Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Monday 5 December 2011

Muuza gongo avishwa gamba Lake

Wenzenu baada ya kuona wenzetu kule Idodomya wakidanganyana na kuudanganya umma kuwa wanaweza kufua nguo zao na kuosha miili yao watakata na harufu iwatoke, sisi wanywa gongo tuliamua kufanya kweli.

Kutokana na kuonekana kama hatuna akili kutokana na ulevi, muuza gongo wetu mama Betty na Mumewe Baba Jaki wamekuwa wakuibia pesa kila uchao. Mtu akishapiga kanywaji na kukamatika wao wanapiga sachi. Yesu! Utamsikia mama Betty akijisemea utadhani ana dini. Kweli siku za mwizi arobaini. Ikifika ya arobaini na moja ananaswa kama alivyonaswa baba Jaki hivi karibuni pale walevi tulipoamua kumvisha gamba.

Ingawa tunawashuku wauza gongo kuwa wezi wetu, tulijua fika mlevi mwenzetu aitwaye Edhard Ruwasha alikuwa ndiye mshirika mkuu wa baba Jaki. Maana, licha ya kuwa marafiki wa muda mrefu, wote wanasifika kuwa na tabia ya udokozi. Hivyo, basi, kumkamata baba Jaki, tulitishia kumchoma moto Edhard baada ya kugundua wizi mkubwa wa pombe zetu. Purukushani iliyofumka pale usiambiwe. Sikujua kuwa walevi kuna kipindi wanakuwa na akili kuliko hata walokole. Maana jeuri waliyo nayo si kutokana na gongo tu bali hata aina ya maisha wanayoishi.

Edhard akiwa hana hili wala lile, si Mzee Jongomeza akalianzisha. Alianza kwa kusema, “Jamani, mmesikia Chama Cha Magamba na Makobe (CCMM).” Hii ni CCMM. Tafadhali msiichanganye na kile chama tawala tusije kutoana macho bure. Najua ukikitaja kila mandata yatavamia kambi yetu na kuvuruga kila kitu.

Aliendelea, “Nasi hapa tuna magamba lazima leo yavuliwe piga ua.”
Mlevi Kambwiriri aliungana na wazo la Mzee Jongomeza. Alisema, “Mwanangu umenena hapa. Maana nasi hapa kambini tuna magamba manene kama ya CCMM. Lazima leo yavuliwa na kuchomwa moto ili tuanze kula vyetu kwa usalama na raha zetu.”

Kwa ufupi ni kwamba, baada ya kusikia Chama Cha Makobe au Magamba kuja na mkakati wa kisanii wa kuvishana magamba na kuvuana nguo kwa kisingizio cha kuvua gamba, nasi walevi tuliona hii ndiyo nafasi adimu ya kuvuana magamba kwenye manywaji yetu. Tulipania wadokozi wote wa mapupu na utumbo pale mezani wapewe vipande vyao bila kumsaza baba Jaki anayetumalizia vyetu akishirikiana na Ruwasha.

Tulipoanza kupiga zegere si baba Jaki kajiingiza akijifanya mtu mwema kutaka mhusika achomwe moto asijue naye ni mmoja wapo. Baada ya Ruwasha kuona anaweza kuwashwa akaamua kumwaga mtama. Alisikika akisema, “Jamani mnanionea na mtaninyotoa roho bure. Mei huwa natumwa na baba Jaki mwenye mali zake. Mie kweli ni kibaka lakini mipango yote ya kuwachomolea vijisimu na fedha hufanywa na baba Jaki mwenyewe.”

Alimgeukia baba Jaki na kusema, “Baba Jaki, kweli tunafanyiana hivi ndugu yangu wakati vyote nichomoavyo huvichukua wewe na kuishia kunipa gongo kidogo?”
Baba Jaki anainama chini akitafuta jinsi ya kujitetea.

Kabla ya kujibu, Ruwasha anaendelea, “Baba Jaki hujui kama siyo mimi kutunza siri zako ungeishakufa zamani? Kumbuka mwaka jana ilipoibiwa simu ya mlevi wa kizungu ya bei mbaya walevi walikushuku na kama si mie kuuchuna unadhani ungekuwa hapo zaidi ya kaburini?”

Wote tulipigwa butwaa kwa ufunuo wa Ruwasha ambaye mara zote alipotuhumiwa alikuwa akikaa kimya tusijue ana mengi. Nakumbuka kipindi kile ilipoibiwa simu ya bei mbaya ya mtasha, Ruwasha alipigwa nusu kufa. Nakumbuka walevi walisema kuwa alipokea kipigo chote hicho na kuhimili ili kumlinda baba Jaki ambaye kumlipa fidia alikuwa akimpa mapupu kila alipokuja kupata kanywaji. Kutokana na tabia ya Ruwasha kumlinda baba Jaki, walevi walifikia kutoa hitimisho kuwa hata baba Jaki akiamua kumchukua mke wa Ruwasha asingemfanya kitu.

Sasa juzi Ruwasha alipoamua kuzoboka mbona wengi tulipigwa na kihoro si kawaida ingawa tulijua baba Jaki ni kibaka lakini hatukutegemea Ruwasha amvishe gamba lake kirahisi na haraka hivi hasa ikichukuliwa kuwa Ruwasha siku zote alikuwa akionekana mdumizi wa kawaida.

Wakati kimbembe kikiendelea, si baba Jaki akataka kutuingiza mkenge, aliamua kuweka muziki wa Katitu ili midundo yake ituchanganye tusimdunde.

Hiyo haikufua dafu. Kwani mlevi Mgigisi aliamua kuanza kumtwisha baba Jaki mandoo na mitama kama hana akili nzuri. Jamaa alimkwida na kuanza kumtembezea kichapo si kawaida. Mkewe mama Betty kuona hali imechafuka, alikusanya pesa aliyokuwa keshapata na kuishia mitini huku akiacha mmewe anapigwa kama kibaka. Na kama si busara za mzee Mburuma, basi baba Jaki angekuwa maiti. Maana walevi walishaamua kumtia moto baada ya kumvisha gunia ambalo lilichukua nafasi ya gamba.

Kama si baba Jaki kuapa na kuahidi kuwa hatarudia na ataendelea kutupa gongo bure walevi, angekuwa marehemu au mwendazake kwa lugha za kimambasa. Amshukuru Mungu kuwa walevi wakiona gongo akili zao huruka kichwani na kubakia wapwakiaji wa kawaida kama ilivyotokea. Hata hivyo, kwa adhabu na kipigo alichopata baba Jaki, nadhani wote wenye tabia kama yake popote walipo wamepata somo. Hata kama wapo wenye tabia chafu kama zake wanaoendelea kupeta kutokana na waathirika wao kuwa majuha, arobaini yao ikifika watachapwa vilivyo. Kipopo chawangoja. Kunusurika kipigo na kuvishwa gamba na gunia ni kuachana na ujanja wa kizamani wa mbuni kumuona adui akafutika kichwa ubawani akidhani na adui atakuwa juha kama yeye. Je wako wangapi wanaowafanyia walevi wao vitu kama hivi? Naona yule anasoma na kusonya kutokana na chama chake kuwa na tabia kama hiyo. Hapa dawa si kusonya au kumchukia mlevi bure. Dawa ni kutia akili na kujua watu wanabadilika. Mwenye masikio na asikie na mwenye akili na atie akilini mapema kabla hajavishwa gamba na kutwishwa mindoo huku akikatwa mtama. Tena wengine ni waheshimiwa. Yakiwakuta haya watakufa kwa ugonjwa wa moyo kama baba Jaki ambaye tangu aumbuliwe anaonekana mwenye mawazo mengi. Hata zile bashasha zake zimetoweka na nafasi yake imechukuliwa na aibu.

Kwa vile nimechonga sana, ngoja nikapate lau chupa moja nizimue akili.

Chanzo: Dira Desemba 5, 2011.

No comments: