ndiko anakotokea mume wangu ambaye bahati mbaya nilimzuia kuja nasi ili akae na watoto.” 
Msudani mmoja anadakia huku akionyesha kidole kwangu “huyu jamaa anatokea Tanzania.” Mama anatabasamu. Napigwa na mshangao tokana na Wazungu wengi kudhani Afrika ni nchi moja. Hivyo, wengi hawajui kuwa Afrika ina nchi zaidi ya hamsini walizotengeneza japo sasa wanaziunganisha. Namuuliza “ni wapi unajua Tanzania?” Anajibu “Arusha, Zanzibar, na Darasalam.”
            Baada ya maongezi mafupi, nawataka radhi tuondoke. Yule mama anatuaga kwa furaha akisema “kama mnaishi hapa, tutakutana tena na mtaongea na mume wangu.” Nami namjibu, “hatuishi hapa. Tunaishi mpakani na Marekani kama kilometa 40 toka hapo japo huwa tunakuja mara nyingi hapa kununua bidhaa.”
            Baada ya kuachana na yule mama, Msudani mmoja anasema “wallahi huyu mama kanifurahisha. Anaipenda Afrika.” Namkatalia. Namuuliza “umesikia alivyosema kuwa anasikitika alimzuia mumewe kuandamana nao ili akae na watoto?” Naongeza “huoni kuwa mwenzetu kaolewa?” Jamaa anastuka. Namwambia “huyu Kawajia yaani mama wa Kizungu hafai.” Tunaachia maongezi hapo na kwenda zetu. Nilipofika nyumbani, nilimpa Nesaa kisa kizima yakaishia hapo.
            Baada ya kama mwezi mmoja, tulirejea na familia kununua mahitaji kawaida. Bila hili wala lile, mwanetu mmoja anasema “naona Waafrika wale.” Kugeuka, tunamuona yule mama wa Kizungu na mumewe Mwafrika wakitujongelea. Mama wa Kizungu ananisalimia kwa bashasha. Anamwambia mumewe “ni yule jamaa niliyekwambia.” Tunapeana mikono jambo ambalo Wazungu wengi huwa hawafanyi. Namgeukia Nesaa na kumwambia “huyu ndiyo yule mama niliyekwambia.”
            Familia mbili zinachangamkiana wazazi na watoto. Mume wa Mzungu ananiuliza kwa kiswahili fasaha na mshangao “hii ndiyo familia yako?” Namjibu “naam.” Anajibu kwa kunyong’onyea “heri wewe umekuja na mkeo.” Nilimuuliza “mwenzetu Tanzania unatokea wapi na ilikuwaje ukawa huku?” Jamaa alitaja atokako Tanzania na namna alivyokuwa akifanya kazi kwenye utalii walopokutana na mkewe wa Kizungu wakaamua kufunga ndoa. Japo hakusema, lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kuukata kwa kuja majuu ambako uliishia kumkata. 
    Japo si wote, wengi wa vijana waliojiingiza kwenye ndoa hizi huishia kuolewa na kutumikishwa mbali na kutumiwa kuzaa watoto ambao kwa nchi zenye upungufu wa watu ni mali, huyu jamaa unaweza kumuweka kwenye kundi hili. Isitoshe, si yeye tu. Wapo wengi ambao, mara nyingi, hujutia uamuzi wao pale wanapojikuta wakimilkiwa na kutumikishwa kama mashini za ngono na watumwa wa mapenzi.
            Kufupisha kisa kirefu, yule bwana, pamoja na kunituchangamkia, hakuonyesha nia ya kutaka tumjue lau kutukaribisha siku moja tutembeleane. Hakutoa namba yake ya simu. Nami, kadhalika, sikutoa namba yangu ya simu. Kwa lugha ya mwili, hakuwa tayari kuwa karibu nasi. Nami nilifahamu ni kwanini. Angependaje tuwe karibu tuone anavyoishi? Pia, tunadhani alijua tunajua waume wa namna hii wanavyoishi kama tutakavyobaini kwenye kisa kingine cha Mfilipino aliyeolewa na mama wa Kizungu.
Chanzo: Mwananchi J'pili.

Wednesday, 19 February 2025

Barua kwa waliofyatuliwa na Tarampu


Kwanza, nawasalimia kabla kuwafyatua lau mfyatuke muwafyatue waliofyatua hadi mkakufyatuliwa na shida mkakimbilia kwa Tarampu aliyefyatuka na kuwafyatua. Nilimwandikia barua. Hajanijibu. Pili, niwajuze. Fyatu niko poa. Najua. Wengi wameniandikia barua mapepe kwa mapepe wakinisikitikia kuwa nitarejea na pingu miguuni na mikononi baada ya Tarampu kufyatuka na kufyatua. Wapo pia wanaoomba nirejeshwe lau wanikoge hasa wale walionibomu nikawachunia. Kadhalika, wapo wanaonionea huruma kuwa nikifyatuliwa na kutua na nitafyatuliwa na ukapuku na mifupo jizi nisiyozoea. Hawa ni nilikuwa nikiwatumia njuluku kidogo mbali na kuwapa moyo kuwa kuna siku ningewasukia waje majuu kutesa wasijue unaweza kuja ukaishia kuteseka.
       Tatu, wapo niliowafyatua hasa wanene wanaotamani nishuke kwenye pipa na pingu nao wanifyatue kuelekea lupango. Hafyatuliwi fyatu vinginevyo nitake. Kwanza, siishi kwa Joji Kichaka mbali na kuwa, hata nikipewa green card, nitaichana. Nani aishi kwenye kaya inayofyatuliwa na kichaa mbaguzi japo ana pwenti?
Nije kwenye inshu. Kwanza, nawashauri watakaofyatuliwa na kurejeshwa na pingu wasikonde na kusononeka. Afrika ina fursa bwererere. Kwa yeyote aliyeishi ughaibuni, kama hazioni, ajue anajifyatua au kujifyatulisha mwenyewe. Najua mifumo yetu ya kikale na kirushwa. Ukikomaa unatoboa. Hivyo, nendeni mkachafyatukie fursa ilmradi msijiingize kwenye siasa za majitaka mkaambiwa mna uraia pacha japo hamna. Pili, nawashauri. Mkishafyatuliwa na kurejea home, fyatueni wanaowafyatua. Anzeni mandingo kuonyesha namna exposure yenu ilivyowakomaza hadi mkang’ang’ania ughaibuni.
Tatu, nawashauri msirudie kosa kudhani kuwa ughaibuni kuna barabara za dhahabu na pepo. Nne, mbali na ubaguzi aliionyesha Tarampu na wengine kama yeye wanaozidi kuchepuka huko Ulaya, mjue adui yenu yuko home siyo ughaibuni. 
Tano, mjiulize hasa wale waliokimbia ukapuku, ilikuwaje mfyatuliwa na kugeuka makapuku kwenye bara lenye utajiri chekwa? Je tatizo ni wanaowafyatua mlowatengeza wenyewe mkashindwa kuwafyatua au nyinyi? Je mmejipanga vipi kuwaelimisha mafyatu juu ya kuwafyatua mafyatu wanene wanaofyatua hadi ukapuku ukawafyatua mkakimbilia ughaibuni bila kuwafyatua?
Sita, hakuna kitu hunichanganya kama sirkal kuhangaika na namna ya kufyatua njuluku toka ughaibuni wakati haina mpango wowote wa kuwasaidia mnapofyatuliwa kama kaya nyingine zilivyofanya kwa mafyatu wao waliofyatuliwa na Tarampu. Sijui hata kama wanajua idadi yenu na mahali mlipo. 
Saba, mjue, njuluku zinazotafutwa na sirkal husaidia mafyatu wezi wanene kuzifyatua na kupoza machungu yenu kiasi cha kushindwa kuwafyatua. Hivyo, husaidia wawafyatue kirahisi. Sasa Tarampu kafyatuka na kufyatua. Mafyatu fyatukeni mfyatue na kudai haki zenu badala ya kutegemea kukimbilia ughaibuni. Hisani huanzia home mafyatu wangu. Hata Tarampu angewajaza madolari na kumkatuma home, wezi wanene wangeyafyatua mkaendelea kuwa makapuku pamoja na kubeba moboksi usiku na mchana.
Kwa wale kama mimi wasio na wasi wasi wa kufyatuliwa wala kulazimika kuchukua uraia kwa sababu uraia pacha ni dhambi kayani, nendeni shule mkafyatue mambo ya maana ili mkirejea lau muwe na nyenzo za kufyatua njuluku kihalali. Mnadhani nisingefyatua shule ningepewa na kuaminiwa uga wa kufyatua ninayo fyatua tena kifyatu bila kuogopa hata mhariri wangu. Sorry. Nimesemaje? Mezea hiyo kama nimekukwaza  bosi wangu. Nilizidisha kanywaji na chigala kubwa.
Najua. Wengi hawatapenda ufyatuzi huu hasa wale wanaowafyatua mafyatu waliogoma kuwafyatuka na kuwafyatua. Kimsingi, Tarampu anatufundisha somo la kujitegemea, kufyatuana, kutokuwa wavivu, kujiheshimu, kutenda na kutendeana haki, na uwajibikaji wa pamoja kama mafyatu tuwe wakubwa hata wadogo. Kwa wanaomkumbuka jembe Joni Kanywaji, alitufundisha kuwa tukifyatuka na kuamua kufyatua mambo, tunaweza. Japo fyatu huyu alikuwa na madhaifu yake, angalau alikuwa na uthubutu wa kifyatu.
Hivyo, badala ya kumchukia na kumshutumu Tarampu, tumshukuru kwa kutukumbusha kuwa mikono na vichwa vyetu si mapambo. Licha ya kutufundisha kwa masimango, Tarampu ameonyesha asivyo mnafiki wala muongo kama wengi waliomtangulia waliokuwa wakitumia misaada ya kuacha mafyatu wetu ughaibuni kama njia ya kutufyatua ili tuwe tegemezi na kufyatuliwa. Ametufundisha kufagia nyumba zetu ili tuwe wasafi japo kiuchumi.
Mnajua siri ya ughaibuni kutuzidi katika kila kitu? Simpo. Kila fyatu huku ni fyatu kweli kweli anayefyatuka na kufyatua bila kuruhusu kufyatuliwa na fyatu yoyote awe na madaraka au la. Huku, mfano, huwezi kufunga rodi kupisha walaji wengi wao wasiolipa kodi bali kuifyatua mbali na kaya kapuku kutoa misaada ukiachia mbali kuingia uwekezaji uliogeuka uchukuaji na ufyatuaji mali na njuluku za mafyatu.
Mwisho, kwa mafyatu walionusurika kufyatuliwa, popote mlipo, gomeni kutuma njuluku hadi mjue haki zenu home. Mfano, muwambie wanaotaka kufyatua au kutegemea njuluku zenu wajenge mazingira yaliyowezesha kaya kama pale kwa jirani kuingiza mabilioni ya dolari. Lazima mjue mna usalama gani mkiwekeza badala ya kufyatuliwa na hadhi sijui maalumu. Nimesemaje? Ngoja nikajifiche wasininyake wakanitia pingu na kunipakiza kwenye pipa bure!
Chanzo: Mwananchi leo.

Monday, 17 February 2025

Ndoa yako imejengwa kwa nguzo ngapi?

Ndoa inaweza kuwa nzuri au mbaya. Pia, ndoa inaweza kujengwa au kubomolewa. Wajenzi na wabomozi wa ndoa ni wanandoa. Ndoa, kama taasisi yoyote ina changamoto zake. Kuna kufanya makosa kwa sababu, kama binadamu wowote, wanafanya makosa. Pia, yanapofanyika makosa lazima kuwepo na suluhu na namna ya kufikia suluhu. Leo tutaongelea ulazima na umuhimu wa wanandoa kkuwa kama daraja au uwili usiotenganishwa wala kuyumbishwa. Daraja, huwa ima na nguzo mbili ingawa kutokana na kukua kwa teknolojia, kuna madaraja yana nguzo moja. Pamoja na kuwa na nguzo moja, madaraja yote huwa na sehemu kuu mbili yaani sehemu ya kuingilia na kutokea.

            Katika kufanya daraja kufaa, kuwa na nguvu, kuhimili mikiki, na kutumika, lazima nguzo mbili zisimame pamoja na kutegemeana ili kufanikisha umuhimu wa kuwapo daraja. Mfano, upande mmoja wa daraja lazima ujue na kukubaliana au kujenga mazingira wezeshi kwa upande wa pili na wa pili kadhalika kwa upande wa kwanza. Mfano, kama upande wa kuingilia utaruhusu magari au wavukaji wengi, upande wapili utashindwa na daraja litayumba au kushindwa kufanya kazi yake ya kuvusha watu na vitu.

            Udaraja katika ndoa unajengwa kwa njia mbalimbali zikiwemo:

Mosi, kukubaliana. Kila kinachoingia au kutoka lazima kipitie sehemu mbili na kubebwa na nguzo mbili au nguzo moja ambayo katika ndoa ni ushirika na wawili. Hapa lazima tukazie. Tunaongelea ndoa ya mke na mume mmoja. Kwa ndoa za mitala, udaraja unawezekana japo kwa taabu. Huko hatutaenda.

Katika dhana ya kulindana, lazima wawili wawe kama nyuki au siafu wanapojilinda au kulinda mzinga au shimo lau. Ukiangalia uhohehahe na utepetevu wa wadudu tajwa, utagundua kuwa bila kushirikiana na kuhamiana, si chochote si lolote. Na wanandoa kadhalika. Mkshikamana, kulilindana, na kuhamiana, wengine watawaogopa. Mkibomoana inakuwa rahisi maadui ambao ni wengi kumalizia. Katika kulindana, lazima kuwa kulihali. Mpendane, mheshimiane, mshirikiane, mhifadhiane, na kuaminiana. Mfano, mkianza kuitana viatu na majina mengine mabaya, wengine watawaita hata makanyagio. Kila kitu mnacho na mna uwezo kubomoa au kujenga, kusuka au kunyoa. Tutatoa visa viwili vinavyotuhusu. Cha kwanza, Nkwazi alitembelea rafiki yake mmoja aishie Kanada. Siku ya kwanza kufika tu, baba alimkaribisha Nkwazi kwa shangwe. Kitu kimoja kilitibua kila kitu. Jamaa alikuwa akimfokea mkewe mbele ya mgeni kama mtoto mtoto mdogo. Hata mtoto mdogo huwezi kumfokea na kumdhalilisha hivyo. Jambo hili lilimuudhi Nkwazi kiasi cha kumwambia mwenyeji wake kuwa asingerudi katika nyumba yake. Mwenyeji alishangaa na kustuka na kuuliza “kwanini.” Nkwazi alimjibu kuwa hakupenda anavyomdhalilisha mkewe hata mbele ya mgeni kitu ambacho kwa Waswahili ni dharau hata kwa mgeni. Jamaa aliahidi kujirekebisha na mambo yakaisha.

Cha pili, kabla ya Nesaa kuja Kanada, marafiki zake Nkwazi walizoea kuuliza ana mke wa aina gani. Aliwajibu kuwa madam huwa ni mtu wa kupenda amani. Ajabu ya maajabu, marafiki zake karibu wote, walianza kumuita Nesaa Madam jina ambalo lilimkaa hadi tunahama mkoa ule tulikofikia. Hata kwenye mapokezi yake uwanja wa ndege, marafiki walionyesha wazi heshima na aina fulani ya woga kulingana na Nkwazi alivyokuwa amemjenga Nesaa ambaye kiumri alikuwa mdogo kuliko marafiki wa Nkwazi.

Mafunzo

Kwanini rafiki wa Nkwazi aliyemkaripia mkewe mbele ya mgeni aliamua kuachana na tabia hiyo? Jibu ni rahisi kuwa mwenzake alimfundisha tabia ya kumjali na kumheshimu mkewe.

            Kwanini marafiki wa Nkwazi, kwa pamoja, walimuita Nesaa Madam kama ishara ya heshima? Ni kwa sababu Nkwazi alimjenga badala ya kumbomoa. Somo kubwa hapa ni kwamba mwanandoa anao uwezo wa kumjenga, kumbomoa, kumheshimisha au kumdharaulisha mwenzake.

Mwisho, kila mwanandoa anao uwezo huu. Hivyo, ili mheshimike, lazima mjiheshimu na kuheshimiana. Kufanya hivyo, lazima kuwa na tabia za haki, usawa, upendo kulindana, kuhamiana, na kutegemeana. Akitukanwa au kudharauliwa mwenzio, nawe kadhalika unatukanwa au kudharauliwa. Kadhalika, akiheshimiwa mwenzio nawe kadhalika unaheshimika. Hapa kuna faida bila hasara. Hivyo, wanandoa, wajue ni daraja lililojengwa na nguzo mbili yaani mke na mume.

Chanzo: Mwananchi Jpili jana.

Sunday, 9 February 2025

Ndoa na vibabu, vibibi vya kizungu vijana muwe macho


 

Tunaona bibi wa kizungu na kijana MwAfrika uwanja wa ndege–––hatuutaji–––wakibusiana. Tumeamua kuandika haya juu utumwa kimapenzi ambamo waafrika ndiyo wahanga. Utumwa huu umejikita kwenye mapenzi bandia ambapo mmoja wa ‘wapendanao’ humtumia mwenzake kulingana malengo na hadhi na rangi yake. Htuzushi. Utaona vibabu/bibi vya kizungu vikifunga ndoa na wavulana/wasichana wa kiafrika mtawalia. Bila kupoteza muda–––hapa kuna tamaa, ujinga, na umaskini–––kama vyanzo vya ukoloni na utumwa huu wa kimapenzi.

            Katika mila za kiafrika, mwanaume hutegemewa kuoa mtu ima wa umri wake au anayemzidi umri japo si kwa mbali sana. Inapotokea mwanaume akaoa mwanamke sawa ua zaidi ya mama yake au binti akaolewa na kibabu sawa na babu yake, jamii hustuka, kuhuzunika, kushangaa, kuchukuia, hata kulaani. Hakuna kitu muhimu katika ndoa kama tegemeo la kuzaa watoto ambao ndiyo malipo kwa jamii na wazazi. Ndoa bila mtoto, kwa muafrika, ni janga. Tujiulize. Inakuwaje wahusika wanaweka kando hitajio hili muhimu? Kuna cha mno? Inakuwaje kijana wa kiafrika kufunga ndoa na zee lisiloweza kumzalia au kumzalisha au kumuachia ujane? Je ni tamaa, ujinga, au umaskini ukiachia mbali kuabudia rangi ambapo mweupe, hasa mzungu, anaonekana mali japo si mali kitu?

            Katika ndoa hizi, kama kweli ni ndoa, wazungu hutumia waAfrika. Hatujawahi kuona MuAfrika mzee akioa msichana mzungu au kijana mzungu akioa bibi muAfrika. Kuna tatizo. Si rahisi kupata majibu sahihi bila kudurusu. Kwa akili ya kawaida, hili si jambo la kawaida, hasa kwa waswahili. Kimsingi, katika ndoa hizi, mweupe ana mamlaka na mswahili hana. Si vibaya kusema kuwa mswahili anaolewa katika mahusiano haya.

            Kiafrika, mwanaume huoa na mwanamke huolewa. Ila katika uhusiano tunaojadili, mwanamke/mwanaume wa kiAfrika huolewa na mzungu ambaye humuoa bila kujali jinsia. Hata katika utumwa huu, mswahili hutegemea akiolewa na mzungu ataukata kwenda majuu na kuchuma madola. Hapa thamani ya maisha ya binadamu ambayo ni kubwa kuliko chochote, huwekwa kwenye vitu vya hovyo tokana na ujinga au umaskini kama masalia ya ukoloni wa kimila ambapo mtu mweupe ni mkombozi wa mtu mweusi ni mkombolewa–––hata kama dhana hii ni hovyo na ushahidi wa utumwa wa kiakili, kimaadili, na kimila.

            Tuweni wakweli. Hivi kuna mapenzi ya kweli kati ya kizee cha miaka–––tuseme miaka 60, 70 au zaidi kuoa kijana wa miaka 30, 35 hata 40 au babu kuoa kigoli umri wa mjukuuwe? Hapa tunapata dhana ya ubaguzi wa kujitakia ambapo muathirika hujiona dhaifu mbele ya mkoloni wake bila kujali jinsia. Je kuolewa na mzungu ni kuukata au kupatikana licha ya kudhihirisha ujinga, umaskini, na tamaa ya wahusika? Tumeisha Ulaya kitambo si haba. Kuna kitu wanacho yaani ubinafsi/umimi (individualism) ambapo mtu kujiona kama huru na asiyejali wengine isipokuwa yeye. Hapa ndipo chanzo cha kwanza cha balaa hili kilipo mbali na ukoloni ambapo waafrika wameaminishwa na wakaamini–––iwe ni kwa kupitia dini au siasa–––kuwa wazungu ni wakombozi wakati ni waangamizaji. Utamuona Yesu mweupe wakati hakuwa mzungu. Mitume wote siyo waafrika. Maandiko matakatifu yote ni ya kigeni na lugha zinazotumika kuyaeneza. Huu ndiyo mzizi wa kila kitu. Waligundua, kutengeneza, na kueneza ‘weupe’ kuwa ukombozi na wengine wenye dhambi. Unashawishikaji kuwa kila mtu anazaliwa na dhambi wakati mtoto mdogo ni malaika?

            Utumwa kwa waafrika ulianza tulipohujumiwa na kurubuniwa kuacha mila zetu tukakumbatia mila hatari za kigeni ziitwazo dini na ustaarabu japo si chochote wala lolote bali maafa kwetu. Mzazi unajisikiaje kijana wako wa kike/kiume anapoolewa na bi kizee kuliko hata baba au mama yake kwa kisingizio cha ‘mapenzi hayana macho.’ Mapenzi yana macho. Ndiyo maana, hayaishi bila kuwa na uhuru na utashi wa kuchagua, ambao katika balaa hili jipya haupo. Binadamu anapotumia njaa, tamaa, ujinga na umaskini kama nyenzo za kufikiri, anaweza kufanya jambo ambalo hata mnyama hawezi kufanya.

            Tumalize kwa kuwashauri vijana wa kiafrika kuacha kuuza utu wao eti kwa tamaa na ujinga wa kwenda majuu. Wakishafikishwa ‘majuu’, huumizwa na kuwa watumwa zaidi wakaishia kujuta kama mmoja niliyekutana naye kwenye mji jirani aliyenyofolewa Arusha na kuishia kwenye utumwa.

Chanzo: Mwananchi leo.

Wednesday, 5 February 2025

I Cry fo Ambazonia and Darfur–––My baby

I Cry for Ambazonia and Darfur

ISBN 9789956554935

Pages 150

Dimensions 203x127 mm

Published 2025

Publisher Langaa RPCIG, Cameroon

Format Paperback

ISBN9789956554935
Pages150
Dimensions203x127 mm
Published2025
PublisherLangaa RPCIG, Cameroon
FormatPaperback

I CRY FOR AMBAZONIA AND DARFUR

by Nkwazi Nkuzi Mhango

The world remains tragically silent on the suffering of the people in Ambazonia, Cameroon, and Darfur, Sudan. Since these conflicts began, the international community has failed to adequately address or arrest the violence and protect innocent lives. Countless people have been killed, displaced, and robbed of their hope. This book serves as both a condemnation and a plea to the international community, urging it to acknowledge its failures in these regions. Nkwazi Mhango argues that this inaction constitutes a form of discrimination against the people of Ambazonia and Darfur, highlighting the stark contrast between the global rhetoric on human rights and the grim reality faced by the victims. “The Cry for Ambazonia and Darfur” is a powerful call for humanity to awaken to its responsibilities. It demands more than just empty gestures; it urges critical self-reflection and a genuine commitment to resolving these conflicts. Mhango implores us to recognize our shared humanity and act with the compassion and justice we would expect for ourselves.

 BOOK PREVIEW
British Pound£
Paperback
£15.00 

ABOUT THE AUTHOR

Nkwazi Nkuzi Mhango

Mhango is the author of Saa ya Ukombozi, Nyuma ya Pazia, Souls on Sale, Born with Voice, Africa Reunite or Perish, Psalm of the Oppressed, Perpetual Search, Africa’s Best and Worst President: How Neocolonialism and Imperialism Maintained Venal Rules in Africa and ‘Is It Global War on Terrorism’ or Global War over Terra Africana?: The Ruse Imperial Powers Use to Occupy Africa Militarily for Economic Gains, How Africa Developed Europe: Deconstructing the His-story of Africa, Excavating Untold Truth and What Ought to Be Done and Known, Africa’s Dependency Syndrome: Can Africa Still Turn Things around for the Better?, Our Heritage, Family Friend of Animal and Matembezi Mbugani (Children’s book co-authored with his wife Nesaa).

Woga, ukale, kujifyatulisha na kufyatuliwa

Juzi nilipata mstuko, mshangao, na masikitiko sina mfano. Nilisoma taarifa kuwa Kenya inafyatua takribani dolari bilioni tano toka kwa diaspora dhidi ya dolari bilioni 1.50 za uwekezaji. Kwa taarifa hii, kenya inafyatua njuluku ndefu kuliko misaada na uwekezaji/uchukuaji. Niligundua ni kwanini kaya yenye mafyatu wachache na ardhi kidogo isiyofikia hata nusu ya mafyatu wetu na neema asilia kiduchu ikilinganishwa nasi inakuwa na uchumi mkubwa kuliko sisi. Katika kutafakari na kufikiri, niligundua kuwa tunajifyatulisha na kufyatuliwa tokana na ukale, woga, na mtima nyongo.
            Sambamba na Kenya, siku chache kabla ya kutolewa taarifa hii, sirkal iliangaza mikakati ya kupata njuluku za diaspora wetu bila kustahiki wala kujenga mazingira mazuri. Kwani, inakataa uraia pacha huku ikishobokea wawekezaji ambao wengi ni wachukuaji tu. Jikumbushe tulivyofyatuliwa na matapeli toka India waliojifanya kuwekeza kwenye Shirika la Reli wakaishia kutufyatua njuluku hata mabehewa. Kabla ya hapo, walikuja ABSA wakafyatua banki yetu ya Biashara na kusepa. Walifuatia BAE Systems, Barriki dhahabu, CHAVDA, EPA, ESCREW, IpTelo, Mabilioni ya Njaa Kaya, Meremetuka, na nyingine nyingi ambapo tulipigwa njuluku ndefu tu. Kama haitoshi, jikumbushe Richmonduli-Dowan, Kagoda, mwanakaya gold na mazabe mengine yaliyofyatua na kufilisi kaya yetu. Tatizo ni nini?
            Wakati wachukuaji wanakuja kufyatua njuluku iliyokwisha tengenezwa, tunakosa njuluku wanayotengeneza wanadiaspora wetu! Akili au matope? Tunazidiwa na vijiinchi kama Gambia chenye watu milioni 2.4 na ukubwa wa 11, 300 km2 kinachozidiwa na mkoa mdogo kama Kilimanjaro wenye ukuwa wa13,250 km2 kilichoingiza dolari 775.6 ikilinganishwa na Bongolalaland iliyoingiza dolari 570 huku uwekezaji ukiwa wa thamani ya dolari milioni 931.60. Fedha ya diaspora haina masharti na shaka kama uwekezaji uliogeuka upigaji.
        Tunahitaji uongozi unaojiamini, wenye ubunifu, wa kisasa, na usiotaka kuvuna usipopanda kama ilivyo. Unataka wabongo wa diaspora watume njuluku wakati huwatambui wala kuwamotisha? Inaingia akilini kweli? Hata unapotaka kuwafyatua kuwapa hadhi maalumu, unawazingua na kuvuta miguu. Ajabu, uraia huu huu unaoonekana mali wakati si mali kitu wanajizolea hata wacheza kandanda! Tunamkomoa na kumfyatua nani? Wawekezaji wanakuja na kujizolea njuluku kwenye shamba la bibi hadi mapipa yetu yanakamatwa ughaibuni na kushitakiwa na kufyatuliwa mamilioni ya dolari. Rejea mamilioni ambayo yeshalipwa au yatalipwa tokana na uzwazwa na woga wa kimfumo.
        Mfano, mnataka wanadiaspora walete njuluku home wakati hawana haki za kumilki mali? Mnawapa hadhi maalumu. Nani aliwapa mamlaka haya wakati Sir God aliwaumbia Bongo? Tunamkomoa na kumfyatua nani zaidi ya kujikwamisha, kujikomoa na kujifyatulisha? Ukiangalia sababu kubwa ya kuogopa uraia pacha si nyingine zaidi ya woga wa siasa za majitaka. Kwani, hizo kaya zilizotoa uraia pacha zimepungukiwa nini? Je mafisi na mafisadi wote ni wana uraia pacha?
         Rafiki yangu Prof Mutua, mwenye uraia wa Kenya na Marekani aliwahi kugombea ujaji mkuu akanyimwa tokana na kuwa mwanafunzi wa jaji mkuu aliyekuwa anamaliza muda wake. Hapakuwa na tatizo na uraia. Ukiachia huyo, Baba wa taifa la Senegal Leopord Sedar Senghor alikuwa na uraia pacha na bado alikuwa rais aliyeleta uhuru na kufanya mambo makubwa kwa Afrika. Inakuwaje sirkal yenye kuogopa na kukataa uraia pacha inaendeshwa na njuluku toka majuu mbali na chaguzi zake kugharimiwa na fedha hiyohiyo? Kunani hapa? Tuambiane ukweli bila kuogopana.
        Kuna kipindi nilimsikia fyatu mmoja mnene mwoga na zwazwa akisema eti tukiruhusu uraia pacha, wageni watachukua ardhi yetu. Ajabu. Mbona wageni wengi walikwishakujitwalia ardhi? Hiyo ardhi tunaifanyia nini zaidi ya kuitelekeza tukitegemea kuagiza majanki toka nje? Nani anaweza kuamini kuwa kaya yenye uwezo wa kuzalisha mchele hata kulisha eneo zima la Afrika Mashariki ingeagiza mchele wenye thamani ya dolari milioni 27.49 toka Thailand mwaka 2023? Yaani tunalishwa na nchi yenye ukubwa takriban nusu yetu wa 513,120 km2 na idadi ya watu 64,785,90? Tukifyatuka na kusema tumerogwa, mtasema tunatukana kweli?
Miaka michache iliyopita, bi mkubwa wangu alikwenda uhamiaji kutafuta passports yake na za wanetu wakati akijiandaa kuja huku. Aliulizwa maswali ya kipuuzi mfano, unakwenda kule kufanya nini? Unamuulizaje fyatu mzima tena mjanja anakwenda majuu kufanya nini? Wewe inakuhusu nini? Mbona mnapotaka tulete njuluku home hamuulizi kaipataje?
        Juzi nilikuwa napitia tovuti ya sirkal inayosuasua juu ya vibali vya kusafiria nje. Hapa Kanada hakuna kitu kama hicho. Kwanini kumsumbua mtu akwambie anakwenda kufanya nini ughaibuni utadhani taahira? Wapo wanaosema eti wanafanya hivyo kuepuka mafyatu kwenda kufanya uhalifu huko. Kwani hakuna sheria? Je hawa wanaopewa hawafanyi uhalifu hasa uuzaji bwimbwi? Kama fyatu anataka kwenda ughaibuni, mpe pasi asepe. Mengine atajijua. Kwanza, hata balozi zetu ughaibuni hazina mpango wala utaratibu wa kuwasaidia wabongo walioko nje vinginevyo iwe ni kwenye kuunga juhudi na mambo mengine ya kisiasa za majitaka.
Tufikie mahali tukue na kukomaa na kuacha uzamani na woga. Vinatuchelewesha na kutufyatua na kutufyatulisha. Hivi samaki ana miguu mingapi?
    Chanzo: Mwananchi leo.

Sunday, 2 February 2025

Mpumbavu aliyevunja ndoa akiamini anaihami


Kuna kisa cha mwanandoa Gilombo (si jinale) tulichoshuhudia.  Gilo hakujaliwa sura wala tabia nzuri. Alikuwa mzinzi wa kutisha aliyelazimisha ndoa kwa kijana handsome na mwenye nazo asiye na uzoefu. Alibahatika kupata mtoto wa kike katika ndoa ya kulazimisha iliyoduma miaka miwili tu.
            Baada ya kuishi na mumewe kwa mwaka mmoja na kulazimisha kubeba mimba bila ya makubaliano, jambo ambalo lililomstua muwe, Gilo aliamini mumewe bwege asiyeweza kustuka wala kushuku. Hivyo, mazabe yake yasingefumka. Taratibu, mambo yalianza kutifuka na kufumka. Mumewe alianza kumshuku kwa kila jambo. Mfano, kuna wanaume waliokuwa wakiwatembelea aliowatambulisha kama ndugu zake. Bahati mbaya, mmojawapo alikuwa akifahamika kwa rafiki wa mumewe waliyekutana JKT. Siku moja, Gilo akiwa ametembelewa na huyu ndugu yake ambaye pia alikuwa mshikaji wake jeshini, alifika rafiki wa mumewe aliyewajua wawili hawa.
            Mume aliporejea na kuwakuta wageni hawa, alimtambulisha ndugu mshikaji wa mkewe kama shemeji yake aliyekuwa amempa mtaji kuanzisha biashara. Rafiki yake alishangaa na kuchukia tokana na aliyojua. Hivyo, alishindwa kuvumilia. Wakati wakiagana, alimuomba rafiki yake awe na kifua amwambie jambo. Jamaa alipasua mbarika na kuweka kila kitu wazi. Baada ya kupita miezi kadhaa, jamaa mshikaji wa Gilo alirejea akitaka fedha zaidi toka kwa mumewe ambaye alimkatalia zamu hii. Baada ya mwizi wake kuondoka, alimbana mkewe aliyekiri kuwa na udugu na uhusiano wa kingono. Tangu siku hiyo, mapenzi yalitoweka.
            Kuona kitumbua kinaingia mchanga, Gilo alianza harakati za kuhami ndoa yake. Alikwenda kwa wachungaji kuomba ushauri na kuombewa. Mambo yalizidi kuwa mabaya. Mwishowe, aliamua kwenda kwa mganga wa kienyeji aliyemwambia kuwa alikuwa na nuksi na alikuwa amerogwa via vya uzazi na shangazi yake. Hivyo, alipaswa kutumia dawa kuingiza ukeni ili kutibu nuksi. Sharti kubwa alilopewa ni kutafuta mwanaume ambaye si mumewe ajipake dawa na kumuingilia mara moja tu. Kwa kutapatapa na upumbavu, Gilo alikubaliana na sharti. Tatizo, ni nani angempata ajipake hiyo ‘dawa?’
            Jibu lilikuwa rahisi. Alimwambia mganga wa kienyeji kuwa hana mtu. Mganga alimwambia kuwa kama angempa fedha, angefanya kazi hiyo. Walikubaliana na Gilo wakajifungia ndani wakafanya ngono. Baada ya kumaliza, mganga wa kienyeji aliongeza sharti jingine kuwa lazima wafanye ngono kwa wiki nzima kila jioni. Gilo alistuka lakini alikuwa ameishaingia mkenge. Alikataa katakata. Mganga kuona hivyo, aliamua kumtishia angemwambia mumewe. Gilo ilibidi akubali. Wakaendelea kufanya mapenzi. Kabla ya wiki kupita, mume alistuka na kuamua kumfuata mkewe pindipo alipoaga jioni anakwenda kwenye maombi. Kimyakimya alimfuata hadi akiingia nyumba ya kulala wageni na mganga. Alifanya harakaharaka akawafuma na kumuacha hapohapo bila hata kurusha ngumi wala tusi.
Katika kushuhudia na baadaye kudurusu sababu za kuvunjika kwa ndoa hii, tuligundua vitu kadhaa. Mosi, ndoa hailazimishwi. Pili, maisha ya kabla ya ndoa yanaaweza kuimarisha, kuyumbisha hata kuvunja ndoa. Tatu, kutokujiamini, ubabaishaji, kutafuta ushauri bila kufikiri na kutahadhari, na kuamini kila ushauri vinaweza kuvunja ndoa. Nne, kutafuta tatizo kwa kutapatapa ni hatari kwa ndoa. Wanadoa wanapaswa kuendana. Kwani, wawili hawa hwakuendana kwa sura na tabia. Japo hili si tatizo, licha ya kulazimisha ndoa, Gilo aligeuka ‘chuma ulete.’ Kwanza, baada ya kuhamia kwa kulazimisha ndoa, Gilo aliwasomba ndugu zake ukiachia kukmtoa fedha mumewe ili kuwatumia wazazi wake kwao. Pili, Gilo, licha ya kumficha mumewe ukweli kuhusiana na maisha yake yaliyosababisha alazimishe ndoa kwa, hakuwa muwazi juu ya maisha yake ya awali.
            Je unajifunza nini hapa? Mosi, ndoa inataka uaminifu na ukweli. Pili, siyo kila ushauri unafaa. Tatu, ndoa haina daktari wala mchungaji isipokuwa wanandoa wenyewe. Nne, hakuna siri ya milele. Tano, usiamini kila mtu na kila kitu. Sita, ndoa inataka kujiamini. Saba, waganga wa kienyeji na wachungaji matapeli ni maadui wakubwa wa ndoa. Nane, katika ndoa, wanawake wana maadui wengi kuliko wanaume. Tisa, mchawi au mlinzi wa ndoa yako ni wewe mwenyewe. Kumi, unapopta tatizo, tumia njia sahihi ukiwa umetulia kufikiri na kufanya utatifiti ukiepuka kufanya maamuzi kwa msongo wa mawazo na hofu.
Chanzo: Mwananchi leo.