The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 15 July 2026

Wanandoa kutendeana haki na wema si hisani


Japo halifurahishi, ni kawaida kuona au kusikia wanandoa wakitendana. Hutofautiana, huchukiana, husuluhishana, baya kuliko yote, huumizana kwa kutenzana ndivyo siyo. Ni jambo jema wanandoa wanapotendeana hasa katika mambo baadhi au yote ya haki kiasi cha kuridhiana, kuridhishana, na kuendelea kufaidi ndoa zao wapaswavyo na watakavyo. Hapa, hakuna miujiza wala mazingaombwe. Ni suala la kuelewa na kuchagua kusuka au kunyoa ili usukwe au kunyolewe.
    Leo, tutaongelea kutendeana kwa maana ya kutenzana. Kuna tofauti kati ya mawili haya. Kutendeana ni kufanyiana mambo yawe mabaya au mazuri. Kutenzana, kimsingi, ni kuumizana. Ukimtenda mwenzio, utamchukia na kumchukuza, utamhujumu, utamhukumu, na hata kumdhulumu. Huku, ndiko kutenzana. Kuhusiana na kutendeana na si kutendana, tushaeleza hapo juu.
            Tukirejea na kutia nukta kwenye, yaani kutendeana haki, tuseme wazi. Hili, ni dhamira na hitajio kuu la ndoa ingawa halifanyiki bila kuwepo kupendana. Kwa vile mzizi wa ndoa ni kupendana, hatutaongelea hili kwa vile lazima liwepo kabla ya mengine, ingawa kadri muda unavyokwenda mambo hubadilika.
            Kwanini kutendeana haki si hisani bali wajibu? Kwanza, hakuna aliyewalazimisha kupendana na kuoana. Hivyo, mkiwa wakweli kwa malengo, nia, na viapo vyenu, bila kutenda na kutendeana haki, ni kama hakuna ndoa. Kama ipo, basi ni ndoa jina ila si ndoa kwa maana yake. Kwanza, mlitafutana, mkapendana, na kuamua, kuapishana, na kuoana ili kuishi kwa pamoja. Je, kwanini mlifanya yote hayo? Jibu ni rahisi. Kila mmoja alikuwa akitafutaakitakacho lakini asichonacho kwa mwenzake. Hivyo, kutendeana haki si chaguo wala hisani bali hitajio muhimu la uwepo wa ushirika wenu.
            Sisi waandishi ni wanandoa waliodumu kwenye ndoa kwa takribani miaka 30. Tunaijua ndoa ndani na nje. Tunaijua kwa mapana na marefu yake. Tunajua raha na karaha zake. Hivyo, tunapoandika haya, hatusomi sehemu zaidi ya kujisoma na kukumbuka mapito yetu m bali na kufanya utatifi juu ya suala zima.
            Kuna usemi maarufu wa kifaransa kuwa l’essence du droit est l’essence du devoir, yaani, bila wajibu hakuna haki. Kwa lugha nyepesi tena kwetu waswahili ni kwamba linapokuja suala la haki ni sawa na mikono miwili kunawishana. Au tuseme ni nikune nikukune. Ndoa ni kukunana na kupata haki kwa kuwajibika na si vinginevyo.
            Tuna usemi wetu binafsi. Kwetu, ndoa ni biashara ya watu wawili wenye malengo na vichaa vinavyofanana na kukubaliana. Kama kweli mnapendana, mtatendeana haki. Hapa, haki si hisani wala ombi bali wajibu. Katika ndoa, haki huja sambamba na upendo na heshima.
            Kama, mfano, mume anataka mke amtii kama haki yake na wajibu wa mke. Je inawezekana akatiiwa bila yeye kumtii huyu atakaye amtii? Kumbuka. Mwenzio siyo roboti lisilo na hiari wala kuweza kuhoji.  Kwanini utake mtu, tena mwenye akili kama wewe au hata zaidi akutii bila wewe kuwa tayari kumtii? Je, inawezekana kutiiwa bila kumtii anayekutii kwenye maisha ya kawaida? Hili, linawezekana kwenye ukoloni, utumwa, na utwahuti lakini si kwenye jamii ya watu wastaarabu. Kama wanadoa waitikiavyo kila jambo, lazima na kwenye kutenda haki wafanye hivyo.
            Katika hili, sisi tunayo kanuni moja mujarabu na rahisi. Huwa tunaulizana. Je, wewe ungekuwa mimi ungefanyaje hasa unapohitajika kunifanyia nini? Nini ungenifanyia sawa na kile ambacho ungekuwa mimi ungependa na kutaka nikufanyie? Tumaanishacho ni kwamba kila umfanyiacho mwenzio, unajifanyia wewe kwa kumtumia.
            Bila kuficha wala kufumba, wawili mpeanavyo ‘chakula cha usiku’, nani humtegea mwenzake? Nani hutoa bila kutegemea kupokea au kupokea bila kutegemea kutoa? Ukitaka kujibu swali hili vizuri, jiulize. Kama mwenzio asingekuwapo kwa sababu yoyote iwayo, hali ingekuwaje? Kama hujui jua. Utoacho ndiyo upatacho toka kwa mwenzako. Ujue pia kuwa yote hutegemea nawe mwenyewe kwa vile kila ufanyacho kwa mwenzio, unajifanyia mwenyewe.
            Waingereza wana msemo kuwa ukitenda wema, utakurudia na ukitenda ubaya, utazunguka na kukuridia pia. Hivyo, elewa. Ukimpenda mwenzio, unajipenda. Pia, ukimchukia, unajichukia. Kadhalika, ukimnya haki au kumdhulumu, unajinyima haki na kujidhulumu mwenyewe. Nini faida ya kufanya hivyo ilihali unajua utapata matokeo yale yale hasa kwa upande wa kudhulumiana au kuumizana?
 Tumalizie kwa kurejea kwenye kuishi pamoja na kupeana ‘chakula cha usiku.’ Lazima mjue. Kupata au kutoa ni nini zaidi ya vile tutoavyo? Lazima kukubali kuwa utapata kadri utoavyo na kukosa kwa kadri usivyotoa. Kila chakula uhitaji maandalizi. Na kula  kadhalika. Mfano, kama hujamlainisha, hutaingia, na kama hatakulainisha, waweza kuingia kwa maumivu mwishowe chakula kikakosa radha. Tunadhani tunaeleweka. Kwanini msilainishane ili wote mpate mkitakacho?
Kila mnachofanyiana kinachokubalika ni haki kwenu sawia. Kadhalika, kila mnachonyimana ni dhuluma sawia.
Chanzo: Mwananchi Jpli juzi.

No comments: