The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Sunday, 18 January 2026

Wajue Wamosou ndoa zao za ajabu


Nchini China na Mongolia, kuna jamii ya watu waitwao Mosou. Ni watu wanaoshika mila kwelikweli. Baadhi ya mila zao hasa kuhusiana na ndoa, zinaweza kukuchanganya, kukushangaza hata kutisha. Kwanza, wao ni matrilineal, yaani, katika jamii hii, mtoto huchukua ubini toka upande wa mama na si baba kama kwetu na jamii nyingi duniani. Hii ni tofauti na dunia nzima ambayo ni patrilineal tokana na kuendeshwa na mfumo dume ambapo ubini wa mtu hutoka kwa baba na si mama. Mfumo wao ni mfumo jike haswa. Japo hapa Tanzania tumewahi kuwa na jamii za namna hii kama vile Wamakua, ambao pia hupatikana sana nchini Msumbiji utamaduni, huu ulikufa zamani.
       Hii, pia, ipo kwenye jamii za Wakikuyu na Wakamba wa Kenya. Mama akijifungua mtoto ambaye hamjui baba yake, humpa ubin wake. Hivyo, usishangae kusikia watu maarufu kama wanamuziki maarufu nchini Kenya kama Ken wa Maria au Kim wa Regina.
Wamosuo wajulikanao kama the Kingdom of Women au himaya ya akina mama. Kwao, mke na mume hawaishi pamoja kama tuishivyo sisi na wala wanaume hawawajibiki kisheria kutunza wala kumilki watoto waliowazalisha. Kila mmoja anaishi kwake na wanakutana au kuachana wakati wowote wanapotaka na kutafuta mwingine. Japo ni kawaida kukuta wawili waishio kama mke na mume, bado hii haiwazuii kuwa na washirika wa ndoa wengine nje ya ndoa hii ambalo ni jambo la kawaida linalofanyika na kukubalika katika jamii hii. Pia, hakuna idadi ya washirika katika uhusiano inayoruhusiwa wala kukatazwa bali suala na uamuzi binafsi wa wahusika.
Kwa vile safu hii ni ya masuala ya ndoa, leo, tutawaletea ndoa za ajabu za Wamusuo. Katika jamii, wanawake wana nguvu na ushawishi mkubwa juu ya familia na ndoa. Wanaruhusiwa kuwa na wanaume wengi kwa wakati mmoja na watoto wanaozaliwa tokana na mahusiano haya ni mali ya mama. 
Pia, jamii ya Wahimba ya kule Namibia inasifika kwa ukarimu kiasi cha mume kumruhusu mkewe kulala na mgeni kama ishara ya upendo na urafiki. Huu utaratibu unaitwa okujepisa omukazendu yaani ishara ya ukarimu na urafiki. Hata hivyo, mke anaweza kukubali au kukataa kulala na mgeni.
Tukirejea kwa Wamusuo, kama ilivyo kwa baadhi ya jamii na dini ambapo mwanaume anaruhusiwa kuwa na wake zaidi ya mmoja, kadhalika nao, mwanamke anaruhusiwa kuwa na wanaume zaidi ya mmoja na hakuna ugomvi.
Kwetu sisi wenye wivu, kuna jambo ambalo Wamusuo hawana. Nalo ni wivu wa mapenzi. Kwani, wanaweza kuwa na wivu wa kugombea uongozi au mali lakini si mapenzi! Mila na utamaduni huu vimewashangaza  wachunguzi na wasomi wengi wa mambo ya kijamii hasa baada ya kugundua kuwa katika jamii hii hakuna unyanyasaji wa kina mama au kina baba. Katika jamii kuna aina ya ndoa kuu inayojulikana kama walking marriage, zouhun, au ndoa inayotembea ambapo wahusika huwa na uhusiano wa kindoa wa muda. Mmoja au wote wakichoka au kuchokana, kila mmoja huacha kumtembelea mwenzake na kutafuta mwingine na mambo huishia hapo.
Katika jamii akina mama au daba, wana mamlaka makubwa juu ya mali na maisha ya familia. Akina mama huwarithisha mamlaka mabinti zao sawa nasi tunavyowarithisha watoto wetu wa kiume. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wanawake wa Kimasuo huwa hawaolewi wala kuishi pamoja kama kwenye ndoa zetu ambapo wawili huwacha familia zao na kwenda kuishi peke yao na kuanzisha na kulea familia. Badala yake huwakaribisha wanaume kuishi na hata kuzaa nao na kila mtu kuchukua hamsini zake. Pia, katika mahusiano ya ndoa ya Kimasuo, hakuna umilki wa pamoja wa mali.
Cha mno, katika jamii hii hakuna kitu kinaitwa ndoa kama tukijuavyo ambapo wawili huingia mkataba wa kudumu kulingana na aina ya ndoa. Kwa Wamosuo, hakuna cheti cha ndoa au ulazima wa mtu kumganda na kuishi na mwenzake. Hivyo, yeyote anaweza kumchagua yoyote wakaishi kwa muda watakao na watakavyo. Hiyo ndiyo ndoa ya Kimasuo.
Chanzo: Mwananchi J'pili leo.


No comments: